DC Dkt.Mashinji:Ukatili wa kijinsia haukubaliki, ukijaribu jela inakuhusu

NA FRESHA KINASA

SERIKALI wilayani Serengeti Mkoa wa Mara imeendelea kukemea vikali vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji, ndoa za utoto pamoja na tohara zisizo salama ambazo zimekuwa zikiwahusisha watoto wa kiume kutahiriwa kwa kutumia kisu maeneo ya porini, hali ambayo imetajwa inaweza kuwa chanzo cha magonjwa ya kuambukiza.
Kauli hiyo imetolewa leo Oktoba 10, 2022 na Mkuu wa wilaya hiyo, Mheshimiwa Dkt. Vincent Mashinji wakati akifungua kongamano kuelekea Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike lililofanyika katika Shule ya Sekondari Mugumu na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, mashirika ya kiraia pamoja na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani humo.

"Madhara ya ukatili wa kijinsia ni mengi sana, ukeketaji unaleta magonjwa ya kuambukiza, unaathiri watoto kisaikolojia na kukatisha masomo yao. Serikali inaendelea kumthamini na kumlinda mtoto wa kike kusudi afikie ndoto zake, kwa hiyo tukikamata mtu anakeketa jela itamhusu kwani ni kosa kubwa,"amesema Dkt.Mashinji.
"Na kwa wale wanaotahiri vijana maporini kwa kutumia visu waache, vijana waambieni wazazi kama wanataka kuwafanyia tohara wawapeleke hospitalini kupata tohara salama. Mkiendelea kutahiriwa kwa kutumia visu mtapata UKIMWI na tetenasi lazima jambo hili liachwe,"amesema.

Aidha, Dkt.Mashinji ameihimiza jamii kuendelea kuwapa haki sawa watoto wa kiume na watoto wa kike ikiwemo fursa ya elimu na kusimamia maendeleo yao kitaaluma kusudi wafikie ndoto zao.
Huku akiagiza makongamano mbalimbali yaendelee kufanyika katika shule za sekondari wilayani humo yenye mada mbalimbali za kujenga na kuwaandaa vijana kuja kuwa viongozi katika taifa.

Amewahimiza wanafunzi wote katika shule za msingi na sekondari wilayani humo kusoma kwa bidii na kuwa na malengo, huku akiwataka wajiepushe na vitendo vya kimapenzi ambavyo vinaathari kubwa katika maendeleo yao ya kitaaluma.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Serengeti, Cosmas Qamara amesema kila mmoja ana jukumu la kuwalinda watoto wa kike na watoto wa kiume sambamba na kuwatimizia mahitaji yao ya msingi na kuwalea katika maadili mema.

Naye Daniel Misoji kutoka Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Mkurugenzi wa Shirika hilo, Rhobi Samwelly amesema, shirika hilo limeendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya vitendo vya ukatili wa kijinsia huku akitaja wasichana 65 waliokolewa na shirika hilo msimu wa ukeketaji.

Ameongeza kuwa, shirika hilo linaendelea kutoa hifadhi kwa wasichana waliokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni kupitia vituo vyake kikiwemo Kituo cha Hope Mugumu na Nyumba Salama Butiama na pia linawaendeleza kitaaluma na kifani kusudi wafikie ndoto zao.
Kabla ya kufanyika kongamano hilo, ulifanyika mchezo wa mpira wa mpira wa miguu kati ya timu ya Hope for Girls and Women in Tanzania na timu kutoka Shirika la World Changer, ambapo Hope for Girls and Women in Tanzania waliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Post a Comment

0 Comments