Mtanzania Hadija binti Kanyama ndiye kiziwi mrembo zaidi Duniani 2022

NA GODFREY NNKO

MTANZANIA Bi.Hadija Rajabu, binti Kanyama ameibuka kidedea katika Mashindano ya Utanashati, Urembo na Mitindo ya Viziwi Duniani ambayo yamefanyika hapa nchini Oktoba 29, 2022.
Hadija ambaye ndiye mrembo kiziwi duniani (Miss Deaf) kwa mwaka 2022 anatwaa ushindi huo ambao ulitwaliwa mwaka 2019 na Kemmonye Mamatsits wa Botswana kupitia mashindano yaliyofanyika Saint Petersburg nchini Urusi.
Huku kwa upande wa wanaume, mwanaume mtanashati kiziwi duniani kwa mwaka 2022 akiwa ni Gareth Kelaart kutoka nchini Australia.

Kelaart anachukua nafasi hiyo kutoka kwa Ajith Kumar ambaye alitwaa taji hilo mwaka 2019 akitokea nchini India.
Hadija ambaye alikuwa ni miongoni mwa wawakilishi sita wa Tanzania ambao nao pia wamefanya vizuri katika mashindano hayo, ana umri wa miaka 24 na amezaliwa Julai 8, 1998 huko Majengo Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.

Binti huyo ambaye elimu ya msingi aliipata huko Mwanga Viziwi mkoani Kilimanjaro mwaka 2006 hadi 2015 na elimu ya sekondari Moshi Ufundi kati ya mwaka 2016 hadi 2019 ndoto yake ni kuwa mwanamitindo mkubwa zaidi duniani.

Ametwaa taji hilo katika mashindano ya 12 duniani ambayo yamefanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika barani Afrika na Tanzania kuwa wenyeji wa kwanza.
Awali Rais wa Mashindano ya Urembo na Utanashati kwa Viziwi Duniani (MMDI),Bi.Bonita Ann Leek amesema, miongoni mwa sababu zilizowashawishi kuyaleta mashindano hayo hapa Tanzania ni pamoja na ukarimu, upendo na umoja wa Watanzania.

Tujikumbushe

Kwa nafasi hiyo ya mrembo na mtanashati, mwaka 2018 mshiriki kutoka nchini Italia, Natalia Comobo alitwaa taji huku mshiriki kutoka Kosovo, Mergim Koshai akitwaa taji la utanashati ambapo mashindano hayo yalifanyikia Taiwan.

Mwaka 2016 mshiriki kutoka nchini Poland, Iwona Cichosz alitwaa taji hilo na kuwa mrembo wa dunia huku mtanashati akiwa ni mshiriki kutoka Jamhuri ya Kenya, Calvin Vogefu ambapo mashindano hayo yalifanyikia Las Vegas nchini Marekani.

Aidha, mwaka 2014 mshiriki kutoka Jamhuri ya Korea Kusini, Yejin Kim alitwaa taji hilo huku nafasi ya utanashati ikichukuliwa na mshiriki kutoka nchini Marekani, Aaron Loggins ambapo mashindano hayo yalifanyikia London nchini Uingereza.

Kwa mwaka 2013 mrembo aliibuka mshiriki kutoka nchini Brazil, Lais Goncalves huku mtanashati akiibuka mshiriki kutoka nchini Ujerumani, Rafael Grombelka ambapo mashindano hayo yalifanyikia huko Sofia nchini Bulgaria.

Wakati huo huo, mwaka 2012 mrembo katika mashindano hayo ya dunia aliibuka mshiriki kutoka Belarus, Natalia Ryabova huku mtanashati akiibuka mshiriki kutoka nchini Uturuki, Cevat Simsek ambapo mashindano hayo yalifanyikia jijini Ankara huko Uturuki.

Kwa upande wa mwaka 2011 mrembo katika mashindano hayo aliibuka raia wa Jamaica, Cassandra Whyte huku mwaka 2010 akiibuka kidedea mshiriki kutoka Ufaransa, Julie Abbou ambapo mashindano hayo yalifanyikia huko Las Vegas nchini Marekani.
Mashindano hayo ambayo yaliwakutanisha pamoja wadau mbalimbali wa Kitaifa na Kimataifa wakiwemo wanadiplomasia na viongozi wa Serikali, mgeni rasmi alikuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye aliwakilishwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mheshimiwa Dkt.Dorothy Gwajima.

Aidha, mbali na Rais wa Mashindano ya Urembo na Utanashati kwa Viziwi Duniani (MMDI),Bi.Bonita Ann Leek pia Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa naye alikuwa mgeni maalumu.

Katika hatua nyingine, wakati akizungumza na waandishi wa habari awali, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt.Hassan Abbas alibainisha kuwa, Serikali pia imewapa zawadi washindi wote wa shindano hilo la kidunia na viongozi wao kutembelea mbuga ya wanyama ya Ngorongoro Oktoba 31,2022 ikiwa ni mwendelezo wa Royal Tour iliyoasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Dkt.Abbas amefafanua kuwa, miongoni mwa sababu zinazoendelea kuifanya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kuaminika na kupewa kipaumbele katika masuala mbalimbali duniani achilia mbali ukarimu, umoja na upendo ni pamoja na utulivu na amani ambayo imetawala kila mahali.
Pia amesema, Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio mbalimbali kuanzia Bara na Visiwani ambavyo kila mgeni akivisikia anatamani kufika ili kuja kufurahia maisha.

"Hapa Tanzania tumejaliwa kuwa na vivutio vingi kuna Serengeti, Ngorongoro, Zanzibar na maeneo mengine mbalinbali ya vivutio vizuri vya kwenda kurelax. Kwa Tanzania tangu mashindano haya yaanze kufanyika, Tanzania ni nchi ya 12 na kwa mara ya kwanza mashindano haya yalifanyika Las Vegas nchini Marekani mwaka 2010,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news