BoT,Frontclear wasaini mkataba wa kihistoria kukuza masoko ya fedha Tanzania

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) na Taasisi ya Kimataifa ya Frontclear ya Amsterdam nchini Uholanzi wamesaini Mkataba wa Makubaliano (MOU) ili kuchochea maendeleo ya fedha na masoko baina ya benki na sekta za kifedha hapa nchini.

Naibu Gavana, Sera za Uchumi na Fedha, Dkt.Yamungu Kayandabila na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Maendeleo ya Masoko ya Fedha- Frontclear, Bw. Philip Buyskes.
 
Mkataba huo umesainiwa jioni ya Oktoba 26, 2022 mbele ya wawakilishi mbalimbali wa benki, taasisi za kifedha na madalali katika Ukumbi wa BoT jijini Dar es Salaam.

Huu unatajwa kuwa miongoni mwa mikataba ya kihistoria ambapo taasisi hiyo ya Kimataifa inakwenda kuwezesha udhamini kwa benki na taasisi mbalimbali za fedha hapa nchini kukuza mitaji yao ili kuweza kuhudumia wananchi kikamilifu mijini na vijijini.

Licha ya majukumu mengine, Benki Kuu ya Tanzania ina mamlaka ya kutoa leseni, kudhibiti na kusimamia benki na taasisi za fedha zikiwemo benki za biashara, taasisi za huduma ndogo za fedha, benki za jamii, benki za maendeleo, kampuni za karadha (credit card), taasisi za mikopo ya nyumba, watoa huduma ndogo za fedha, taasisi za taarifa za wakopaji, maduka ya kubadilisha fedha za kigeni na ofisi za uwakilishi za benki zilizoko nje.

Pia, Benki Kuu ina wajibu wa udhibiti na usimamizi wa masuala ya kifedha (uwekezaji) wa mifuko ya hifadhi ya jamii nchini Tanzania. Jukumu la msingi katika udhibiti na usimamizi wa taasisi za fedha ni kuhakikisha kuna uthabiti, usalama na ufanisi wa mfumo wa fedha na kupunguza uwezekano wa wenye amana kupata hasara.

ECA

Mkuu wa Fedha, Ubunifu na Masoko ya Mitaji, Idara ya Maendeleo ya Sekta Binafsi na Fedha katika Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa barani Afrika (ECA), Bi.Sonia Essobmadje amesema kuwa,kusainiwa kwa mkataba wa makubaliano kati ya BoT, Frontclear na kamisheni hiyo, kunaonesha dhamira ya pamoja ya kuendeleza soko la fedha la Tanzania, ikiwa ni pamoja na soko shirikishi zaidi la benki na soko la dhamana nchini.
"Masoko ya fedha yaliyo imara zaidi na jumuishi ni fursa muhimu katika kukuza uchumi.Msingi wa soko la fedha ni utoaji wa mikopo baina ya benki, ambapo benki hukopa na kukopeshana kwa kutumia vyombo vya fedha kama vile kuingia mikataba, dhamana na mingineyo kwa mizania nzuri.

"Benki Kuu na benki zinategemea masoko ya baina ya benki kushughulikia matatizo ya haraka katika ukwasi na kuleta mabadiliko chanya katika sera ya fedha,"amesema.

ECA iliyoanzishwa na Baraza la Uchumi na Kijamii (ECOSOC) la Umoja wa Mataifa (UN) mwaka 1958 kama moja ya tume tano za kanda za Umoja wa Mataifa, jukumu lake ni kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi wanachama wake, kukuza ushirikiano wa kikanda, na kukuza ushirikiano wa kimataifa kwa maendeleo ya Afrika.

Kamisheni hiyo, inaundwa na nchi 54 wanachama barani Afrika, na ina jukumu la pande mbili kama tawi la kikanda la Umoja wa Mataifa na kama sehemu muhimu ya mazingira ya kitaasisi ya Afrika, ECA ipo katika nafasi ya kutoa michango ya kipekee kushughulikia changamoto za maendeleo barani Afrika.

Naibu Gavana

Naye Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt.Yamungu Kayandabila amesema,mbali na taasisi hiyo kutoa dhamana pia wanatoa mafunzo kwa washiriki kwenye masoko ya fedha.

"Kwa hiyo tutakuwa tunapata mafunzo mbalimbali kwa maana ya watu wetu wa Tanzania, kwa ujumla sekta ya fedha nchini,"amesema Dkt.Kayandabila.
Pia amesema, Frontclear kutoka nchini Uholanzi ikiwa ni taasisi ya kifedha imekuwa ikishirikiana na nchi hasa benki kuu za nchi husika katika kukuza msoko ya fedha.

"Katika kukuza masoko ya fedha wanafanyaje? Ni sehemu fulani ya kuimarisha ukwasi, tunapozungumza kuhusu ukwasi tunazungumzia dhana pana katika soko,kwa mfano mabenki tunafahamu yanakopeshana yenyewe kwa yenyewe wakati mwingine zile benki kubwa huwa sio rahisi kuzikopesha benki ndogo.

"Kwa hiyo wale wakubwa wanakopeshana wenyewe kwa wakubwa na wale wadogo wanakwenda kwa wadogo zao. Sasa hii taasisi inakuja kuwa katikati kama mlivyosikia itatoa gurantee, maana yake ninaweza kusema bila kutaja benki fulani mfano benki A inataka mkopo kutoka benki C, basi basi wenyewe wataingia katikati watatoa hiyo dhamana.

"Kama huyu mtu asingekuwepo kwa mfano benki hii ingeweza kupata tu shilingi 10,000. Sasa kwa uwepo wao inaweza kupata hata shilingi 15,000. Kwa hiyo unaona ni taasisi ambayo imekuja kusaidiana na sisi.

"Taasisi hii haipo tu hapa kwetu, tayari ipo kwenye nchi nyingi kama walivyosema wapo kwa wenzetu Uganda, Rwanda, Zambia Kenya,Ghana kwa hiyo tumefikiria na sisi itakuwa ni fursa nzuri ya kuanza nao.

"Mbali na kutoa hiyo dhamana pia wanatoa mafunzo kwa washiriki kwenye masuala haya ya mambo ya masoko ya fedha, kwa hiyo tutakuwa tunapata mafunzo mbalimbali kwa maana ya watu wetu wa Tanzania kwa ujumla, sekta ya fedha.

"Nikisema sekta ya fedha sio mabenki peke yake, hii ninamaanisha wenzetu wa pensheni,bima na wengine ambao wako kwenye sekta. Lakini sekta kubwa kwa maana ya mabenki watafaidika zaidi kwa sababu tumekuwa tukiona kwamba mabenki yale makubwa yamekuwa yanawasahau wale wadogo, wanasema huyu mtu hawezi kunirudishia fedha yangu au wanawalipisha kwa riba kubwa kidogo, kwa hiyo hawa wanakuja kuweka dhamana hiyo,"amefafanua Naibu Gavana huyo.

Wadau

Aidha, kwa nyakati tofauti wawakilishi kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) wametumia nafasi hiyo kupongeza hatua iliyofikiwa na BoT, Frontclear na ECA kwa kusaini makubaliano hayo ambayo yanalenga kuziongezea ufanisi benki ili kuimarisha masoko ya fedha nchini.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) ambaye pia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa CitiBank Tanzania,Geofrey Daniel Mchangila amesema, huo ni mkataba muhimu katika seka ya fedha nchini.

"Nadhani kwa mkataba huu ambao Benki Kuu imesaini na taasisi hii ni hatua kubwa ya kimapinduzi katika sekta hii ya fedha, kwa maana ukiangalia katika sekta nzima ya soko la fedha la kimabenki linahusisha takribani mabenki 45.

"Haya mabenki 45 kuna mabenki ambayo ni ya saizi ya kati na saizi ya juu na katika saizi hizo huwa kuna suala zima la appetite (shauku) ambayo mabenki yanayo katika kukopeshana.
"Kwa muda mzuri, na katika hilo unakuta kuna suala zina la appetite ambayo mabenki yanayo kwa muda mfupi na katika hilo unakuta kwamba hakuna mojawapo ya group ambalo labda lisihisi sawasawa ama lisiwe na ziwe limit za kuweza kukopesha benki nyingine.

"Huu mkataba sasa umekuja kwanza kwa ajili ya kuongeza ufahamu katika soko zima la fedha ikiwemo upande wa Benki Kuu ambao ni regulators (wasimamizi) sisi wa soko hili la kifedha, lakini pia sisi upande wa mabenki.

"Umuhimu wetu wa pili linakuja kuyaleta mabenki haya ya aina tatu saizi ya kati, ya chini na saizi ya juu kwa pamoja kwa kuwapa gurantee kwamba zile benki za juu huko nyuma labda zilikuwa zinasita kidogo kuwapatia kiasi kikubwa cha fedha kwa muda mfupi hizi benki za chini basi zitapewa gurantee ambazo zitaweza sasa kuwapatia pesa.

"Na wale wataweza kufunga ile gape iliyoko kwenye urali wao wa fedha na kuongeza mikopo yao katika uchumi wa nchi. Kwa hiyo kimsingi itasaidia sio tu kuziwezesha zile benki za chini na za kati kupata mikopo kutoka kwenye sekta ya soko la fedha bali vile vile hizo benki kupata hizo fedha kuweza kuzitumia kuweza kukopesha kwa wateja mbalimbali katika uchumi wetu, hivyo kuweza kusaidia katika juhudi nzima, mikopo inatolewa katika sekta mbalimbali na kuweza kufikia wananchi katika sekta mbalimbali nchini,"amesema Makamu Mwenyekiti huyo.

CEO Buyskes

Wakati huo huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Frontclear, Philip Buyskes amesema kuwa, watahakikisha wanasimama katika nafasi yao ili kuhakikisha masoko ya fedha nchini yanakuwa imara ili yaweze kuwahudumia Watanzania katika maeneo yote nchini kwa ustawi bora wa uchumi.
Amesema, masoko mengi ya fedha yanayoibukia kama ilivyo kwa Tanzania, yanakabiliwa na changamoto ya kimuundo, mgawanyiko mkubwa wa soko na kutegemea zaidi sekta ya benki kama chanzo pekee cha ukwasi wa ndani, hivyo vinapotokea vikwazo vinachangia kudhoofisha ukuaji.

"Kwa hali ya kawaida ya soko hili linapaswa kuwa himilivu na imara, hivyo likishindwa kuhudumia kwa pande mbili kutokuwa na uhusiano mwema kwa hofu ya kushindwa kurejesha mikopo, utachangia mgawanyo duni wa ukwasi na hatari.

"Pia huathiri uthabiti wa jumla wa mfumo wa kifedha na jukumu la kupanua vyema mikopo na bidhaa za kifedha kwa uchumi halisi, hivyo tutahakikisha tunasimama katikati imara,"amesema Afisa Mtendaji Mkuu huyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news