Azam FC yang'olewa Kombe la Shirikisho barani Afrika

NA DIRAMAKINI

AZAM FC ya jijini Dar es Salaam, Tanzania imeondoshwa rasmi kwenye Kombe la Shirikisho barani Afrika kutokana na tofauti ya mabao 3-2.

Ni baada ya kupoteza kwa kufungwa 3-0 ugenini siku chache zilizopita dhidi ya Al Akhdar ya Libya, ambapo ushindi wa leo wa mabao 2-0 nyumbani hakuwa na tija.

Leo Oktoba 16, 2022 Azam FC ilimenyana na Al Akhdar ya Libya katika dimba la Azam Complex lililopo Kata ya Chamanzi katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Azam FC walihitaji ushindi wa mabao 4-0 ili kusonga mbele, lakini lengo limeonekana kukwama licha ya safu yao kupata nafasi nzuri za kupata ushindi mnono.

Katika mtanange huo, Idris Mbombo dakika ya 27 alimalizia pasi mpenyezo ya Prince Dube na bao la pili lilikuwa la kujifunga kwa beki wa Akhdar dakika ya 58 katika hatua za kuokoa kwa kichwa mpira wa kutengwa uliopigwa na Ayoub Lyanga.

Hayo yanajiri ikiwa tayari, Simba SC wamefanikiwa kwenda Hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Primiero de Agosto ya Angola katika mchezo wa marudiano Hatua ya 32 Bora leo Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Bao pekee la Simba SC leo limefungwa na mshambuliaji wake Mzambia, Mosea Phiri dakika ya 33 na sasa Wekundu wa Msimbazi wanakwenda Hatua ya Makundi kwa ushindi wa jumla wa 4-1 kufuatia kuwafunga 3-1 Agosto kwao, Luanda wiki iliyopita.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news