DAR NI SALAMA: 'Panya road' sita wauawa

NA DIRAMAKINI

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewaua wahalifu sita (Panya Road) waliokuwa wakielekea eneo la Goba katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kufanya uhalifu Septemba 17,2022
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum, Jumanne Muliro amesema, baada ya taarifa kutoka kwa raia wema, walibaini wahalifu hao walikuwa kwenye gari aina ya Noah kutoka eneo la Mabibo kuelekea Goba kufanya uhalifu na ndipo walipowakamatia eneo la Makongo Area 4.

"Tuliweka mtego, na tuliwasimamisha eneo la Makongo, na walikuwemo watuhumiwa tisa wa ujambazi maarufu Panya Road wakiwa na vifaa vya jadi, walitoka na mapanga ndani ya Noah hiyo kwa lengo la kutoroka chini ya ulinzi.

"Askari waliwatadharisha na kujihami, na kupiga risasi juu, na kutaka kila njia wasitoroke, lakini katika purukushani hizo sita walijeruhiwa vibaya na watatu wakatoroka, wahalifu hao sita walipeleka hospitali, lakini wakapoteza maisha,"amesema Kamanda Muliro.

Pia Kamanda Muliro amesema, eneo la tukio waliweza kukamata mapanga tisa, na kisu kimoja na dhana za kuvunjia katika matukio mbalimbali.

"Uchunguzi wa awali kwa watuhumiwa hao umebaini kuwa, miongoni ni viongozi wa makundi hayo ya kutumia silaha, na wapo waliopata kuhukumiwa na kutoka kisheria,"amesema Kamanda Muliro.

Kamanda Muliro amewataja waliotambulika kati ya waliopoteza maisha kuwa ni Salum Juma (Babu Salum) umri kati ya miaka 20-27 mkazi wa Mbagala.

Pia mwingine ni Khalifa Khalifa mkazi wa Buguruni ambaye naye inaonesha aliwahi kukamatwa kwa makosa ya uhalifu wa kutumia mapanga jijini Dar es Salaam.

Aidha, amebainisha katika upelelezi umebaini kuwa, vinara hao walishiriki kwenye tukio la Kawe na eneo la Buguruni kwa kuiba na kuua.

Kamanda Jumanne Muliro amesema, Jeshi la Polisi linaendelea kutekeleza kwa haraka agizo lililotolewa na Mkuu wa Jeshi hilo la kuwashughulikia wahalifu nchini huku akiwataka wananchi kutokuwa na hofu yoyote, kwani chini ya vyombo vya ulinzi na usalama jijini hilo na Tanzania kwa ujumla ni salama.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news