HAWA TEMBO WARRIORS, FAHARI YA TANZANIA

NA LWAGA MWAMBANDE

OKTOBA 11, 2022 Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa ametimiza ahadi ya Serikali ya kuizawadia timu ya soka ya Taifa ya Tembo Warriors iliyoshiriki mashindano ya Kombe la Dunia kwa watu wenye ulemavu nchini Uturuki.

Katika michuano hiyo, Tembo Warriors walionesha bidii, juhudi na maarifa ambayo yaliwawezesha kuwa na ushindani dhidi ya wapinzani wao kutoka mataifa mbalimbali huku ikiibuka miongoni mwa timu 10 bora duniani.
Mheshimiwa Waziri Mchengerwa kwa kuthamini juhudi hizo,siku hiyo jijini Dar es Salaam alitekeleza ahadi yake kwa timu hiyo ambayo aliitoa awali wakati wakielekea nchini Uturuki kushiriki michuano hiyo ya Dunia. Siku hiyo, kikosi hicho kilikabidhiwa hundi ya shilingi milioni 40 kama zawadi.

Mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande anasema, utekelezaji huo wa ahadi unaonesha heshima na thamani kubwa kwa kikosi hicho ambacho kimeipeperusha vema bendera ya Taifa duniani,pia inawatia moyo huku zawadi hiyo ikituma ujumbe kwa wingine kuwa, mkifanya vizuri Taifa linathamini kazi na juhudi husika, endelea kujifunza hapa;

1:Hawa Tembo Warriors, fahari ya Tanzania,
Kweli wamefanya kazi, ni bora kuwasifia,
Wameonyesha ujuzi, kwenye kombe la dunia,
Zawadi zao wapewe, na sifa ziendelee.

2:Ona kwa mara ya kwanza, kwenda kombe la dunia,
Michezo walivyoanza, mechi walijishindia,
Wengine waliwafunza, hadi robo kufikia,
Zawadi zao wapewe, na sifa ziendelee.

3:Wengi mara ya kwanza, makundi wangeishia,
Na tena wangejiponza, wangefungwa wangelia,
Tembo tunawapongeza, pazuri wamefikia,
Zawadi zao wapewe, na sifa ziendelee.

4:Ufunguo tumepata, hapo tulipofikia,
Huku tuzidi kusota, timu kujiandalia,
Kesho tuzidi kupeta, Afrika na dunia,
Zawadi zao wapewe, na sifa ziendelee.

5:Tusijerudia nyuma, tuweze kushikilia,
Vijana wanaosoma, tuweze kuwatumia,
Mafunzo wapate vema, wende tuwakilishia,
Zawadi zao wapewe, na sifa ziendelee.

6:Enyi Tembo Warriors, wanasoka Tanzania,
Mmeifanya kazi, sisi tunajivunia,
Tembea kifua wazi, sisi twawashangilia,
Zawadi zao wenyewe, na sifa ziendelee.

7:Waziri ametimiza, vile aliahidia,
Sote tunawapongeza, sifa zinazozidia,
Mmecheza mmeweza, pazuri mmefikia,
Zawadi zao wenyewe, na sifa ziendelee.

8:Tunaamini wengine, nao tutawasikia,
Watoe zawadi nene, mabalozi Tanzania,
Mifuko yenu inone, mzidi kufurahia,
Zawadi zao wenyewe, na sifa ziendelee.

9:Mmefungua mlango, nchi yetu Tanzania,
Tutafikia malengo, dunia kuifikia,
India kuna mpango, yashiriki Tanzania,
Zawadi zao wenyewe, na sifa ziendelee.

10:Tembo Warriors heko, pazuri tumefikia,
Tumejawa na kicheko, kote tunakopitia,
Sasa jina letu liko, kwenye soka la dunia,
Zawadi zao wenyewe, na sifa ziendelee.

11:Na Serengeti Girls, wako kombe la dunia,
Wasichana kazikazi, India watufanyia,
Wazidi kugawa dozi, sisi tutafurahia,
Zawadi zao wenyewe, na sifa ziendelee.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news