NHC yapiga tafu ujenzi wa madarasa wilayani Butiama

NA FRESHA KINASA

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limekabidhi msaada wa vifaa vya ujenzi ikiwemo saruji mifuko 91, nondo 26 na misumari vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 2.5 kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Sekondari Busegwe inayojengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Butiama mkoani Mara.
Msaada huo umekabidhiwa Oktoba 3, 2022 eneo hilo la ujenzi wa shule hiyo katika Kata ya Busegwe na Meneja wa NHC Mkoa wa Mara, Eliaisa Keenja kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Bw.Nehemia Mchechu.

Keenja amesema, wametoa msaada huo kufuatia maombi yaliyotolewa na wadau wa maendeleo kutoka kata hiyo walioomba wasaidiwe ujenzi wa jengo hilo linalojengwa kwa michango ya wadau kufuatia maboma mawili kukamilika kutokana na michango na nguvu kazi za wananchi.
Msaada huo unalenga kukamilisha boma hilo ili Serikali ikamilishe hatua ya kuezeka kusudi yawasaidie wanafunzi wa kata hiyo wanaotembea kwenda kusoma katika Shule ya Sekondari Butuguri umbali mrefu wa kilomita 14.

"Shirika la NHC limekuwa likisaidia kuunga mkono juhudi mbalimbali za maendeleo zinazofanywa na serikali kwa jamii. Na ndio maana tumekabidhi vifaa hivi visaidie ujenzi wa jengo hili ambalo linajengwa kwa nguvu za wadau wa maendeleo nasi tukiwa sehemu ya wadau wa maendeleo tumeona tutoe msaada huu usaidie watoto ambao wanatembea umbali mrefu kama tulivyoambiwa wasome karibu na kwao,"amesema Keenja.
Mwenyekiti wa wadau wa ndani wa maendeleo, Richard Mkoji amesema, zamani ilikuwa kata moja ya Butuguri baada ya kutengwa wakaona ni vyema waanzishe shule hiyo wawasaidie watoto wao ili kuepuka adha ya kutembea umbali wa kilomita 14 kwenda Butuguri kusoma.

"Tuliwaomba NHC watusaidie kukamilisha boma letu walau watupe saruji na nondo, bahati nzuri wametupatia msaada huo tunashukuru sana kwa msaada wao na niombe wadau mbalimbali watusaidie kujenga shule hii ambayo itakuwa mwarobaini kwa watoto wetu kutembea umbali mrefu na kuepukana na vishawishi njiani kutoka kwa madereva bodaboda.
"Kata yetu ya Busegwe ina vijiji vitatu ambavyo ni Nyanza, Busegwe na Kigori ujenzi huu unafanywa kwa nguvu za wananchi kujitolea kwa kushirikiana na wadau ulianza mwaka jana matarajio yetu yakienda vizuri ninaamini serikali itamalizia hatua ya mwisho ya kukamilisha ili kusudi shule ianze maana pia ujenzi wa nyumba ya mwalimu unaendelea kwa nguvu za wananchi,"amesema Mkoji.

Ibrahimu Bukume ni Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Busegwe amelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa kwa kuunga mkono utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kupitia msaada huo.

"Chama Cha Mapinduzi kinefurahi kwa hatua hii muhimu ambayo NHC wamefanya Kama wadau wa Maendeleo kuunga juhudi za Serikali inayoongozwa na CCM ninaamini kabisa msaada wao utakamilisha boma na pia niombe wadau wajitokeze kushiriki shughuli hii na kuchangia maendeleo mbalimbali,"amesema Bukume.
Neema Japheti ni Mkazi wa Busegwe (54) ambapo ameieleza DIRAMAKINI kuwa, wanafunzi wamekuwa wakitembea umbali mrefu kwenda shule na kwamba watoto wa kike wamekuwa wakipata vishawishi wakiwa njiani kutoka kwa waendesha bodaboda na pia kufika wakiwa wamechoka shuleni hali ambayo inaathiri maendeleo yao kitaaluma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news