Rais Dkt.Mwinyi:Tunzeni miundombinu hii ya TEHAMA

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema uzinduzi wa minara ya mawasliano ya simu kwa kiasi kikubwa itaiwezesha Zanzibar kuingia katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akipata maelezo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Tanzania, Bi. Joustine Tmashiba, wakati akitembelea Kituo cha TEHAMA baada ya kukifungua Oktoba 26,2022 katika eneo la Bwefum Wilaya ya Magharibi “B” Unguja.(Picha na Ikulu).

Mheshimiwa Rais amesema hiyo ni fursa muhimu kwa wananchi pamoja na kukua kwa sekta ya uwezeshaji kiuchumi.

Amesema hayo katika ufunguzi wa minara 42 pamoja na vituo 11 vya TEHAMA huko Bwefuu Mkoa Mjini Magharibi iliyojengwa kupitia fedha za Ruzuku za mfuko wa Mawasiliano kwa Wote.

Amesema, matumizi ya huduma za mawasiliano kwa sasa hayaepukiki kwa sababu mawasiliano yanagusa moja kwa moja maisha ya wananchi, ikiwemo walioko vijijini katika shughuli zao za kila siku.

Akitolea mfano, Dkt.Mwinyi amesema, matumizi ya TEHAMA yamekuwa yakiongezeka ikiwemo maeneo ya vijijini na kuchukua fursa kubwa za kiuchumi na hivyo kuongeza kipato cha wananchi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa Tuzo Maalum kwa pamoja na Mawaziri wa SMZ na SMT (kulia kwa Rais) Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Tanzania.,Mhe. Nape Mnauye na (kushoto kwa Rais) Waziri wa Ujenzi Mawasiliani na Uchukuzi Zanzibar, Mhe.Dkt. Khalid Salum Mohamed, baada ya ufunguzi na kukabidhi Kituo cha TEHAMA Bwefum Wilaya ya Magharibi “B” Unguja.(Picha na Ikulu).

“Nachukua nafasi hii kuupongeza Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kwa kushirikiana na kampuni za Tigo/Zantel katika ujenzi wa minara 42 na vituo 11 vya TEHAMA hatua hii inakwenda kufungua fursa muhimu za uwekezaji na kiuchumi,”amesema.

Pia Dkt.Mwinyi amewataka wakazi wa maeneo hayo kuitunza miundombinu hiyo na kuilinda dhidi ya uharibifu unaoweza kurudisha nyuma hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa.

Amesema miundombinu hiyo inahitaji kutunzwa na kuenziwa ili kuepuka uharibifu unaoweza kufanywa, hivyo akachukua fursa hiyo kuwataka viongozi wa Shehiya kuhakikisha inalindwa.
Naye Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Dkt.Khalid Salum Mohammed amesema uzinduzi wa minara hiyo ni sehemu ya ahadi ya kufikisha mawasiliano vijini na kuondosha kabisa tofauti iliyopo kati ya maeneo ya mijini na vijiji.

“Kinachofanyika leo ni kufikisha huduma za maendeleo kwa kasi kubwa ya kufikisha huduma za mawasiliano hadi vijijini ili kuondosha tofauti na pengo la huduma hizo na kufika hadi vijijini,”amesema.

Mapema,Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye aliupongeza Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ambayo ni Taasisi ya Muungano kwa kwa kazi kubwa ya kufikisha huduma za mawasiliano ya intaneti kwa wanafunzi wa skuli 29 za Zanzibar pamoja na vifaa vyake, hatua ambayo itatoa nafasi nzuri kwao kufahamu matumizi ya TEHAMA na kuongeza ufaulu.
Katika hatua nyingine, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Justine Mashimba alisema wamejipanga kikamilifu kuhakikisha mawasiliano yote yanafika vijijini ili wananchi waweze kutumia fursa za kiuchumi.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mawasiliano na Miundombinu Suleiman Kakoso alizipongeza Serikali zote mbili kwa kuweka mikakati ya kuimarisha mundombinu ya mawasiliano, ambapo sasa yanakwenda kufungua huduma za mawasiliano na TEHAMA hadi vijijini.

Post a Comment

0 Comments