KAPITA NIMEKAMATWA-3:Sheria nitazitii, nisirudie kung’atwa

NA LWAGA MWAMBANDE

BILA kushinikizwa au kushurutishwa na mtu au kitu chochote, unapaswa kutambua kuwa usalama barabarani ni jukumu la kila mmoja wetu.

Picha kwa hisani ya Twitter ya Damas.

Ukitii sheria bila shuruti unaweza kujikuta unaendesha chombo chako cha moto kwa amani, kuwakinga na kujikinga dhidi ya majanga ikiwemo ajali ambayo inaweza kukatisha uhai wako au wa wengine barabarani.

Ndiyo maana,kwa dereva makini lazima ahakikishe chombo chake anachoendesha kipo katika hali ya usalama, anafunga mikanda, kuzingatia mwendo salama, kufuata alama za barabarani bila kujali ni kipindi cha kiangazi au mvua. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, ukitii sheria za usalama barabarani bila shuruti hauwezi kujutia maisha, endelea;

1.Nimefwata estii, kapita nimekamatwa,
Ninasema sirudii, kwa jinsi nilivyopatwa,
Sheria nitazitii, nisirudie kung’atwa,
Wewe fwata mwendo wao, utayeumia wewe.

2.Lile basi nanihii, lakimbia ninavutwa,
Spidi si nchi hii, huku vumbi tunapatwa,
Kama hawaangalii, picha zao zinafutwa,
Wewe fwata mwendo wao, utayeumia wewe.

3.Si gari la watalii, ya kwamba watakamatwa,
Au wale dini hii, ili wapate kutetwa,
Ni wakuu boma hii, wanapenda kuburutwa,
Wewe fwata mwendo wao, utayeumia wewe.

4.Kuna watu nchi hii, wanaopaswa kusutwa,
Sheria za nchi hii, kwao kama zaokotwa,
Jinsi hizo hawatii, hadi kifo wakipatwa,
Wewe fwata mwendo wao, utayeumia wewe.

5.Wala hawafikirii, ajali waweza patwa,
Ndivyo hawasubirii, kwenye kona unapitwa,
Hatari za njia hii, humo ndani waburutwa,
Wewe fwata mwendo wao, utayeumia wewe.

6.Mbio kwao jubilii, kwani hao wanang’atwa,
Ni wakuu kambi hii, wasojali kukeketwa,
Kwelui mambo hayo zii, yaishe yaweze futwa,
Wewe fwata mwendo wao, utayeumia wewe.

7.Meambiwa ndiyo hii, spidi bora kufwatwa,
Heri hawajitakii, kuhamishwa na kusutwa?
Pita hawaangalii, juu yako ukipatwa,
Wewe fwata mwendo wao, utayeumia wewe.

8.Waonye hawasikii, jinsi wao wanavutwa,
Kwanini hawatambii, magari yanayoletwa,
Bora kama digrii, huko yanako tafutwa,
Wewe fwata mwendo wao, utayeumia wewe.

9.Sisi wale pande hii, mchecheto tunapatwa,
Ajali ile na hii, ambayo ndugu wapatwa,
Zingeshuka mara hii, sheria zikifuatwa,
Wewe fwata mwendo wao, utayeumia wewe.

10.Niseme sifwatilii, wanaopaswa kusutwa,
Miye si wa nchi hii, kwa vifo jinsi twavutwa,
Yenu siyaangalii, sheria zapaswa fwatwa,
Wewe fwata mwendo wao, utayeumia wewe.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments