NYAMAPORI YA KUCHOMA PANDE:TAWA na wake wapambe, wameandaa kwa zamu

NA LWAGA MWAMBANDE

MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ni miongoni mwa taasisi za umma chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo ina jukumu la kusimamia rasilimali husika kwa ustawi bora wa kizazi cha sasa na kijacho.

TAWA imeanzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 8 cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya mwaka 2009 (Sura ya 283), kupitia Tangazo la Serikali Na. 135 lililochapishwa Mei 9, 2014.

Aidha, ilianza kufanya kazi Julai Mosi, 2016 ikiwa na majukumu ya msingi ya uhifadhi wa bayoanuai na usimamizi endelevu wa rasilimali za wanyamapori nje ya Hifadhi za Taifa na Hifadhi ya Ngorongoro.

Hii inajumuisha kusimamia jumla ya eneo la kilomita za mraba 136,287.06 linalojumuisha Mapori ya Akiba, na Maeneo Yanayodhibitiwa nchini, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake.

TAWA licha ya kutegemea uhifadhi na utalii, wameongeza nguvu kwa kufungua mabucha ya nyamapori, vitalu vya uwindaji wa kitalii na utalii wa picha,uwekezaji wa hoteli na kambi za kitalii ukiwemo uwekezaji mahiri nchini.

Novemba 5, 2022 katika Hifadhi ya Pori la Akiba Pande iliyopo nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam kuna jambo kubwa, hili ni mojawapo ya pori linalosimamiwa na TAWA ikiwa ni kilomita zaidi ya 40 kutokea katikati ya jiji hilo la kibiashara kuelekea Bagamoyo na unapokaribia kufika Kituo cha Bunju B mkono wa kushoto kuna bango kubwa linaloonesha njia ya Mabwepande ambapo ni kilomita nane mpaka hifadhini.

Ni hifadhi yenye wanyama wadogo mbalmbali achilia mbali miti ya tao la Pwani. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema,tayari amejiandaa kwa Novemba 5, mwaka huu ili aweze kwenda kuonja nyama ya wanyamapori katika tukio maalumu lililoandaliwa na TAWA kwa ajili ya Watanzania na wageni mbalimbali, endelea;


1:Kuna nyama choma Pande, Jijini Dar es Salaam,
Twakusihi chondechonde, hili jambo lifahamu,
Ni nyamapori vipande, kaonje wake utamu,
Ni hapo Novemba tano, tembelea burudika.

2:Huu mpango kabambe, ambao kwetu muhimu,
TAWA na wake wapambe, wameandaa kwa zamu,
Nenda mbio ukatambe, kisha nyama choma tamu,
Ni hapo Novemba tano, tembelea burudika.

3:Ni utalii wa ndani, kwetu sote ni muhimu,
Rasilimali za ndani, kuzitumia muhimu,
Tembelea nenda ndani, ukafaidi kwa zamu,
Ni hapo Novemba tano, tembelea burudika.

4:TAWA wameshatangaza, sasa ni ya kwetu zamu,
Pande kwenda jisogeza, kwa siku hiyo muhimu,
Kwa afya kujihimiza, mazoezi ni muhimu,
Ni hapo Novemba tano, tembelea burudika.

5:Nyama pori ya kuchoma, hujaionja utamu,
Ni mbalimbali wanyama, kitaka onja kwa zamu,
Ukionja ninasema, tafika zamu kwa zamu,
Ni hapo Novemba tano, tembelea burudika.

6:Jinsi unavyoshiriki, kuipata nyama tamu,
Ni njia ya kubariki, shughuli ile muhimu,
Yaani unatia tiki, uhifadhi ni muhimu,
Ni hapo Novemba tano, tembelea burudika.

7:Unataka nyama gani, uonje wake utamu?
Wala wanyama porini, udhaniao watamu?
Fika Pande ni nyumbani, uonjeonje kwa zamu,
Ni hapo Novemba tano, tembelea burudika.

8:TAWA tunawapongeza, kwa uamuzi muhimu,
Hifadhi kuendeleza, nasi tule nyama tamu,
Ni lishe itaongeza, kwa afya za wanadamu,
Ni hapo Novemba tano, tembelea burudika.

9:Mimi ninajiandaa, kwenda kula nyama tamu,
Sitabaki kushangaa, huku nabaki na hamu,
Nenda nikamle paa, hadi iniishe hamu,
Ni hapo Novemba tano, tembelea burudika.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments