UHALIFU UACHENI: La sivyo mtachakaa, mkishatiwa mbaroni

NA LWANGA MWAMBANDE

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewaua wahalifu sita (Panya Road) waliokuwa wakielekea eneo la Goba katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kufanya uhalifu Septemba 17,2022

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum, Jumanne Muliro amesema, baada ya taarifa kutoka kwa raia wema, walibaini wahalifu hao walikuwa kwenye gari aina ya Noah kutoka eneo la Mabibo kuelekea Goba kufanya uhalifu na ndipo walipowakamatia eneo la Makongo Area 4.

Amesema, eneo la tukio waliweza kukamata mapanga tisa, na kisu kimoja na dhana za kuvunjia katika matukio mbalimbali.

Mshairi wa kisasa,Bw.Lwaga Mwambande anaendelea kusisitiza kuwa, yeyote ambaye anajifanya kuwa hodari wa kutekeleza vitendo vya kihalifu,anapaswa kuaga familia yake kabisa, kwa kuwa kuna mawili aidha kuuawa au kutiwa mbaroni ambako huko atanyooshwa kisawasawa, jifunze kupitia shairi hapa chini;


1:Wahalifu sikizeni, ondokeni mitaani,
Mwajitia hatarini, ni pingu ziko njiani,
Kufika mahakamani, kwenu hiyo ahueni,
Panya Road mitaani, uhalifu uacheni.

2:Mambo ya kuumizana, mkija kwetu nyumbani,
Na tena kuibiana, kuleta umasikini,
Hayo yatutaki tena, hebu rudini nyumbani,
Panya Road mitaani, uhalifu uacheni.

3:Tena mmeenda mbali, mwatutia mautini,
Haramu kwetu halali, mwatutia msambweni,
Kuna la mgambo kweli, mtatiwa hatiani,
Panya Road mitaani, uhalifu uacheni.

4:Maonyo yametolewa, kwa kila pande nchini,
Kama yameshasikiwa, kwetu sote ni Amani,
Kama yadharauliwa, machozi yako njiani,
Panya Road mitaani, uhalifu uacheni.

5:Serikali yetu hii, iliyo madarakani,
Yataka muwe watii, na muishi kwa amani,
Mipango bajeti hii, kwa vijana ni makini,
Panya Road mitaani, uhalifu uacheni.

6:Ni mtaa kwa mtaa, msako uko njiani,
Kote kule mnakaa, ni bora tawanyikeni,
La sivyo mtachakaa, mkishatiwa mbaroni,
Panya Road mitaani, uhalifu uacheni.

7:Panya Road mitaani, ni hamasa mitaani,
Tusiwe usingizini, sungusungu ni kazini,
Tukutane viwanjani, huko tutoane soni,
Panya Road mitaani, uhalifu uacheni.

8:Dar Salamu zikizeni, hebu rudini nyumbani,
Na tena kwa wenye dini, mnajitia dhambini,
Kwa Mungu wenu tubuni, mkaishi kwa amani,
Panya Road mitaani, uhalifu uacheni.

9:Wito pia kwa wazazi, wenye watoto nyumbani,
Hebu fanya uchunguzi, mienendo ya nyumbani,
Hayo hasa ni malezi, wasikumbwe mitaani,
Panya Road mitaani, uhalifu uacheni.

10:La mgambo limelia, wahalifu mitaani,
Vituko vyenu achia, mwajitia kitanzini,
Rungu kubwa lawajia, hamtapata Amani,
Panya Road mitaani, uhalifu uacheni.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments