Newala Mji yaanza kutekeleza maagizo ya Waziri wa Ardhi

NA MWANDISHI WETU-WANMM

HALMASHAURI ya Mji wa Newala Mkoa wa Mtwara imeanza kutekeleza maagizo ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Mhe.Dkt.Angeline Mabula ya kuzitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha zinapima na kumilikishwa maeneo yake yakiwemo ya shule, zahanati na vituo vya mabasi ili kuepuka migogoro ya ardhi. Watumishi wa sekta ya ardhi wakitoa huduma za ardhi katika kituo jumuishi Mtwara.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Newala, Shamim Daudi Mwariko amekabidhiwa jumla ya hati saba na Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mtwara, Rehema Mwinuka ambapo hati tano kati ya alizokabidhiwà ni za shule za msingi na hati mbili ni za zahanati.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Newala mkoani Mtwara, Shamim Daudi Mwariko (kulia) akikabidhiwa hatimiliki za ardhi saba na Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mtwara, Rehema Mwinuka mkoani Mtwara.

Shule za msingi zilizopata hatimiliki za ardhi ni Mtangalanga, Kiduni, Butiama, Mcholi II na Mkoma I huku upande wa zahanati zikiwa ni Mkoma I na ile ya Makondeko.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi hati hizo mkoani Mtwara, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Mtwara, Rehema Mwinuka ameipongeza Halmashauri ya Mji wa Newala kwa uamuzi wa kupimiwa maeneo yake na kuzitaka halmashauri nyingine katika mkoa huo kuiga mfano wa halmashauri hiyo kwa kupima na kumilikishwa maeneo yake ili kuepuka uvamizi katika maeneo hayo.
Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mtwara, Rehema Mwinuka (kulia) akimsikiliza mmoja wa wateja wakati Ofisi ya Ardhi Mkoa ilipotoa huduma jumuishi za sekta ya ardhi.

“Nichukue fursa hii kuwapongeza halmashauri ya Mji wa Newala kwa uamuzi wenu wa kupima maeneo yenu, hii itasaidia sana kupunguza migogoro ya ardhi inayotokana na uvamizi na niombe hakmashauri nyingine ziige mfano wenu,”amesema Rehema.

Mbali na kukabidhi hati kwa Halmahauri ya Mji wa Newala, Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mtwara amewaongoza watumishi wa mkoa wake kutoa hati kwa wamiliki wa ardhi waliokamikisha taratibu za kupatiwa hati sambamba na kusikiliza na kutatua changamoto za sekta ya ardhi katila kituo jumuishi.
Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mtwara, Rehema Mwinuka akiwa katika picha ya pamoja na wananchi aliowakabidhi hati.(PICHA NA WIZARA YA ARDHI).

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanzisha utaratibu wa ofisi zake za ardhi katika mikoa kuwa na vituo jumuishi vya kusikiliza na kutatua changamoto za ardhi pamoja na kutoa hatimiliki za ardhi ikiwa ni juhudi za kusogeza huduma karibu na wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news