Rais Samia azindua kituo cha kusafirisha umeme Kigoma na Kagera

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amezindua njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolt 220 kutoka Nyakanazi-Geita yenye urefu wa kilomita 144.

Kituo hicho cha umeme cha Nyakanazi kilichopo wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera pia kinasafirisha umeme kupeleka Kigoma hivyo kuiwezesha Kigoma kupata umeme wa gridi kwa mara ya kwanza.

Rais Samia amezindua miradi sita katika kituo hicho yenye thamani ya shilingi bilioni 600 ambayo itasaidia kusambaza umeme katika maeneo ya Ngara, Biharamulo na Kigoma. Awali umeme katika maeneo hayo ulizalishwa kwa njia ya majenereta.

Kuzimwa kwa majenereta hayo kumesaidia kuokoa shilingi bilioni 60 kwa mwaka ambazo zilikuwa zikitumika katika mafuta na matengenezo ya majenereta hayo.

Aidha, umeme unaozalishwa katika kituo hicho utatumika pia katika viwanda pamoja na migodi ya mikoa jirani na hivyo kuchangia kukua kwa uchumi wa nchi.

Rais Samia amehitimisha ziara yake ya kikazi leo Mkoani Geita na kuanza ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Kigoma ambapo amefungua Hospitali ya Wilaya ya Kakonko na kuzindua mradi wa maji wa Kanyamfisi, Kibondo mjini.

Rais Samia pia amezindua barabara ya Kabingo – Nyakanazi (km 50) pamoja na kuweka Jiwe la Msingi ujenzi wa barabara ya Kibondo mjini – Nduta eneo la Twabagondozi yenye urefu wa kilomita 25.9.

Post a Comment

0 Comments