YA KENYATTA NI YA MOI, YA RUTO NI YA KIBAKI

NA LWAGA MWAMBANDE

JAMHURI ya Kenya ilifanya Uchaguzi wake mkuu Agosti 9, 2022, na kumchagua Dkt.William Ruto wa Muungano wa Kenya Kwanza kuwa Rais wa tano wa taifa hilo la Afrika Mashariki kwa kura milioni 7,176,141 sawa na asilimia 50.49.
Dkt.Ruto alimuangusha mwanasiasa mkongwe, Raila Odinga wa Muungano wa Azimio la Umoja aliyepata kura milioni 6,942,930 sawa na asilimia 48.85 ambapo alikuwa anagombea kwa mara ya tano na aliyekuwa anaungwa mkono na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Uhuru Kenyatta anayemaliza muda wake.

Huo ulikuwa ni uchaguzi wa saba wa mfumo wa vyama vingi na wa tatu tangu kuanzishwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC). Mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande anakushirikisha jambo muhimu kuhusu siasa za Kenya, endelea kupitia shairi hapa chini;

1. Ya Kenyatta ni ya Moi,
Ona ameachwa hoi,
Sasa ndio hakohoi,
Nyumbani aelekea.

2. Alidhania haboi,
Kumfanya Ruto toi,
Kumbe Baba goigoi,
Siasani apotea.

3. Sasa Ruto ainjoi,
Ameshapaa hapoi,
Ni Rais siyo toi,
Toroli linapepea.

4. Ya Ruto ni ya Kibaki,
Moi hakumuafiki,
Uhuru kampa tiki,
Watu walipotezea.

5. Elfu mbili na mbili,
Moi rais wa pili,
Litaka kufunga goli,
Uhuru kumtetea.

6. Alikivuruga chama,
KANU wengi wakahama,
Na Uhuru kasimama,
Mbele aweze sogea.

7. Limtaja himahima,
Kugombea kwenye chama,
Urais kusimama,
Ili kiti kutetea.

8. Wananchi kumuona,
Vichwa vyao wakakuna,
Kura zao hakuona,
Mbali akatelezea.

9. Kibaki akaibuka,
Urais akashika,
Moi akaaibika,
Kwa aliyemtetea.

10. Marais wana yao,
Na Wakenya wana yao,
Kura zao ndio ngao,
Kwa hizo wajitetea.

11. Hawaangalii sura,
Wanapozipiga kura,
Uchaguzi kwao bora,
Si amri kupokea.

12. Ona kwa miaka kumi,
Ruto amesaga lami,
Makamu mwenye usemi,
Kataka mpotezea.

13. Hendisheki kuingia,
Mbali kamfagilia,
Baba kamkumbatia,
Kuanza kumtetea.

14. Ruto akawekwa kando,
Asake yake mawindo,
Lionekana uvundo,
Ili aweze potea.

15. Kenyatta kamkumbatia,
Raila mfagilia,
Huku akifikiria,
Kijiti atapokea.

16. Wakenya limsikia,
Hata kumshangilia,
Huku wakifikiria,
Watavyompotezea.

17. Uchaguzi kuingia,
Nafasi akatumia,
Baba debe mpigia,
Kama mwana na bembea.

18. Sote tulimsikia,
Ruto akimsagia,
Ikulu hataingia,
Mbali atapotelea.

19. Ndivyo Moi alifanya,
Kibaki akimsonya,
Akidhani atasanya,
Kura za kumtoshea.

20. Wakenya achana nao,
Moyoni wanalo lao,
Wakampiga mabao,
Uhuru akapotea.

21. Sijui alisahau,
Ilivyochezwa nahau,
Kwamba yeye angalau,
Ruto singemzomea?

22. Yaliyomkuta yeye,
Alidhani yake yeye,
Kumbe liposhindwa yeye,
Raila atapotea.

23. Ya Moi ni ya Kenyatta,
Elimu bora kupata,
Rais unapopita,
Wengine acha zomea.

24. Pembeni kijikalia,
Kampeni kuangalia,
Mwisho utafurahia,
Mshindi tayetokea.

25. Ni katiba yambana,
Naye Ruto kuonana,
Jinsi walivyonangana,
Hana la kujitetea.

26. Miezi mepita kadha,
Pasi yao mawaidha,
Alimuona bughudha,
Ikulu anajongea.

27. Wakenya ni wakomavu,
Kura silaha ya nguvu,
Wanapiga kavukavu,
Uhuru amelegea.

28. Kizuri Ruto kasema,
Madaraka kisimama,
Atafanya mambo mema,
Bila mtu kuzomea.

29. Uhuru aende vema,
Kupumzika Bungoma,
Hata aje Dasalama,
Mafao atapokea.

30. Afrika Mashariki,
Kenya siasa zatiki,
Ya kwenu yana mantiki,
Darasa tunapokea.

31. Uwazi kutamalaki,
Mchakato umetiki,
Siri siri hamtaki,
Elimu tumepokea.

32. Vyombo vya habari pia,
Kweli tumefurahia,
Kubanwa tujasikia,
Habari metuletea.

33. Mahakama ya upeo,
Mnastahili cheo,
Hakuna upendeleo,
Yale mmetuletea.

34. Mahakama zetu pia,
Vema mkajifunzia,
Mazuri kutufanyia,
Tusije tukapotea.

35. Elimu imeingia,
Kazi kwetu kutumia,
Pazuri tutafikia,
Na nchi kuendelea.

36. Sasa tunawatakia,
Makubwa kujifanyia,
Mmeweze kufurahia.
Huyu Ruto kutokea.

37. Nchi ya watafutaji,
Muda kupata mtaji,
Myapate mahitaji,
Nchi ikiendelea.

38. Hasa ajira vijana,
Jinsi wanavyobanana,
Tutapenda kuwaona,
Shida zao zapotea.

39. Serikali za Kaunti,
Mzidi kujizatiti,
Huku mkipanda chati,
Wananchi kutetea.

40. Na pia mabunge yote,
Sasa mna nguvu zote,
Fanya mazuri yapite,
Kenya itaendelea.

41. Kenya ikisonga mbele,
Kwetu hakuna kelele,
Nasi tutasonga mbele,
Tuzidi kuendelea.

42. Afrika mashariki,
Chaguzi tumelaiki,
Nasi kwetu zikitiki,
Sote tutaendelea.

43. Lakini tukibakia,
Chaguzi tunabania,
Wimbo wa demokrasia,
Macho tutautolea.

44. Rais Ruto sikia,
Pale ulipoanzia,
Wengi tumefurahia,
Hebu mbele endelea.

45. Zaburi uliyosoma,
Kwa kweli mekaa vema,
Kwake Mungu kuegema,
Hili zidi kuchochea.

46. Wategemea magari,
Na silaha za hatari,
Wameishia sifuri,
Mungu amewatetea.

47. Sasa washika mpini,
Usianze ufitini,
Wengine ukahaini,
Amani ikapotea.

48. Vile umeahidia,
Heshima kuwapatia,
Uhuru kusambazia,
Vivyo hivyo endelea.

49. Sote twakuangalia,
Ahadi kutimizia,
Hapo nawe tazidia,
Hongera kujichotea.

50. Mungu ibariki Kenya,
Izidi mema kufanya,
Kusiwe na kutapanya,
Na mali zikapotea.

51. Uwe muda kukusanya,
Na mali nyingi kusanya,
Na majeraha kuponya,
Muweze kuendelea.

52. Marais huko Kenya,
Kazi zenu mkifanya,
Vyombo vya kwenu kusanya,
Huko kwenu endelea.

53. Kampeni kuwafanyia,
Wale mnafikiria,
Ulozi mwawafanyia,
Ona sasa wapotea.

54. Lichomfanyia baba,
Kwamba kura ziwe haba,
Sawa mama kule leba,
Mtoto akapotea.

55. Hapa alipofikia,
Baba bora kitulia,
Hekima kutupatia,
Chansi imeshapotea.

56. Yale ametufanyia,
Kwa kweli twafurahia,
Kenya ilipofikia,
Haki ameitetea.

57. Heri tunamtakia,
Huku akifikiria,
Kwanini hajafikia,
Pale juu kutokea.

58. Heshima bado anayo,
Anabaki baba huyo,
Ila urais kwiyo,
Ndiyo umeshapotea.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments