WAZIRI MKUU AZINDUA MPANGO KABAMBE WA SEKTA YA UVUVI

*Asema mpango huo utakuwa chachu ya kuendeleza ukuaji wa uchumi wa buluu.

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Sekta ya Uvuvi utasaidia kukuza sekta hiyo na kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa hadi kufikia asilimia 10 kwa mwaka kutoka asilimia 1.8 ya sasa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizindua mpango kabambe wa Sekta ya Uvuvi utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka kumi na tano kuanzia 2021/2022 hadi 2036/2037, Kwenye ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Septemba 20, 2022. Kushoto ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki na kulia ni Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Dkt. Christina Ishengoma (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa mpango huo ambao utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka 15 kuanzia 2021/2022 hadi 2036/2037 unaumuhimu mkubwa katika ukuaji wa sekta ya uvuvi pamoja na Uchumi wa Buluu.

Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wadau wote wa sekta ya uvuvi kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa ina nia ya dhati ya kuhakikisha kila mmoja ananufaika na sekta hiyo.

Amesema hayo leo Septemba 20, 2022 wakati wa uzinduzi wa Mpango Kabambe wa Sekta ya Uvuvi, katika ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dar es Salaam. “Tutaendelea kupokea mapendekezo yenu ili tuweze kuboresha sekta hii, ubunifu wenu ni muhimu, wote tunataka tuzungumze lugha moja.”

Waziri Mkuu amesema kuwa mpango huo unaendana na maono ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuleta mapinduzi makubwa kwenye sekta zote ikiwemo sekta za uzalishaji. “Mpango huu utasaidia kwa kiwango kikubwa kutekeleza dhamira hiyo njema ya Mheshimiwa Rais, tunataka twende kwa kasi zaidi.”

Mheshimiwa Majaliwa amesema uwepo wa mipango mbalimbali katika sekta ya uvuvi utawezesha rasilimali hiyo kulindwa, kusimamiwa, kuendelezwa, kuhifadhiwa na kutumiwa kwa njia endelevu na hatimaye kuchangia kikamilifu katika kutoa ajira, kipato, chakula na lishe kwa jamii ya Watanzania kwa ujumla.

“Matumizi endelevu ya rasilimali ya uvuvi yanategemea sana uwepo wa mipango madhubuti ya kusimamia matumizi na uendelezaji wa rasilimali hizi.”

Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa utekelezaji wa mpango huo utakuwa chachu ya kuendeleza kasi ya ukuaji wa Sekta ya Uvuvi na utasaidia kuongeza kwa kiasi cha samaki na mazao ya uvuvi yaliyochakatwa na kusafirishwa nje ya nchi kwa asilimia 30.

“Mpango huu utakuwa chachu ya kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya uvuvi kutoka tani 473,592 hadi kufikia tani 639,092, sawa na ongezeko la asilimia 35.”

Aidha, Mheshimwa Majaliwa amezitaka Wizara na Taasisi zote za Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sekta Binafsi, Taasisi zisizo za Kiserikali, Madhehebu ya Dini pamoja na wadau wa maendeleo kupokea Mpango huo. “Uzingatieni mpango huu katika mipango yenu ya kisekta na kuendelea kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kufanikisha utekelezaji wake kwa maslahi mapana ya Taifa”

Naye, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema mpango huo utakuwa jumuishi na hautamuacha yeyote anayejishughulisha na sekta ya uvuvi. “Moja ya lengo la mpango huu ni kuongeza uwekezaji wa sekta binafsi na sekta ya umma, sekta binafsi karibuni muwekeze kwenye sekta hii kwa kushirikiana na shirika letu la Uvuvi.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Uvuvi Tanzania Profesa Yunus Mgaya amesema mpango huo utaleta maendeleo katika sekta ya uvuvi kwa kipindi cha miaka 15. “Mpango huu utasaidia kukuza uchumi wa buluu na kuvutia zaidi wawekezaji katika sekta hii ya uvuvi.”

Wakizungumza katika uzinduzi huo, wadau wa sekta ya uvuvi kwenye maji asili wamesema kuwa wameridhishwa na ushirikishwaji katika uandaaji wa mpango huo na wanaahidi kuutekeleza ili usaidie katika kukuza sekta hiyo.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Tipo Nyabenyi amesema wamefurahishwa kushirikishwa na Serikali katika uandaaji wa mpango huo ambao wanaamini kwa kiasi kikubwa utaleta mchango katika kutatua changamoto mbalimbali katika sekta hiyo.

“Kuwa na mpango na kutekeleza yaliyo kwenye mpango ni mambo mawili tofauti, ni imani yangu kuwa yale yaliyo kwenye mpango huu yatatekelezwa ili kuwa na maendeleo endelevu katika sekta ya uvuvi.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news