PAPAI LA MKURANGA

NA ADELADIUS MAKWEGA

OKTOBA 25, 2022 nilipata ugeni nyumbani kwangu Mbagala majira ya saa tatu za usiku, mama mmoja ambaye ni kada wa CCM alifika kunisalimu, akisema kuwa kwa siku nne hakuwepo jijini, alifunga safari Wilayani Mkuranga mkoani Pwani.
Kwa kuwa ndugu yangu huyu aliniambia hayo, nilimuuliza alikwenda Mkuranga kufanya nini?. Majibu yake yalikuwa huko ni shambani kwake ana shamba lao la urithi. Nilimpongeza sana kwa kwenda shambani kulima huku nikimwambia watu wa Mbagala na Mkuranga ni ndugu.“Pokea zawadi ya Papai la Mkuranga.” Mwanakwetu nilipokea kwa mikono miwili.

Nilishukuru sana maana sijala mapapai ya pwani miaka mingi mno. Nilimshukuru tena na tena mama huyu kwani tangu niwepo Dar es Salaam Oktoba 12, 2022 sikujaliwa kupewa zawadi yoyote isipokuwa zawadi hii ya Papai la Mkuranga.

Kwa hakika papai hili lilikatwa na kugawana mimi na jamaa zangu kadhaa hapo nyumbani. 

Nikiwa hapo tulizungumza mambo mengi katika mama huyu aliyeniletea papai aliniambia kuwa wao kwa sasa katika Kata ya Mbagala wana changamoto kubwa ya uhaba wa shule ya sekondari huku wakiwa na shule tatu za msingi. Watoto wao wanapata hisani ya kusoma katika kata zingine. 

Mwanakwetu hilo kwangu lilikuwa jambo la kushangaza mno leo hii ipo kata ambayo haina shule ya sekondari? Wakati serikali ya Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete zilihimiza jambo hilo kwa kina?

Nilipouliza kwanini Kata ya Mbagala ambayo ni kata kongwe haina shule ya sekondari? Niliambiwa kuwa kuna wakati kata hii ilipata fedha za kununua eneo huko Kwa Mkondola na kulipiwa zaidi ya shilingi milioni 200 na baadaye eneo hilo likaonekana kuwa linabonde halifai kwa ujenzi wa shule ya sekondari.

Jambo hilo la miaka kadhaa sasa, huku kukiwa na hoja kuwa wanaweza kujenga shule hiyo Mbagala kwa Maganya-Mwembe Pacha lakini nalo eneo hilo lilitakiwa kulipiwa na eneo jirani na eneo la Mwembe Pacha kubadilishiwa matumizi yake kutoka soko na kuwa shule ya sekondari wakati hilo halijafanyika.

Mtendaji wa kata hii Habiba Mohamed alisema bayana kuwa ni kweli kata yake haina shule ya sekondari na baadhi ya wadau wanashauri kuwa shule ya msingi mojawapo ibalishwe kuwa shule ya sekondari, lakini Mtendaji Habiba anasema wazi kuwa hilo ni gumu sana kwani hata shule za msingi zenyewe ni chache ikilinganishwa na uwiano wanafunzi madarasani. Kata hii inaitaji shule zaidi ya mbili mpya.

“Kama tunaibadilisha shule ya msingi kuwa sekondari hapo tutakuwa tunahamisha tatizo kutoka mkono wa kulia kwenda mkono wa kushoto.” Alisema Mtendaji Hadija.

Tukiwa katika mazungumzo hayo huku Papai la Mkuranga likilika tulimtafuta Diwani wa Kata ya Mbagala mheshimiwa Michael Makwega na yeye aliungama wazi kuwa ni kweli kata yake inatatizo la uhaba wa shule ya sekondari na hicho ndicho kilio cha chao na watoto wao wanasoma katika kata za mbali na kama wangekuwa na shule hiyo jambo hilo lingepunguza gharama kwa wazazi ikiwamo pesa za nauli ili watoto wao wafike mapema shuleni.

“Kata yetu imepata pesa za ujenzi wa sekondari lakini kutokana na kukosa eneo lenye vigezo jambo hilo limesababisha zaidi ya shilingi milioni 480 zimehamshiwa kata nyingine.”

Hiyo inatoa picha ya wazi kuwa Serikali Kuu inatenga pesa kwa ajili ya kata hii. Shida Je pesa hizo zitakuwa zinahamishiwa kwenda kata zingine mara ngapi?

Nilipokuwa nazungumza na mgeni huyu nilibaini kuwa Kata ya Mbagala haina shida ya eneo la kujenga shule, shida ni kufanya maamuzi tu. Hapa pana maeneo ya zamani mawili na maeneo mapya mawili. 

Maeneo ya zamani ni lile la Mkondola ambao limelipiwa , likidaiwa lipo katika kilima, hoja hii haina maantiki ni hoja dhaifu sana katika nchi yetu zipo shule nyingi zilizo milimani najirani na mabonde n ahata sauti ya maji yakipitia kando ya madarasa ya shule hizo kila siku mathalani Shule ya Misingi Mbura A na Mbura B huko Lushoto Mkoani Tanga, linalotakiwa kufanywa ni kutengeneza miundo mbinu vizuri na eneo hilo litumike. 

Eneo la pili ni lile la Mwembe Pacha, eneo hili ni la umma yanawezwa kujengwa hata madarasa matano kwa kuanzia alafu watu jirani wanalipwa kidogo kidogo. Hapo panawezwa kupokewa wanafunzi wa kidato cha kwanza mapema Januari, 2023.

Maeneo mapya nayo yapo mawili kwanza ni eneo jirani na Mto Mzinga upande wa Mbagala jirani na barabara mpya iliyojegwa hivi karibuni na CCM Diria kuelekea Mbagala Bugudadi hapo panawezwa kujengwa ukuta, ukajazwa vifusi alafu ujenzi wa shule kuanza mara moja. Hili ni eneo ambalo hakuna malipo yoyote kwa mtu yoyote yule.

Kwa upande wa maeneo mapya, serikali inaweza kuzungumza na familia ya Marehemu Jaji Kimicha na familia hii kutoa sehemu ya ardhi yake kwa makubaliano maana eneo hili linamilikiwa na watu binafsi kwa muda mrefu tangu wakati wa ukoloni, familia ya Bibi Sela (Bibi Sara) na baadaye Jaji Kimicha.

Siyo jambo la busara mtu mmoja akamiliki aeneo kubwa wakati jamii kando yake ikitafuta eneo la kujenga shule. Serikali inapaswa kutazama baadhi ya sheria zake hizo hasa kwa maeneo ya mijini, wamiliki hao walipewa eneo hilo kama shamba ni si kama makazi, sasa Mbagala si mashamba bali ni makazi.

Haiwezekani mtu alipewa eneo la kubwa kama shamba sasa Mbagala ni mji bado mtu huyu akabaki na eneo hilo.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam anapaswa kushiriki vikao vya Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, asitume uwakilishi huko afuatilie hili la kuhamishia fedha za miradi ya maendeleo ya kata zinazokosa maeneo ya ujenzi au hoja zozote zinazokwamisha ujenzi. 

Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam hizo fedha milioni 480 asimamie fedha zinarejeshwa kata ya Mbagala na mwisho eneo la ujenzi lichaguliwe haraka sana ili kuchapulisha ujenzi wa shule ya sekondari ya Kata ya Mbagala ili kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza waliofanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu.

Kitendo cha kuhamisha fedha za miradi si jambo zuri, iwek kwa kata ya Mbagala aua kata yoyote ile nchni Tanzania. Viongozi watimize wajibu na fedha zitumike kama zilipopangwa wakati wa kuombwa.

Mwanakwetu kumbuka tulikuwa sebuleni kwetu tunayazungumza haya tukila Papai la Mkuranga lililotupatia hekima kubwa ya kutatua kero hii ya ndugu zetu, muda ulisonga na kada huyu wa CCM akatoka zake kurudi kwake na mimi nikauchapa usingizi.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Post a Comment

0 Comments