JE, TUNANGOJA KUPIGA RAMLI ? TUENDELEE KULA PAPAI LA MKURANGA

NA ADELADIUS MAKWEGA

KATIKA matini yangu iliyopewa jina Papai la Mkuranga, mwanakwetu nilizungumza hoja ya Makatibu Tawala wa Mikoa Kushiriki vikao vya Mabaraza ya Madiwani ambayo mara zote kwa mwaka havizidi vikao saba na nilitaja hoja ya Kata ya Mbagala mkoani Dar es Salaam kukosa shule ya sekondari.KARIBU PAPAI LA MKURANGA HAPA

Hoja hii niliitaja kutokana na kuhamishwa matumizi ya shilingi milioni 480 ya fedha za Kata ya Mbagala kupelekwa kata nyingine kwa kuwa ndugu zangu wa Mbagala ikidaiwa kuwa hawakuwa na eneo la ujenzi wa shule ya sekondari lenye sifa zinazodaiwa ziwe, japokuwa maeneo kadha niliyataja msomaji wangu katika matini hayo.

Katika matini hiyo nilisema wazi kuwa kama kila mara pesa ikipangiwa katika eneo fulani alafu ikahamishiwa eneo lingine kila wakati jambo hilo si jema na alilete siha njema ya maendeleo kwa eneo lililopangiwa pesa tangu awali.

Mwanakwetu kwa leo sitaki kwenda mbali zaidi katika hilo tafsiri yake ni kuwa kitendo hicho kilichofanyika katika fedha za Kata ya Mbagala mkoani Dar es Salaam inawezekana kinafanyika katika maeneo mengi ya Tanzania. 

Ninasema wazi kuwa jambo hilo si zuri, halikubaliki, hoja ya sababu ya kuhamiswa fedha hizo kupelekwa maeneo mengine hazipaswi kupigiwa makofi na vigelegele na mtu yoyote yule na shangwe yoyote juu ya kuzihamisha fedha hizo zinapaswa kukataliwa na kutazamwa kwa jicho kali.

Wahusika wanapaswa kuzifanyia kazi haraka hoja zote za kufanikisha pesa hizo zinabaki katika eneo husika ilikuwapa maendeleo eneo lililoomba pesa hizo katika mpango wa maendeleo ya kata husika.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Hassan Abbas Rungwa yeye mwenyewe kama angekuwepo katika kikao hicho kilichotoa baraka hili jambo nina Imani hilo lisingefanyika. 

Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam afahamu kuwa ni jambo la aibu tunaposema kuna kata katika mkoa wake haina shule ya sekondari, Yeye kama kiongozi, yeye kama mtu aliyepewa dhamana na yeye kama mzazi.

Utafiti wangu unaonesha wazi kuwa makatibu tawala wa mikoa mingi wanatuma uwakilishi katika mabaraza ya madiwani, kwa hakika mimi binafsi ninaona kuwa jambo hilo halikubaliki, linakinyima mambo mengi kikao cha Baraza la Madiwani kama Katibu Tawala Mkoa akiwapo.

Mojawapo mambo mengi yanayojadiliwa kikaoni hapo Katibu Tawala wa Mkoa ni vigumu kuyajibu moja kwa moja kama akituma uwakilishi. 

Labda majibu hayo hadi aandikiwe barua au kupelekewa nakala ya muhtasari wa kikao hicho ambako nakala moja inakwenda kwa Katibu Mkuu TAMISEMI, jambo hilo linatumia muda mwingi. Muhtasari mara zote hauwezi kuonesha hali halisi ya mjadala ulivyo bali mwandishi ataandika kwa kupunguza ukali wa tukio lilivyokuwa likiendelea kikaoni.

Katibu Tawala wa Mkoa wowote akiwepo katika kikao cha Baraza la Madiwani itasadia kutambua na kuona kwa macho yake uwezo wa watumishi wa halmashauri na wilaya husika. Watumishi hao wakiwamo wakuu wa idara na Katibu Tawala wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji, Mkuu wa Wilaya pia na hata Kamati nzima ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya husika. Kikaoni inaweza kuonesha namna ilivyofanya kazi kutokana na michango ya madiwani.

Hapo Katibu Tawala wa Mkoa atafahamu kama ndugu hao wanafanya kazi kwa kushirikiana au kila mmoja na luake, atafahamu tabia zao ndani ya vikao, .itasaidia kutambua hata taarifa zinazofika kwake ni majungu au ukweli, atatambua pia kuwa hapa pametiwa chumvi nyingi au hapa pametiwa chumvi kidogo.

Katibu Tawala wa Mkoa ni Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa husika ambayo mara zote inakusanya wajumbe mbalimbali kutoka vyombo vya ulinzi na usalama katika mkoa huo, kama akishiriki vikao hivyo yeye mwenyewe atakuwa shuhuda wa mengi kutoka kila wilaya ya mkoa husika.

Kitendo cha katibu huyu kuwepo katika vikao cha Mabaraza ya Madiwnai ya kila halmashauri kitasaidia sana kumuongoza yeye binafsi na hata kamati nzima ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa juu ya mapendekezo sahihi juu ya jambo lolote lile lenye maslahi ya wengi katika mkoa huo na sio kugonja kupewa taarifa za maandishi ambayo inaweza kupunguzwa au kuongezwa chumvi.

Pia hili linaweza kusaidia kuondoa migogoro mingi iliyopo baina ya watendaji katika wilaya ambayo mingi haina tija kwa wananchi bali ni maslahi watu binafsi tu .

Mwanakwetu naomba kwa leo niishie hapo na kuiweka kando kalamu yangu inayolalamikia na kusisitiza kuwa kila Katibu Tawala wa Mkoa yeye mwenyewe moyoni mwake aone umuhimu wa kushiriki vikao hivyo vya mabaraza ya madiwani na kuepuka maamuzi ya kuhamisha fedha za maendeleo kwenda katika maeneno mengine kama hili la Kata ya Mbagala mkoani Dar es Salaam, kilichotakiwa kufanyika mapema ni kufanya maamuzi ya pahala pa kujenga tu. Makatibu Tawala wa Mikoa kushiriki katika vikao hivyo na hata hili la kujenga shule ya sekondari ya Kata ya Mbagala JE TUNANGOJA KUPIGA RAMLI ?

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news