Aliyemkata mpenzi wake nyeti asakwa

NA DIRAMAKINI

JESHI la Polisi mkoani Mwanza linamtafuta mtu aliyefahamika kwa jina moja la Masoud kwa tuhuma za kumkata sehemu za siri pamoja na chuchu za matiti zote kwa aliyekuwa mpenzi wake aliyedumu naye miezi miwili.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, SACP Ramadhani Ng’anzi ambapo amebainisha kuwa,tukio hilo lililotokea Oktoba 9,mwaka huu, majira ya saa 16:45 jioni, huko maeneo ya hifadhi ya Msitu wa Sayaka uliopo Kata ya Itumbili Wilaya ya Magu mkoani humo.

Amesema kuwa, katika uchunguzi wa awali mwanamke huyo (jina lake linahifadhiwa) alifanyiwa ukatili huo kwa imani za kishirikina ambapo mtuhumiwa alimuadaa kuwa anaenda kumuonesha shamba la dengu lililopo katika msitu wa hifadhi ya Sayaka na walipofika alimkaba shingoni na kupoteza fahamu na kutekeleza unyama huo.

Kamanda huyo amesema kuwa, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linafanya kila jitihada kuhakikisha linamtia nguvuni mtuhumiwa huyo ili aweze kufikishwa katika vyombo vya dola.

Hata hivyo, mhanga wa tukio hilo anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Bugando na hali yake inaendelea vizuri.

Post a Comment

0 Comments