Dkt.Msuha ataja mikakati ya Wizara ya Maliasili na Utalii

NA MWANDISHI WETU

MKURUGENZI wa Idara ya Wanyamapori, Dkt. Maurus Msuha amesema moja ya mkakati wa Wizara ya Maliasili na Utalii ni kuhakikisha migongano baina ya binadamu na wanyamapori hasa kwenye maeneo ya pembezoni mwa hifadhi inapungua kwa kiasi kikubwa.
Kikao cha timu ya Watalaam kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Shirika la Maendeleo ya Ujerumani (GIZ), kilichokutana leo Jijini Dodoma kwa ajili ya kutambulisha mradi wa kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu unaotarajiwa kuanza hivi karibuni mkoani Ruvuma.

Ametoa kauli hiyo leo tarehe 18 Oktoba, 2022 wakati wa kutambulisha mradi wa kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu katika kikao kilichofanyika Jijini Dodoma kilichozikutanisha timu ya Watalaam kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Shirika la Maendeleo ya Ujerumani (GIZ),

Hatua hiyo inakuja kufuatia Serikali ya Tanzania kupokea Euro milioni 6 sawa na shilingi bilioni 13.2 kutoka Shirika la Ujerumani la GIZ kwa ajili ya mradi wa kupunguza migogoro baina ya binadamu na wanyamapori katika mfumo wa Ikolojia Selous Niassa

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt.Msuha amesema Serikali imekuwa ikifanya kila liwezekanalo ili kuhakikisha kuwa Wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya Hifadhi hawaathiriwi na wanyamapori hao badala yake wanatumia maeneo hayo katika kujinufaisha kiuchumi
Ameeleza kuwa moja ya mikakati ambayo Serikali imekuwa ikifanya ili kukabiliana na wanyamapori hao ni kuwavisha vifaa maalum vya utambuzi kwa wanyamapori viongozi pamoja na kuwajengea uwezo wananchi katika kukabiliana na wanayamapori wakali na waharibifu.

Naye, Mkurugenzi wa GIZ nchini Tanzania, Dkt. Mike Folke amesema Serikali ya Ujerumani imelazimika kutoa fedha hizo kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika Uhifadhi wa Wanyamapori.

‘’Watanzania wanapenda sana kuhifadhi wanyamapori hivyo kama migongano kati ya binadamu na wanyamapori hataidhibitiwa Watanzania hawa wanaowapenda wanyama hao wataanza kuwachukia wanyama hao,’’alisistiza Dkt. Mike Folke.

Mradi huo wa kukabiliana na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu utakaofanyika katika baadhi ya Wilaya za Ruvuma zenye changamoto za wanyama unatarajiwa kuanza hivi karibuni na utadumu kwa kipindi cha muda wa miaka mitatu (2022-2025).

Post a Comment

0 Comments