Rais Samia aipongeza Serengeti Girls kwa kuibamiza Les Bleues

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameipongeza timu ya Serengeti Girls kwa kuibamiza Les Bleues ya Ufaransa mabao 2-1 katika michuano ya Kombe la Dunia kwa Wasichana chini ya Umri wa Miaka 17 (U17).

"Hongereni vijana wangu Serengeti Girls kwa ushindi wa 2-1 mlioupata leo dhidi ya Ufaransa. Nawaomba Watanzania tuendelee kuwaombea na kuwatia hamasa vijana wetu ili waendelee kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika Kombe la Dunia kwa Wanawake chini ya miaka 17 huko India,"ameeleza Rais Samia.

Watanzania walishangazwa na mechi ya kuvutia iliyowashirikisha mabinti hao ambapo huo ni ushindi wa kwanza wa Tanzania katika michuano hiyo ya Dunia.

Mtanage huo dhidi ya Wafaransa ulipigwa Oktoba 15, 2022 katika Uwanja wa Fatorda (Uwanja wa Pandit Jawaharlal Nehru) uliopo Margao, Goa, India.

Mabao ya Serengeti Girls yalifungwa na Diana Mnally dakika ya 16 na Christer Bahera dakika ya 56 kwa penalti, wakati la Ufaransa lilifungwa na Lucie Calba dakika ya 75.

Kwa ushindi huo, Serengeti Girls watateremka tena uwanjani Jumanne ijayo kukamilisha mechi zao za Kundi D kwa kumenyana na Canada.

Post a Comment

0 Comments