ACT Wazalendo ni sauti mbadala-Mheshimiwa Othman

NA MWANDISHI WETU

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, amesema chama chake kimejipambanua kuwa ni sauti mbadala kwa wananchi.
Mhe. Othman, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameyasema hayo leo huko Jang'ombe, Mkoa wa Mjini (Kichama), akizungumza na viongozi wa chama hicho, katika ziara maalum ya kuimarisha chama kwa majimbo ya Zanzibar.

Amesema, kwa miaka mingi wananchi walio wengi walikuwa wamekosa sehemu sahihi ya kusemea mambo yao, hivyo sauti mbadala ya wananchi kwasasa ni chama cha ACT Wazalendo.
Mhe. Othman ameeleza azma ya chama chao kwamba mbali na kuwatetea wananchi katika yale wanayopaswa kufanyiwa na Serikali, lakini pia watasimamia katika kuwapatia maisha bora yanayostahili.

"Wala hakuna haja ya serikali kukasirika pindi wananchi au sauti mbadala ikieleza kwani kutekeleza matakwa ya wananchi ni sehemu ya uwajibikaji unaohitajika,"amesisitiza Mhe. Othman.
Kuhusu wanaohoji juu ya chama chao kuwa sehemu ya serikali wanayoikosoa, Mhe. Othman amesema ACT Wazalendo kuwepo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa sio ihsani bali ni matakwa ya kikatiba, na watasifu panaposifika na watakosoa panapostahiki kwani “serikali ni mali ya wananchi na sio ya chama cha siasa.“

"ACT ipo kwenye serikali kwa sababu tunataka kuirekebisha Zanzibar, na tutahakikisha heshima ya nchi inarudi, kutakuwa na uwajibikaji kwa viongozi na kuwepo chaguzi za haki na ustaarabu," amesisitiza Mhe. Othman.
Makamu Mwenyekiti huyo amesema katika kutekeleza hilo, chama chake kimeanzisha wasemaji wa kisekta ambao ni mawaziri kivuli nje ya serikali waliopewa jukumu la kufuatilia mwenendo wa serikali na kutoa njia mbadala kwa namna inavyostahili.

Amesema Zanzibar ni nchi yenye utajiri mkubwa na iliyokuwa na mamlaka yake kamili, na kama hapatokuwepo sauti mbadala yenye kueleza uhalisia, basi hali ya maisha itazidi kuwa ngumu.

Naye Mjumbe wa Kamati Kuu wa chama hicho, Ndugu Ismail Jussa Ladhu, amesema njia pekee ya kuijenga Zanzibar ni siasa za kistaarabu, uwajibikaji wa viongozi wa umma na kuwa na mamlaka yake kamili.
Akisoma risala kwa niaba ya chama jimboni humo, Kaimu Katibu, Ndugu Ali Miraji, amesema jimbo hilo lenye idadi ya shehia tano, wadi mbili na matawi saba, kwa sasa limejikita katika shughuli za ujenzi wa chama na wapo tayari kupokea maagizo yoyote kutoka ngazi za juu ya kuyatekeleza.

"Mhe. Makamu wa Kwanza wa Rais, jimbo letu lina idadi kubwa ya vijana ambao wapo tayari kupokea maagizo ya chama, na hii ni ishara kubwa kwamba vijana wamekipokea chama na vijana ndio tumaini letu,“alisema Naibu Katibu huyo.

Viongozi mbalimbali kutoka ngazi ya jimbo mkoa na Taifa wakiongozwa na Kaimu Naibu Katibu Mkuu Ndg. Salim Bimani, wameambatana na Makamu Mwenyekiti katika katika ziara hio ya ujenzi wa Chama, inayoendelea tena jioni ya leo katika jimbo la Mpendae.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news