'Nabi bado yupo sana'

NA DIRAMAKINI

UONGOZI wa Klabu ya Yanga yenye maskani yake mitaa ya Jangwani jijini Dar es Salaam umefafanua kuwa, Kocha Mkuu Nasreddine Nabi bado yuko kwenye safu ya klabu hiyo, na kukanusha madai kuwa ametimuliwa.

Awali yalizushwa madai kuwa, pande hizo mbili kwa maana ya uongozi wa klabu hiyo na kocha zimetofautiana, hivyo kumtaka Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, CEO Andre Mtine kuvunja ukimya kuhusu sakata hilo Oktoba 25, 2022.


Kupitia programu tumishi ya Yanga (Yanga App), CEO Mtime alinukuliwa akisema: “Uongozi wa Yanga unawataarifu wanachama na mashabiki kuwa Nasreddine Nabi bado ni Kocha Mkuu wa timu yetu.”

Kisha akatumia jukwaa hilo kuishauri familia ya Yanga kuthibitisha kila mara taarifa zinazohusu klabu hiyo kupitia chaneli zake rasmi za vyombo vya habari kama vile Yanga App, tovuti na mitandao ya kijamii.

Taarifa za Yanga App zinaonesha zaidi kwamba uongozi unamtakia Nabi na benchi lake la ufundi kila la heri katika mechi yao ya leo dhidi ya KMC itakayochezwa katika dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

"Tunafahamu kuwa ratiba yetu ni ngumu, tunafanya kila jitihada kuendana na uhalisia unaotukabili kwa sasa. Tuna mechi ngumu mbele yetu na huo ndio ukweli ambao tunapaswa kupambana nao. Sio suala la nani atacheza ni suala la alama tatu," amesema Kocha Mkuu Nasreddine Nabi.

Post a Comment

0 Comments