Waziri Dkt.Kijaji aagiza Kiwanda cha 21th Century Morogoro kufanya kazi saa 24

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Uwekezaji,Viwanda na Biashara,Mheshimiwa Dkt.Ashatu Kijaji amewataka wafanyakazi wa Kiwanda cha nguo cha 21th Century kilichopo mkoani Morogoro kuendelea kufanya kazi saa 24 kwa siku saba, kwa kuwa Serikali inaendelea kutatua changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika kiwanda hicho bila kupunguza wafanyakazi au kufunga kiwanda.
Mheshimiwa Dkt.Kijaji ameyasema hayo baada ya kufanya ziara katika kiwanda hicho Septemba 17, 2022 ambapo amesema kuwa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/220 imeitaka Serikali kuendeleza viwanda vilivyopo na kufufua vilivyokufa ili kuweza kutengeneza ajira za watanzania milioni saba, hivyo Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan haipo tayari kuona kiwanda hicho kinafungwa.

Dkt.Kijaji pia amesema, Serikali ipo tayari kushirikiana na kiwanda hicho kutatua changamoto mbalimbali zilizowasilishwa zikiwemo kukatika kwa nishati ya umeme, maji pamoja na kuchukua hatua kwa wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa za nguo kinyemela nchini bila kulipa kodi na kuleta ushindani wa kibiashara baina yao na viwanda vya nguo nchini ikiwemo Kiwanda cha 21th Century Textile.
Aidha, ametoa ushauri kwa viongozi wa kiwanda hicho kuacha tabia ya kulalamika juu ya upungufu wa maji isipokuwa wajaribu kutumia njia ya (recycling) ya kutumia maji yaliyopo na sio kuyaacha yakipotea bila sababu ya msingi na kuzingatia ubora wa bidhaa zinazozalishwa kiwandani hapo ili kuweza kuendana na ushindani wa soko la kimataifa

Akitoa taarifa za utekelezaji wa Kiwanda hicho cha Afisa Sheria na Utawala wa Kiwanda hicho, Bw. Nicodemus Mwaipungu amesema kuwa kiwanda hicho kimetoa ajira za kudumu zaidi ya 2,400 kwa watanzania ila kinaweza kutoa hadi ajira 3,000 lakini kutokana na changamoto za maji, umeme pamoja na ushidani wa kibiashara unaosababishwa na uingizwaji kinyemela wa bidhaa nchini bila kulipia kodi.

Mwaipungu ameiomba Serikali kusaidia kupambana na waingizaji haramu wa bidha za nguo ambao wamekuwa wakiuza kwa bei ndogo na kusababisha kiwanda hicho kutofanya bishara kama ambavyo inatarajiwa.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi TUICO Kiwandani hapo, Bw. Halfani Mahamudu ameiomba Serikali kuongeza nguvu kutatua changamoto zinazokikabili kiwanda hicho ili kunusuru ajira za Watanzania 2400 ambazo zipo hatarini kutoweka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news