Hapa Nyasho hatuwezi kuishi na wahalifu, toeni taarifa-Diwani Mtete

NA FRESHA KINASA

DIWANI wa Kata ya Nyasho Manispaa ya Musoma mkoani Mara, Mheshimiwa Haji Mtete amewataka wananchi wa Kata ya Nyasho kutoa taarifa polisi juu ya watu wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu ili wawajibishwe.
Ameyasema hayo Oktoba 20,2022 wakati akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Nyasho Kati katika kikao cha pamoja kilichohusisha wananchi,maafisa wa Jeshi la Polisi pamoja na wataalam mbalimbali wa serikali.

Mheshimiwa Mtete amesema kwamba, vitendo vya kihalifu vimekuwa vikifanyika katika kata hiyo na wanaofanya vitendo hivyo ni vijana ambao wanaishi katika mitaa ya kata hiyo. Hivyo,wananchi watoe taarifa sahihi za wahalifu wote kwa vyombo vya dola kwa hatua kali za kisheria.

Amesema, nia ni kuona wananchi wanafanya kazi zao na kuishi kwa utulivu na amani hivyo vitendo vya kihalifu na wahalifu wote hawana nafasi kwani wanarudisha nyuma maendeleo ya wananchi na Serikali kwa ujumla.

"Tusiwafumbie macho wanaofanya uhalifu, wanajeruhi watu kwa kukata mapanga na kuiba mali za watu vitendo hivi havikubaliki hata kidogo lazima wananchi tuungane kwa pamoja kuwafichua na kutoa ushahidi mahakamani wanapokamatwa kusudi tatizo hili tulikomeshe,"amesema Mheshimiwa Mtete.
Aidha, Mheshimiwa Mtete ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha shilingi milioni 120 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarsa sita katika Shule ya Sekondari Nyasho. Na pia akasema ujenzi wa mitaro katika mtaa wa Nyasho kati na Nyasho Shuleni ambapo ujenzi huo unafanywa na TARURA ili kuwaondolea adha ambayo wananchi walikuwa awali wakiipata.

Kwa upande wake Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la TMRC Kigera ambaye ni Mkazi wa Kata ya Nyasho amesema,wananchi wawe tayari kushiriki katika ulinzi shirikishi kudhibiti uhalifu.

Amewataka wazazi na walezi wa watoto wanaotuhumiwa kujihusisha na uhalifu wawakanye waachane na uhalifu, kwani haulipi na wasipofanya hivyo sheria zipo ziwawajibishe kikamilifu.

Kwa upande wake Afisa Lishe wa Manispaa ya Musoma Emmanuel Kanisius akizungumza katika mkutano huo amesema, serikali imekuja na mpango wa kuhakikisha watoto wanapata chakula shuleni ili kukabiliana na tatizo la utapiamlo. Hivyo, amewaomba wananchi watakapoambiwa kuchangia chakula watoe mwitikio chanya kufanikisha jambo hili ili kuondoa tatizo la utapiamlo kwa watoto.
"Kwa upande wa Serikali za mitaa kuepuka tatizo hili la utapiamlo kwa kinamama wajawazito lazima wazingatie lishe bora, kuwapunguzia majukumu mazito ya kazi kina mama wajawazito hii itasaidia sana,"amesema Emmanuel.

Amewahimza wazazi na walezi kufanya mabadiliko kwa kuzingatia mfumo bora wa lishe ikiwemo kula aina za vyakula vyenye wanga, protini, matunda, mbogamboga, mafuta na vyakula vyenye madini kwani vinaumuhimu mkubwa kwa afya bora.

Amesema, iwapo wazazi na walezi watashiriki kikamilifu kuunga mkono juhudi za serikali za kuhakikisha wanasimamia vyema suala la lishe itakuwa rahisi tatizo hilo kulitatua kwani watoto wengi katika Manispaa ya Musoma wanakabiliwa na utapiamlo.

Post a Comment

0 Comments