'Waliotukeketa wilayani Serengeti wawajibishwe'

NA FRESHA KINASA

WASICHANA watano kutoka familia tofauti tofauti katika Wilaya ya Serengeti mkoani Mara waliofanyiwa ukatili wa kijinsia kwa kukeketwa hivi karibuni ambao kwa sasa wanapatiwa hifadhi katika Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama kinachomilikiwa na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania la mkoani Mara wameiomba Serikali kuwachukua hatua kali za kisheria kwa kuwawajibisha vikali waliowafanyia ukatili huo.
Wengi wao wakiwa na umri mdogo kati ya miaka 8-16 katika mahojiano maalum na DIRAMAKINI wamesema, lazima ukeketaji upigwe vita kwa nguvu zote na kila mmoja.

Pia Serikali ihakikishe inatoa adhabu kali kwa wahusika wanaobainika kuwakeketa wasichana kutokana na madhara yatokanayo na kitendo hicho ambacho huchangia kukatisha masomo yao, kwani wanapokeketwa huandaliwa kuozeshwa katika umri mdogo na kupelekea washindwe kutimiza ndoto zao.

Wameyasema hayo Septemba 2, 2022 wakati wakizungumza na DIRAMAKINI kituoni hapo, ambapo wamesema, wasichana wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika masomo yao sawa na watoto wa kiume na kufika mbali na kuja kuleta maendeleo thabiti katika nyanja ya kiuchimi na kijamii kwa siku za usoni iwapo watawezeshwa, kulindwa na kuthaminiwa kuanzia ngazi ya familia.

Wameongeza kuwa, kuna mbinu mpya ya ukeketaji inayotumiwa na wazazi ambapo ngariba wanasafirishwa kwa bodaboda usiku na kufanya ukeketaji tofauti na awali ambapo ngariba alikuwa anasubiria wasichana kwenye kibaga (eneo la kukeketa), lakini kwa sasa ngariba hupita usiku katika familia ambapo kuna msichana anayetakiwa kukeketwa wakikwepa kukamatwa. Hivyo Serikali wameomba iongeze mbinu za kukabiliana nao ili kuwanusuru wengi dhidi ya kadhia hiyo.

"Nilikuwa naishi na mama mdogo, Baba na Bibi nyumbani, Baba alikuwa hapendi nikeketwe, lakini bibi akamshauri Baba nikeketwe Baba akakubali wakaandaa mpango ilikuwa ni mchana mwezi wa nane sikumbuki siku ( Agosti) mwaka huu, Baba akatoka kazini ni fundi viatu Mjini Mugumu hapa Mtaa wa Sedeko alipofika nyumbani nikaitwa akasema ni lazima nikeketwe, nikasema siwezi kwani nilikuwa nimeshafahamu madhara ya ukeketaji nikiwa shule nasoma kabla hajaniachisha mwezi Juni, 2022 nilikuwa nasoma Mapinduzi Day kidato cha kwanza.

"Nikakataa akasema tayari ameshamlipa ngariba hela na ngariba huyo atakuja muda wowote akaniambia nioge akasema yeye anarudi kazini hata kama hatakuwepo Bibi atashughulika ilipofika jioni Baba akatoka kazini akakuta ngariba hajafika nyumbani akampigia simu huyo ngariba akasema yuko mbali,

"Baba akaniambia twende kwa rafiki yake eneo la mnada mpya na ngariba atakuwa huko mimi muda huo nilikuwa nasonga ugali nikaamuriwa niache kupika akachukua vitenge na wembe akamuita bodaboda akanipandisha tukaenda mpaka kwa rafiki yake na baba yangu,"amesema Mbendo (si jina lake halisi) na kuongeza kuwa,

"Tulipofika tukamkuta ngariba akiwa na mzee wa kimila wamekaa wakanichukua wakanipeleka kichakani jirani na nyumba ya rafiki yake na Baba yangu nikakeketwa baada ya kukeketwa nikafungwa kitenge na kupakwa unga sehemu iliyokatwa mzee wa kimila akanichapa miguu na kichwa ndipo tena nikapanda bodaboda kurudi nyumbani tulifika saa tatu usiku nyumbani. Kesho yake asubuhi nimemaliza kunywa uji baba akampigia simu mama mdogo ambaye ndie ninaishi naye baada ya mama yangu mzazi kuachana na Baba.

"Akamwambia, anitoe nyumbani anipeleke kwa Baba mkubwa wangu ni jirani tu nikaenda kwa Baba mkubwa nikakaa pale baadaye Polisi walikuja nyumbani kwetu wakamkuta Baba ametoka kazini alipowaona akataka kukimbia wakamkamata na kumhoji mimi niko wapi? Akasema nimesafiri wakamwambia asiwadanganye aseme ukweli.

"Wakakagua ndani hawakunipata akawaambia ndipo akawaambia nipo kwa Baba mkubwa wakaja wote wakiwa na Baba wakanikuta tulikuwa wawili tumekaa wakahoji jina langu Kati ya wale wawili ( jina limehifadhiwa) nikaitikia wakanichukua na kunileta Hope Nyumba Salama. kwa kweli niliumia sana baada ya kukeketwa maana nilipata maumivu makali, nilitokwa damu nyingi nililia bila msaada." amesema Mbendo.

Naye Kolongezi miaka 14 ( si jina lake halisi) amesema alikeketwa kutokana na shinikizo la wazazi wake ambapo walimwambia asipokeketwa watamfanyia kitendo kibaya sana japo hakukubali, na ndipo ulipofanyika mpango wa siri akakeketwa usiku kwa kushitukizwa. Ambapo ameiomba serikali kuongeza ukubwa wa adhabu kwa wale wanaobainika kuwakeketa wasichana ili wawaozeshe na kuwakatisha masomo yao.
Mkuu wa Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama, Daniel Misoji amesema kuwa mpaka sasa Kituo hicho kimepokea wasichana 65 katika kipindi cha mwezi mmoja kati ya hao 65, watano wamekeketwa tayari ambapo walipelekwa hospitalini kuchunguzwa na kupewa matibabu.

Na tangu Julai 28,2022 wameendelea kutoa programu za masomo ya Sekondari na Msingi kwa wasichana hao wakiwa kituoni hapo kwa mfumo wa Tuition.

"Tumekuwa tukipokea wasichana kutoka Ustawi na Dawati la Jinsia na Watoto ambao huokolewa wakiwa katika hatari ya kutaka kukeketwa wakifika hapa kituoni tunawapa chakula, nguo, ushauri wa kisaikolojia, elimu ya ukatili wa kijinsia, tunawafundisha haki za watoto, tunawapa hifadhi ya kulala na chakula muda wote kabla ya kuwarudishwa kwao msimu wa ukeketaji unapoisha kwa makabidhiano ya kisheria na wazazi wao.

"Na tuliowapokea ndani ya mwezi mmoja wengi wao wana umri wa miaka 8-16 kutoka Kata ya Kebanchabancha, Mosongo, Nyamoko,Sedeko, Nyansurura Rung'abure, pia hivi sasa shule zinapoelekea kufunguliwa tumejiandaa kuwarudisha makwao kwa kwenda kujenga mahusiano na wazazi wao tukiwa na watu wa Ustawi wa Jamii, Dawati la Jinsia na watoto, maendeleo ya jamii na shirika la Hope tunawapa mahitaji ya shule kama madaftari, kalamu ili kuhakikisha wanasoma kufikia ndoto zao,"amesema Daniel Misoji.

"Tumekuwa tukipokea wasichana ambao huletwa katika Kituo hiki kutoka kwa Dawati la Jinsia na Watoto Polisi, Ustawi wa Jamii na madai ya kwamba shirika hukamata wasichana na kuwaleta hapa kituoni kwa nguvu si kweli sisi hatuna mamlaka ya kufanya hivyo na jamii itambue hivyo.

"Vipo vyombo ambavyo kisheria vinawaleta hapa na wanapofika kuna fomu maalumu wanajaza kuonesha kuwalinda watoto tunafuata taratibu zote za kisheria na viongozi wa Serikali hufika hapa kituoni kuona watoto hawa na wanatupa ushirikiano mzuri sana katika kuhakikisha tunatokomeza ukeketaji Serengeti,"amesema Misoji.

Daniel ameishukuru Serikali wilayani Serengeti kwa kuendelea kulipa ushirikiano wa dhati Shirika la Hope katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwemo kufanya kazi kwa karibu kutoa elimu ya madhara ya ukatili wa kijinsia kwa jamii katika kuhakikisha wanakuwa salama.
Dkt.Joachim Eyembe ni Daktari Bingwa wa Upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara akizungumza na DIRAMAKINI amesema, madhara ya ukeketaji ni pamoja na mama kutokwa damu nyingi wakati wa kujifungua hali ambayo inaweza kusababisha kupoteza maisha, maumivu makali wakati wa kukeketwa, hatari ya kupata magonjwa ya kuambukiza ( UKIMWI), mama kutopata raha wakati wa tendo la ndoa, na kuathiri ka kisaikolojia kutokana na kufanyiwa kitendo hicho.

Jacob Lutubija ni Askofu wa Kanisa la Tanzania Missionary Revival Church (TMRC) lililopo Kata ya Kigera Manispaa ya Musoma ambapo akizungumza na DIRAMAKINI amesema, ukeketaji haufai, badala yake jamii imheshimu Mungu na kuacha kufanyiana vitendo vinavyoumiza nafsi na kwamba watu waishi maisha ya kuthaminiana na kupendana sambamba na kumpendeza Mungu na sio kufanyiana ukatili kwani Neno la Mungu halijaagiza hivyo hata kidogo.

Neema Yusto na Jenepher Peter ni wakazi wa Mugumu Wilaya ya Serengeti wamelipongeza Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania kwa kutoa hifadhi kwa wasichana ambao hukimbia ukeketaji, wamesema licha ya Serikali kuendelea kukemea vikali mila hiyo bado kuna watu wanakeketa watoto wao wa kike kama sehemu ya kujipatia kipato kwani binti akikeketwa huozeshwa wazazi hupata mali (mifugo), wamesisitiza wazazi na walezi wawasomeshe watoto wa kike kwani urithi pekee usioharibika ni elimu.
Agosti 27, 2022 katika kikao cha baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Mkuu wa wilaya hiyo, Mheshimiwa Dkt.Vincent Mashinji alisema kuwa, suala la ukeketaji linaendelea kufanyika wilayani humo na kwamba Serikali haitaki kuona kitendo hicho kikifanyika na itaendelea kuwachukulia hatua za kisheria wahusika wote kwani hakifai na ni kinyume cha sheria na viongozi washiriki kukemea ukeketaji katika maeneo yao.

"Suala moja kubwa ambalo linatusumbua kichwa hivi sasa ni suala la ukeketaji, zoezi linaendelea huko mtaani watu wanakeketana ninajua ni suala gumu kuliongelea maana ni mila na ni mapokeo ya toka enzi na enzi...tunatokaje huko kwenye hili. Kuna watu wamezoea na kuna watu wanasema lifike mwisho kuna wanao kubali kuna wanaokataa. Msimamo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukeketaji ni marufuku," alisema Dakt. Mashinji katika baraza hilo la madiwani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news