RAIS WETU SAMIA ANAO UBINADAMU: Kulipwa michango yao, waloachishwa ni vema

NA LWAGA MWAMBANDE

OKTOBA 26, 2022 Waziri wa Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameridhia watumishi walioondolewa kazini kwa kughushi vyeti kurejeshewa michango yao.
Ni waliyochangiwa katika Mifuko ya Hifadhi ambayo kwa Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ni asilimia tano na kwa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ni asilimia 10 ya mshahara.

Mheshimiwa Waziri Prof.Ndalichako ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma huku akifafanua kuwa,marejesho ya michango yataanza rasmi kutolewa Novemba Mosi, 2022 na amezitaka mamlaka husika kukamilisha malipo hayo kwa haraka zaidi.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande licha ya kupongeza uamuzi huo wa hekima na busara wa Rais Samia, anawasisitiza walengwa kuhakikisha wanazingatia maelekezo ya Serikali ikiwemo kuwa na nyaraka zinazotakiwa ili kufanikisha mchakato huo.

Miongoni mwa nyaraka hizo ni picha mbili ndogo na nakala za kibenki yaani ambazo zinaonesha akaunti iliyo hai, kwani malipo hayo hayatolewi fedha taslimu na kitambulisho, endelea;

1:Rais wetu Samia, anao ubinadamu,
Yake ukiangalia, kwa kweli yatia hamu,
Twafurahi twasikia, mema yale yanadumu,
Kulipwa michango yao, waloachishwa ni vema.

2:Sijui sababu Samia, jinale lavuta hamu?
Suluhu kashikilia, kuyaondoa magumu?
Haya anatufanyia, yafaa hadi dawamu,
Kulipwa michango yao, waloachishwa ni vema.

3:Nchi walitumikia, wakishika majukumu,
Kazi walitufanyia, kila mtu yake zamu,
Pale walipotitia, nao ni ubinadamu,
Kulipwa michango yao, waloachishwa ni vema.

4:Kazi kuwakatikitia, wengi hali zao ngumu,
Kipato kujipatia, kwao ni sintofahamu,
Makato kijipatia, ni nafuu twafahamu,
Kulipwa michango yao, waloachishwa ni vema.

5:Ndiye Rais Samia, ambaye kashika zamu,
Watu awaangalia, roho ya ubinadamu,
Mema anawafanyia, nao wapate jikimu,
Kulipwa michango yao, waloachishwa ni vema.

6:Makubwa atufanyia, yajaa ubinadamu,
Machache kikutajia, utazipata salamu,
Mengine twaaminia, yatazidia kutimu,
Kulipwa michango yao, waloachishwa ni vema.

7:Walo walolialia, bila kupata hukumu,
Lupango kuzungukia, bila kesi kufahamu,
Wengi aliwaachia, sasa tuko nao humu,
Kulipwa michango yao, waloachishwa ni vema.

8:Lissu kutokutajia, kwangu takuwa vigumu,
Risasi zilipomwingia, sote hilo twafahamu,
Ni Mama yetu Samia, sipitali alitimu,
Kulipwa michango yao, waloachishwa ni vema.

9:Hata tunaangalia, kwa wake ubinadamu,
Kazi anatufanyia, tupunguzia ugumu,
Vituo afya zidia, na kupanua elimu,
Kulipwa michango yao, waloachishwa ni vema.

10:Wale wamshambulia, kama ya kwao magumu,
Wengine wafurahia, hatua zake muhimu,
Haya amewafanyia, kwao ni zawadi tamu,
Kulipwa michango yao, waloachishwa ni vema.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news