Ibwe avaa viatu vya Zakaria kwa muda Azam FC

NA DIRAMAKINI

MTANZAJI wa runinga ya Azam ya jijini Dar es Salaam,Hasheem Ibwe ameteuliwa na uongozi wa timu ya Azam FC ya jijini Dar es Salaam kuwa Afisa Habari wa muda.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Oktoba 18, 2022 na uongozi wa timu hiyo ambapo Ibwe atakuwa Kaimu Afisa Habari wake kuanzia tarehe tajwa hadi hapo itakapotangazwa vinginevyo.
Ibwe anachukua nafasi hiyo kipindi hiki ambacho, Afisa Habari wa Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ anatumikia adhabu ya kufungiwa na Bodi ya Ligi.

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Oktoba 4, 2022 ilimfungia Zakaria kwa kipindi cha miezi mitatu na kutozwa faini ya sh.500,000.

Ni kwa kosa la kushutumu waamuzi wa mchezo wao dhidi ya Tanzania Prisons FC uliyopigwa uwanja wa Sokoine jijini Mbeya Septemba 30, 2022.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwenye kamati hiyo ilidai kuwa, Thabiti alitenda kosa hilo huku akifahamu kuwa timu yake ilikuwa imeshatumia njia sahihi ya kikanuni kwa kuiandikia barua Bodi ya Ligi Kuu Tanzania kuhusu malalamiko yao kwa waamuzi.

Aidha, kanuni ya 39:(8 & 10) ya Ligi Kuu kuhusu Waamuzi na Kanuni ya 46:(3 & 10) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Viongozi zinasisitiza klabu kutumia njia sahihi kuwasilisha malalamiko yao kwa TPLB/TFF na kuwataka viongozi kuepuka kulalamika ama kushutumu waamuzi kupitia vyombo vya habari na mahali pengine popote.

Hata hivyo, adhabu hiyo kulingana na taarifa hiyo ilitolewa kwa uzingativu wa Kanuni ya 46:10 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Viongozi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news