Waziri Dkt.Mabula awapa 'assignment' wadau wa uendelezaji milki nchini

NA GODFREY NNKO

UHABA mkubwa wa nyumba hususani zile bora na za gharama nafuu ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili Sekta ya Milki nchini Tanzania.
Hayo yamesemwa leo Septemba 1, 2022 na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula wakati akifungua mkutano wa wadau wa uendelezaji milki nchini unaofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku mbili.

Amesema, kwa nyakati tofauti Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali ili kuchochea ukuaji wa sekta ya miliki nchini ambazo zimewezesha matokeo makubwa katika sekta hiyo.

"Matokeo hayo ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya miradi ya uendelezaji milki, sisi sote ni mashuhuda wa uendelezaji mkubwa wa majengo unaoendelea hususani kwenye maeneo ya miji na majiji, mashirika kuongeza tengeo la uwekezaji kwenye Sekta ya Milki mfano, PSSSF, NSSF, NIC, NHC.

"Pia taasisi za nje kushiriki katika uwekezaji kwenye sekta ya nyumba mathalani kampuni kama Avic Town, Palm Village na nyinginezo ikiwemo kukua kwa uwekezaji wa ndani, kuongezeka kwa idadi ya benki na taasisi za fedha zinazowekeza kwenye sekta ya milki toka benki tatu zilizokuwa zikitoa mikopo ya nyumba mwaka 2009 hadi benki 33 sasa na kujitokeza kwa makampuni binafsi ya upangaji na upimaji ardhi.

"Licha ya mafanikio hayo, bado Sekta ya Milki imekuwa na changamoto kadhaa mojawapo ikiwa ni uhaba mkubwa wa nyumba hususani nyumba bora na za gharama nafuu. Nchi yetu inakadiriwa kuwa na upungufu wa takribani nyumba milioni tatu na ongezeko la mahitaji ya wastani wa takribani nyumba 200,000 kila mwaka,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula.

Pia Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amesema,kasi ya taasisi za uendelezaji milki kuzalisha nyumba bado ni ndogo.

"Takwimu zinaonesha kuwa kuanzia mwaka 2010 hadi 2022,taasisi kubwa nane zimefanikiwa kujenga nyumba takribani 13,837 tu, sawa na wastani wa nyumba 1,153 kwa mwaka.

"Tukumbuke pia zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linaloendelea nchini litaiwezesha Serikali kuwa na kanzidata ya nyumba zote nchini, hivyo kupata takwimu sahihi za upungufu wa nyumba nchini. Hii itafungua fursa zaidi ya kujua mahitaji halisi ya nyumba kwa kila mwaka,"amesema Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amesema kuwa,pamoja na jitihada za Serikali za ujenzi wa nyumba za makazi zenye gharama nafuu bado kumekuwa na malalamiko kwa baadhi ya wananchi wanaodai kushindwa kumudu hitaji hilo kutokana na gharama za juu.

Amesema, suala hilo linapaswa kuangaliwa kwa umakini, kwani linawafanya watu wengi kudhani kwamba Serikali haiwasaidii kitu ambacho ni kinyume kwani hujiridhisha kulingana na aina na ubora wa nyumba kabla ya kupanga bei husika.

“Mtu anasema hizi nyumba zina gharama kubwa, lakini swali la kujiuliza ni je? Analinganisha kwa mtazamo upi, maana lengo la serikali nikutaka watu wake waishi katika nyumba bora sasa katika eneo hili ni vyema pia wadau mkaja na maoni katika mjadala wenu,"amesema Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula.

Ameongeza kuwa, Serikali inalenga kuwawezesha wananchi kuwa na makazi bora yaliyo katika hadhi kama inavyokusudiwa na wizara na kwa mujibu wa sera na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 Ibara ya 76.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amesema,chama kimeelekeza Serikali kujenga mazingira ya kuwawezesha wananchi nchini kujenga nyumba bora na za gharama nafuu mijini na vijijini.

Pia ilani ya uchaguzi inaitaka Serikali kuhakikisha kuwa uboreshaji wa sekta unaenda sambamba na kuwa na sera mpya ya nyumba na maendeleo ya makazi. Suala ambalo litawafanya wananchi mijini na vijijini kujenga nyumba bora.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amesema, ujenzi huo unatarajia kuendana na uwepo wa huduma mbalimbali za kijamii za kimiundombinu ikiwemo barabara, maji vituo vya afya kwa kuweka jitihada za kufanikisha mikakati iliyokusudiwa.

“Tutahakikisha pia tunaanzisha mikopo ya nyumba kupitia sera wezeshi zilizowekwa na Serikali ili kuwa na uendelezaji wa milki kwa taasisi zilizopo ambazo sitasimamia zoezi zima la kuwainua Watanzania kuwa na makazi bora,”amesema Waziri Dkt.Mabula.

Waziri Dkt.Mabula ameongeza kuwa, upo umuhimu wa kuwekeza katika sekta ya milki na kufanya maboresho katika baadhi ya sheria nchini ili kuwa na sera ya nyumba yenye mazingira rafiki kwa wawekezaji na kuwafanya watu wengi kuishi katika nyumba za gharama nafuu.

“Kutokana na jitihada hizi sasa kuna ongezeko la miradi na sisi ni mashuhuda wa ujenzi unaoendelea kufanywa na mashirika mbalimbali ikiwemo NSSF, NHC na mengineyo yenye lengo la kuziwezesha jamii kuwa na makazi bora,” amebainisha Dkt. Mabula.

Katibu Mkuu

Awali Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Allan Kijazi wakati akimkaribisha Mheshimiwa Waziri, Dkt.Mabula amesema kuwa, sekta hiyo ina fursa kubwa na ina nafasi ya kuchangia uchumi wa nchi.
"Kikao hiki tumekiitisha kwa kutambua umuhimu wa Sekta ya Miliki katika uchumi wa Taifa, ukiangalia takwimu za mataifa mbalimbali utaona wazi kwamba sekta ya miliki ina fursa kubwa sana ya kuchangia uchumi wa nchi yoyote.

"Lakini kwa bahati mbaya kwa upande wa nchi yetu, bado sekta hii mchango wake ni mdogo, ndiyo tukaona kuna haja ya kukutana ili kujadiliana tuweze kufahamu tatizo liko wapi, tujipange vipi na tuendelee kushirikiana vipi ili kuhakikisha kwamba mchango wa sekta hii katika uchumi wa Taifa unazidi kuongezeka.

"Ukizingatia kwamba Dunia imebadilika, ushindani wa kiuchumi ni mkubwa na hakuna budi kwa kila nchi kujitathimini kuangalia maeneo ambayo kuna maboresho ambayo yanahitajika ili kuchukua hatua,"amesema Dkt.Kijazi.

Dkt.Kijazi amesema, kusudio hilo pia linalenga kuhakikisha wanafikia mahitaji yaliyokusudiwa na Sekta ya milki nchini na kuibua changamoto na mikakati mipya itakayosaidia kusonga mbele.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news