AWAMU HII TUNENE:Rais Samia wetu, Msalato amefika

NA LWAGA MWAMBANDE

OKTOBA 30, mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma.

Picha na constructionreviewonline.com

Hatua hiyo ni mwendelezo wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati na isiyo ya kimkakati inayofanikishwa kila kona ya nchi kupitia Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia.

Mheshimiwa Rais wakati akiweka jiwe hilo katika Kata ya Msalato jijini humo hakusita kutoa angalizo kwa Watanzania ambao wanapewa fursa za ajira katika maeneo ya miradi kuzingatia uaminifu, uadilifu na kuepuka vitendo vya udokozi wa vifaa ambao mara nyingi huwa unachangia kudhoofisha utekelezaji wa miradi husika.

Mradi huo wa njia nne za ndege utatekelezwa kwa awamu mbili ambapo utagharimu zaidi ya shilingi Bilioni 600 hadi kukamilika kwake, mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anakushirikisha jambo hapa chini, endelea;


1:Mwaka jana hadi sasa, makubwa yamefanyika,
Barabara zetu hasa, kuweza tengenezeka,
Nchi yawa ya kisasa, maeneo yafunguka,
Miradi kumi na nne, imekwishakamilika.

2:Miradi kumi na nne, imekwishakamilika,
Serikali si wengine, haya yaliyofanyika,
TANROADS tuione, vizuri yawajibika,
Miradi kumi na nne, imekwishakamilika.

3:Kilometa mia nane, themanini zinafika,
Awamu hii tunene, hizo zimeshajengeka,
Tucheke wao wanune, haya yanayosikika,
Miradi kumi na nne, imekwishakamilika.

4:Hatuendi nyuma sana, zingine zilojengeka,
Aprili mwaka jana, awamu sita kufika,
Kazi tumeshaiona, tena Yazidi fanyika,
Miradi kumi na nne, imekwishakamilika.

5:Mikoa kuunganisha, ni kazi inafanyika,
Lengo ni kuharakisha, maendeleo kufika,
Yale mambo ya kushosha, yote yaweze futika,
Miradi kumi na nne, imekwishakamilika.

6:Miradi nchini kote, ile metekelezeka,
Wote baraka wachote, kwao dola yatumika,
Kwa urahisi wapiti, uchumi ukijengeka,
Miradi kumi na nne, imekwishakamilika.

7:Hii awamu ya sita, kazi hiyo mefanyika,
Maeneo yanapeta, barabara kujengeka,
Sasa wanapitapita, raha imeongezeka,
Miradi kumi na nne, imekwishakamilika.

8:Arobaini na nne, miradi inafanyika,
Hiyo hasa ni mingine, kilometa kitajika,
Serikali tuione, jinsi inawajibika,
Miradi kumi na nne, imekwishakamilika.

9:Eapoti Msalato, nayo sasa yajengeka,
Tumeshapata kipato, toka Benki Afrika,
Itaongeza mvuto, itakapokamilika,
Miradi kumi na nne, imekwishakamilika.

10:Rais Samia wetu, Msalato amefika,
Kuona eneo letu, uwanja tapojengeka,
Imeanza kazi yetu, hadi tapokamilika,
Miradi kumi na nne, imekwishakamilika.

11:Kazi inaendelea, hakuna kupumzika,
Lengo linaendelea, mambo vizuri kuweka,
Mema tunayapokea, Serikali kitumika,
Miradi kumi na nne, imekwishakamilika.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments