Serikali yatambua mchango wa HGWT mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia Serengeti

NA FRESHA KINASA

SERIKALI wilayani Serengeti mkoani Mara imepongeza juhudi za kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni zinazofanywa na mashirika mbalimbali likiwemo Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) kupitia Mkurugenzi wake, Rhobi Samwelly.
Shirika hilo limetajwa kuwa miongoni mwa mashirika ambayo yana mchango mkubwa kwa Serikali hasa kutoa hifadhi kwa wahanga wa vitendo hivyo, kutoa elimu kwa Jamii ya madhara ya ukatili wa kijinsia na kuwaendeleza kielimu watoto wa kike katika kuhakikisha wanafikia ndoto zao.

Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Serengeti, Cosmas Qamara wakati akizungumza katika Kituo cha Hope Mugumu alipotembelea akiwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, mashirika ya kiraia ikiwa ni sehemu ya kuelekea Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike ambayo itafanyika Oktoba 11, 2022 ikiwa na kauli mbiu isemayo 'Haki yetu hatima yetu, wakati ni sasa'.
Qamara amesema,Serikali ya wilaya hiyo inatambua na kuthamini juhudi za mashirika yote yanayofanya kazi za kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia na hivyo kuisaidia Serikali katika mpango wake wa kutokomeza vitendo hivyo ambapo awali amesema vilifanyika hadharani watoto wa kike kukeketwa tofauti na sasa ambapo vinafanyika kwa siri.

Ameongeza kuwa, Serikali wilayani humo itaendelea kushirikiana na mashirika yote katika kupambana na vitendo hivyo, huku akiomba kasi ya utoaji wa elimu ya kutokomeza ukatili iendelee kutolewa kwa makundi yote hasa maeneo ya vijijini ambako bado ukatili unafanywa kutokana na mwamko mdogo wa elimu.
Aidha, ameomba mila na desturi zilizopitwa na wakati ambazo bado ni kikwazo kwa watoto wa kike na wanawake ziachwe mara moja kwani hazina faida, na badala yake mila nzuri zenye manufaa ziendelezwe ambazo zitajenga Jamii katika misingi ya umoja, upendo na amani.

Amewaomba pia wadau mbalimbali kuendelea kuwasaidia watoto wanaopata hifadhi katika vituo vya Nyumba Salama na Hope Mugumu kwa kuwapa mahitaji yao ya msingi katika kutekeleza jambo la upendo kwa kuwajali watu wenye uhitaji kwani ndiko kuchota baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Neema Msuya akizungumza na wasichana wa Nyumba Salama na Hope Mugumu Kituoni hapo amewahimiza kusoma kwa bidii na kuishi katika maadili mema wakitambua kwamba wana nafasi ya kuandaa kesho yao yenye kung'ara kuanzia sasa ili waje walete maendeleo katika jamii.

Naye Mkuu wa Kituo cha Hope Mugumu, Daniel Misoji akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa shirika hilo, Rhobi Samwelly amesema,shirika hilo limekuwa likitoa hifadhi kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia, kuwaendeleza kielimu na kitaaluma wasichana wanaohifadhiwa kituoni hapo.
Ameongeza kuwa, shirika linaendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali wilayani humo pamoja na wadau wote na wananchi katika kuhakikisha kwamba ndoto za watoto wa kike zinatimia. Huku akishauri jamii kutowakeketa watoto wa kike na kuwaozesha katika umri mdogo kwani ni kuwanyima haki ya kupata elimu na ni kosa kisheria.

Katika kuelekea siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike, Serikali wilayani Serengeti imeweza pia kuendesha kongamano lililowakutanisha wadau kutoka mashirika mbalimbali wakiwemo wananchi, wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Pia, wametembelea vituo vinavyotoa hifadhi kwa wasichana waliokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni ikiwemo Kituo cha Nyumba Salama kinachomilikiwa na Kanisa la Anglican Mugumu, Shirika la World Changer na Kituo cha Hope Mugumu cha Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania ambapo pia wametoa mahitaji mbalimbali katika vituo hivyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news