KUMBUKIZI YA MIAKA 23:MWALIMU TWAMKUMBUKA

NA LWAGA MWAMBANDE

OKTOBA 14, ya kila mwaka ni siku ambayo Taifa letu huwa linaadhimisha kumbukizi ya kifo cha Baba wa Taifa letu na aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mwalimu Nyerere alifariki dunia Oktoba 14, 1999 katika Hospitali ya Mt.Thomas iliyopo jijini London, Uingereza alipokuwa akipatiwa matibabu na kuacha simanzi kubwa ndani na nje ya nchi.

Kwa maana nyingine, leo Oktoba 14, 2022 Watanzania wanaadhimisha kumbukizi ya miaka 23 bila Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anakushirikisha mambo muhimu kumuhusu Baba wa Taifa kupitia shairi hapa chini, endelea;

1:Ni Rais mwananchi, sifa hiyo yamfaa,
Tena mwasisi wa nchi, vile alituandaa,
Makabila kuwa nchi, Kiswahili tumevaa,
Miaka ishina tatu, Mwalimu twamkumbuka.

2:Lipigania uhuru, kuja TANU toka TAA,
Nchi ikapata nuru, kwa Amani tunakaa,
Uhuru bila ushuru, elimu ilizagaa,
Miaka ishina tatu, Mwalimu twamkumbuka.

3:Kule kwake chungulia, alikokuwa kikaa,
Rahisi kupafikia, wepesi ulivyojaa,
Na hata kuchungulia, unaona hadi paa,
Miaka ishina tatu, Mwalimu twamkumbuka.

4:Mali kuyalimbikiza, kwani tembo amejaa?
Ndivyo alijieleza, kwake kusijekujaa,
Kwa kweli alimaliza, uadilifu lijaa,
Miaka ishina tatu, Mwalimu twamkumbuka.

5:Pale mtu anakufa, mema ndiyo yanakaa,
Naye hakuleta ufa, kufanya yenye kinyaa,
Alijawa maarifa, alivyokuwa shujaa,
Miaka ishina tatu, Mwalimu twamkumbuka.

6:Tanzania nchi yake, hapa ndipo alikaa,
Hakujali mambo yake, kote alitapakaa,
Hasa msimamo wake, dhuluma alikataa,
Miaka ishina tatu, Mwalimu twamkumbuka.

7:Jina lake Afrika, kwa kweli limezagaa,
Hasa vile hakuchoka, ukombozi kuandaaa,
Hadi uhuru kufika, kweli nchi lichakaa,
Miaka ishina tatu, Mwalimu twamkumbuka

8:Maputo, Luanda kote, wanajeshi lizagaa,
Kukomboa nchi zote, Mreno ashindwe kaa,
Ukoloni waufute, watu huru weze kaa,
Miaka ishina tatu, Mwalimu twamkumbuka.

9:Hapa kwetu Tanzania, jinsi sisi tunakaa,
Makabila zidi mia, kote yametapakaa,
Nani anaangalia, Kiswahili chazagaa,
Miaka ishina tatu, Mwalumu twamkumbuka.

10:Mazuri bora kuenzi, vema tuzidi kukaa,
Yasopasa kuyaenzi, tuyatupe kwenye jaa,
Tufanye tunayoenzi, kwetu kusiwe njaa,
Miaka ishina tatu, Mwalimu twamkumbuka.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news