RC Sendiga atoa onyo kwa wafanyabiashara

NA DIRAMAKINI

MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Queen Sendiga amepiga marufuku tabia ya baadhi ya wafanyabishara kupandisha bei ya bidhaa za ujenzi pindi wanaposikia Serikali imetoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwani kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria.

Agizo hilo alilitoa hivi karibuni wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuwa serikali ya mkoa huo imepokea fedha zaidi ya sh. Bilioni 3.8 zitakazotumika kujenga vyumba vya madarasa 191 ili kuondoa upungufu wa madarasa uliopo mkoani humo.

Amesema kuwa, kumekuwepo madai kuwa wapo baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa na tabia ya kupandisha bei za vifaa vya ujenzi pindi wanaposikia Serikali imetoa fedha za kutekeleza miradi mikubwa wakiamini kuwa huo ndio wakati wao wa kujipatia faida kubwa.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa, kwa mfanyabishara atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria kwani huyo atakuwa ni muhujumu uchumi na hawezi kuachwa aendelee kukwamisha jitihada za serikali pia kuwaumiza wananchi kwa kuwauzia bidhaa kwa bei kubwa tofauti na uhalisia.

Alisema kuwa, serikali imetoa fedha hizo na kupanga kuwa kila darasa moja litajengwa kwa thamani ya shilingi milioni 20 na ni lazima fedha hizo zitoshe, lakini kama wafanyabiashara watapandisha bei ya vifaa vya ujenzi kiholela huenda fedha hizo zisitoshe hali ambayo serikali ya mkoa haitakubali hilo litokee.

Pia Sendiga aliwataka wawekezaji mbalimbali katika sekta ya utalii wajitokeze kwa wingi kuja kuwekeza mkoani Rukwa kwani mkoa huo una fursa nyingi za utalii kuna vivutio mbalimbali na vya kipekee vilivyotangazwa na vingine bado havijatangazwa na havijulikani.

Alisema kuwa, kuna fursa nyingi kwa wawekezaji hao ikiwemo kuwekeza katika hoteli za kitalii, kuwafundisha vijana namna bora ya kuhudumia watalii pamoja na biashara ya usafirishaji kwa watalii kwani hivi sasa watalii wengi wanamiminika nchini kutokana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuvitangaza vivutio vilivyopo nchini kupitia filamu ya The Royal Tour.

Mmoja wa wananchi wanaoishi katika Halmashauri ya Sumbawanga mkoani Rukwa, Fransis Sebastian aliyezungumza na DIRAMAKINI alimshukuru Rais Samia na Serikali yake yote kwa kuamua kutoa fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 191 vya madarasa.

Pia amesema kuwa, Serikali imempunguzia mzigo mwananchi kwani ilipaswa michango ya kuchangia ujenzi wa shule ianze, lakini hivi sasa wananchi wao wanajikita na maandalizi ya sare pamoja na vifaa vingine vya kwenda navyo shule mwanafunzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news