Kunyimana tendo la ndoa yatajwa kuwa chanzo cha msongo wa mawazo, vipigo

NA DIRAMAKINI

TABIA ya baadhi ya wanandoa kunyimana tendo la ndoa ni miongoni mwa sababu zinazosababisha migogoro baina yao, msongo wa mawazo sambamba na kushamiri kwa vitendo vya ukatili kwa watoto wao.

Mkuu wa Kituo cha Polisi Muze kilichopo Kata ya Muze wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa, Valentine James amebainisha hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi.

Amesema kuwa, katika dawati la jinsia lililopo katika kituo hicho kuna migogoro mingi iliyoripotiwa na wanandoa ambayo alieleza kuwa, chanzo chake ni kunyimana tendo la ndoa na imekuwa ikisababisha hasira baina yao.

Mkuu huyo wa kituo amesema kuwa, changamoto zaidi inakuwa kwa watoto wa wanandoa hao kwani wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili ikiwemo kupata vipigo kutoka kwa wazazi kutokana na hasira alizonazo.

''Mwanandoa anapokuwa na hasira na akashindwa kumuadhibu mwenzi wake amekua akihamishia hasira zake kwa watoto, hivyo wamekuwa wakipigwa na kuumizwa chanzo chake inakuwa ni hasira za mzazi kutokana na mgogoro wa ndoa pamoja na msongo wa mawazo alionao,''amesema.

Amesema kuwa, changamoto nyingine ni baadhi ya wanaume wamekuwa na tabia ya kuchukua mazao ya chakula nyumbani na kwenda kuyauza kisha kwenda kufanya starehe na wanawake wengine hali inayosababisha kuibuka migogoro katika familia zao.

James aliziomba taasisi za kidini pamoja na mashirika ya kijamii yanayojihusisha na kutoa ushauri kwa wanandoa kufika katika kata hiyo ili kutoa ushauri kwa kuwa kesi hizo zinazohusu ugomvi unaosababishwa na kunyimana tendo la ndoa zimekua zikiongezeka siku hadi siku.

Akizungumzia changamoto ya migogoro hiyo ya ndoa mtaalamu wa saikolojia aliyepo katika kituo cha afya Mazwi mjini Sumbawanga, Shangwe Braya amesema kuwa wapo baadhi ya wazazi ambao wakikosana hasira zao zinaishia kwa watoto kwa kuwapiga.

Braya amsema kuwa, ni vizuri wazazi wakatafuta njia nyingine ya kufikia suluhu ya matatizo yao na si vipigo kwa watoto, kwani wamekuwa wakiwaathiri kisaikolojia na kuwaharibia maisha yao.

Picha na iStock.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news