NHC yaja na siku 60 za 'moto' wapangaji mguu ndani, mguu nje

NA GODFREY NNKO

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limetangaza kuanza kampeni kabambe ya miezi miwili kuanzia sasa ambayo inalenga kukusanya madeni kwa wapangaji wa nyumba zake waliopo na waliohama kote nchini ambayo yanakadiriwa kufikia zaidi ya shilingi bilioni 20.

"Kwa hiyo tumeamua sasa kufanya kampeni ya kukusanya madeni haya, niseme tu kwamba kuanzia Novemba Mosi, 2022 hadi Desemba 30, 2022, takribani miezi miwili tunaanzisha kampeni ya kukusanya madeni haya.

"Wapo wapangaji katika nyumba zetu ambao wanadaiwa kodi na malimbikizo, natoa rai waende katika ofisi za Shirika la Nyumba la Taifa mahali popote zilipo karibu nao waweze kulipa kodi zao kwa wakati, baada ya miezi miwili tutachukua hatua mbalimbali ikiwemo hatua ya kisheria kukamata mali zao na kuweza kuzinadi kufidia kodi ambayo tunawadai na pia tutawanyang'anya upangaji kwa sababu watakuwa wamevunja wenyewe mkataba wa upangaji na kuweza kuwapatia Watanzania wengine;

Meneja Habari na Uhusiano wa NHC,Bw.Muungano Saguya ameyasema hayo leo Oktoba 30, 2022 katika ofisi za makao makuu ya shirika hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na kampeni hiyo ya miezi miwili itakayoongozwa na kauli mbiu ya LIPA KODI YA NYUMBA KWA MAENDELEO YA TAIFA LETU.

Madeni sugu

Saguya amesema, awali shirika hilo lilikuwa linadai madeni ambayo yanafikia shilingi bilioni 26, lakini baada ya ufuatiliaji shilingi bilioni tano zimelipwa huku tathimini na uchambuzi waliyofanya ukionesha kuwa zaidi ya shilingi bilioni sita kati ya fedha hizo huenda zisilipike kutokana na sababu mbalimbali.

Miongoni mwa sababu hizo, Bw.Saguya amesema ni pamoja na wadaiwa (wapangaji) kufariki,kuhama na baadhi ya kampuni kufilisika hivyo wapo katika mchakato wa kuomba kibali kutoka bodi ili kuona namna ya kumalizana na kadhia hiyo, wakati kampeni pia ikiendelea kufuatilia madeni mengine.

"Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kama mnavyofahamu tumekuwa tukiwaambia tunawadai wapangaji wetu malimbikizo makubwa ya kodi, kama mnavyofahamu tuliweza kuwambia kipindi cha nyuma yanafikia shilingi bilioni 26 hizi ni fedha nyingi sana za umma ambazo zingetumika kufanya mambo mengi ikiwemo ujenzi wa nyumba na matengenezo ya nyumba zetu.

"Lakini tuliwaambia tunafanya kampeni kubwa ya kukusanya madeni hayo, na kweli tumefanya kampeni hiyo kwa kufuatilia kila mahali na kila mdaiwa na wapo wadaiwa wengine ambao ni waungwana wamejaribu kulipa madeni hayo na malimbikizo wanayodaiwa.

"Na wengine wameweka utaratibu wa namna ya kukamilisha madeni hayo, kwa hiyo kutoka shilingi Bilioni 26 ambayo tuliwaambia tunadai tulifanikiwa kipindi ambacho tuliwaambia tunakusanya madeni hayo, tumefanikiwa kukusanya shilingi bilioni tano.

"Na yapo madeni baada ya kufanya uchambuzi wa kina yanafikia takribani shilingi bilioni sita, haya yanahitaji kibali cha Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuweza kuyafuta kwa sababu hayakusanyiki kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo baadhi ya makampuni kufilisika na baadhi ya wapangaji wetu kufariki.

Juhudi kubwa

"Kwa hiyo unaweza ukaona kuna deni lilikuwepo tukalipunguza na kuna lingine ambalo tunahitaji kuliondoa kutokana na kwamba halikusanyiki, lakini yapo madeni mapya yanayozalishwa kutokana na bili tunazofanya kila mwezi, Shirika la Nyumba linatoa ankara kila mwezi zinazofikia takribani shilingi Bilioni 8.3 Sasa kadri unavyotoa ankara zile unazokusanya kuna kiasi kingine kinabakia.

"Lakini pia wapo wapangaji ambao walikuwa wakikaa kwenye nyumba zetu na walihama wameondoka bila kutoa taarifa wakiwa na madeni, sisi katika shirika tuna njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya dola kuhakikisha kwamba tunawapata watu hao, zipo mamlaka ambazo zinaweza kufahamu uko wapi.

"Sisi tunaenda kutumia mamlaka hizo kuweza kufahamu walipo hawa wapangaji na madeni yetu. Ili hatimaye tuweze kukusanya kodi hizo ambazo kimsingi ni mali za Watanzania wote,"amesema Bw.Saguya.

Shukurani

Katika hatua nyingine, Bw.Saguya amesema, NHC inawashukuru wapangaji wote ambao wamekuwa wakitimza wajibu wao wa kulipa kodi kwa wakati.

"Nipende kusema kwamba, shirika linawashukuru kwa dhati kabisa wapangaji wote ambao wamekuwa wakitimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa wakati, kama mnavyofahamu nyumba hizi ni mali ya Watanzania wote na nyumba hizi takribani 17,111 zipo maeneo mbalinbali nchini Tanzania, kwa hiyo unaweza ukasema nyumba za shirika ziko chini ya asilimia moja ya nyumba zote zilizoko nchini.

Nyumba zinahitajika

"Kwa maana hiyo kila Mtanzania ana haki ya kukaa kwenye nyumba hizo, shirika kila mwezi tunapokea maombi ya wapangaji wapya wanayofikia 200, unaweza kuona kwamba kila mwaka tunapokea maombi yasiyopungua 2,400.

"Hata hivyo sisi shirika hatuna uwezo wa kutimiza maombi hayo mapya kwa sababu nyumba zetu tayari zimejaa. Sasa niseme tu kwamba wajibu wa mpangaji anayeweza kukaa kwenye nyumba hizi za shirika ambazo ni mali ya umma ni kulipa kodi tu.

"Kinyume cha hapo hatakuwa na uhalali huo kwa sababu Watanzania wengi wanataka kuingia kwenye nyumba hizi wanashindwa kwa sababu nyumba zimejaa na kuna Watanzania wamepata bahati ya kukaa kwenye hizi nyumba na wanashindwa kulipa kodi kwa wakati.

"Ni wakati mwafaka kwa wapangaji ambao wanashindwa kulipa kodi wajitafakari, na wale wote walikuwa kwenye nyumba za shirika wakawa wameacha madeni waende kwenye ofisi za shirika popote walipo waweze kulipa madeni yao, baada ya miezi miwili tulioutoa tutatangaza majina yao kwenye vyombo vya habari ili Watanzania waweze kuwafahamu watu wanaohujumu shirika lao,"amesema.

Msese

Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi Milki wa NHC, Eliah Msese amewaasa watanzania wote kutotumia vishoka wanaojifanya kutoa msaada wa upatikanaji wa nyumba za shirika hilo.

Msese amesema, kila mwananchi mwenye uhitaji na nyumba za shirika hilo anapaswa kufika katika ofisi zao
zilizopo nchini kote ili kuwa na uhakika wa umiliki wa nyumba hizo.

Pia amesema kuwa, upo utaratibu mzuri uliowekwa wa kuhakikisha mwananchi anapata nyumba bila kutumia vishoka na kwamba kwa kufuata utarabu huo kutasaidia kuondokana na tatizo la vishoka.

Mbilinyi

Naye Meneja Ukusanyaji Madeni kutoka NHC,Bw.Levinico Mbilinyi amesema kuwa, NHC inapokea maombi mengi ya wapangaji wapya ambayo yanaonesha uhitaji ni mkubwa wakati wengine wakishindwa kutumia vema nyumba hizo kwa kulipa kodi kwa wakati.

“Maombi haya ambayo hata hivyo hayawezi kutimizwa na shirika kutokana na nyumba kuwa chache, yanaonyesha Watanzania wengi wanazihitaji nyumba hizi za shirika. Kwa hiyo uhalali wa wapangaji kuendelea kuwa katika nyumba za Shirika la Nyumba utakuwepo tu kwa kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa wakati.

"Pia ni kosa la kimkataba mpangaji kupangishwa kwenye nyumba ya NHC na mtu mwingine, yule mtu anapokuja kushindwa kulipa kodi sisi tunapofanya ufuatiliaji, tunafanya ufuatiliaji ya yule mtu ambaye tuna mkataba naye kwa hiyo yule mpangaji ataingia hasara kwa sababu tutachukua vyombo, tutakwenda kuviuza ili kufidia lile deni wakati yeye anamlipa huyo mtu wa kati wake. Hivyo, tunawasihi wananchi wasipangishwe na mtu mwingine nje ya NHC,"amesema Bw.Mbilinyi.

Madeni ya Serikali je?

Meneja Habari na Uhusiano wa NHC,Bw.Muungano Saguya amefafanua kuwa,taasisi za Serikali zinazodaiwa na shirika hilo zipo katika hatua za mwisho kuyakamilisha.

"Madeni tunayodai taasisi za Serikali hayazidi shilingi Bilioni 3.3 na hayo madeni tayari tumeshafanya mazungumzo na Serikali kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

"Na tayari, taasisi mbalimbali za serikali zinazodaiwa zimeshaenda kufanya uhakiki wa madeni yao na tumeshawekeana utaratibu wa kulipa madeni yao. Kwa hiyo, kule (serikalini) hakuna shida, shida kubwa ipo kwa wapangaji binafsi ambao wengine wameondoka na madeni.

"Wapo vishoka kama ilivyo kwenye taasisi nyingine, wapo watu wanaofanya michezo michezo sisi kama shirika tunafahamu na tumekuwa tukishirikina na Jeshi la Polisi na tunawakamata,wengine wapo kwenye vyombo vya sheria.

Muhimu

Bw.Saguya amefafanua kuwa, "Kwa hiyo tumeshatangaza mtu yeyote anayepangishwa kinyemela katika nyumba za shirika, aje ofisi za shirika atoe taarifa kwamba amepangishwa na fulani, analipa kodi kiasi hiki wakati kodi halisi ni kiasi hiki.

"Sisi tutampa mara moja upangaji, kuliko kwenda kupangishwa na mtu anatumia nyumba ya shirika kama nyumba yake binafsi, anakupangisha na kwa nini ukubali kupangishwa kimsingi na wewe una uhalali wa kupangishwa kwa kufuata taratibu.

"Kwa hiyo tunatoa rai kwa mtu ambaye amepangishwa kiholela ajisalimishe kwenye shirika na sisi tutampa upangaji kwa utaratibu wa kisheria,"amesisitiza Bw.Saguya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news