Serikali yakiri mchango wa Sekta ya Madini kuimarika nchini

*Mchango wa wachimbaji wadogo umekua kutoka asilimia 4 hadi 40

NA MWANDISHI WETU

IMEELEZWA kuwa,mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeendelea kuimarika kutokana na kuongezeka kwa usimamizi wa shughuli mbalimbali za madini ambapo mwaka 2021 ulifikia asilimia 7.2 na ukuaji wake ulifikia asilimia 9.6.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji katika kilele cha Maonesho ya 5 ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini katika viwanja vya Bombambili mkoani Geita.

Pia, Dkt. Kijaji amesema Sekta ya Madini ni muhimu kwenye mchango wa uchumi wa Taifa ambapo ameitaka Wizara ya Madini kuendelea kuisimamia sekta hiyo kwa lengo la kuongeza mchango wake kwenye Pato la Taifa.
Aidha, Dkt Kijaji amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa nia yake ya dhati ya kuleta mabadiliko chanya kwenye Sekta ya Madini kupitia maelekezo yake anayoyatoa kila mara.

Dkt. Kijaji ametoa wito kwa Wizara ya Madini kuendelea kushirikiana na Wadau mbalimbali ili kupata teknolojia ya uongezaji thamani madini kwa lengo la kuachana na usafirishaji wa madini ghafi.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Kijaji amesema Kauli Mbiu ya mwaka huu isemayo "Madini ni Fursa za Uchumi, Ajira na Maendeleo Endelevu" inachochea uwekezaji katika Sekta ya Madini na pia inahamasisha ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na watanzania kwa ujumla.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amempongeza Rais Samia kwa kuitangaza vyema Sekta ya Madini dunia kote na kupelekea wawekezaji kuwekeza kwenye sekta mbalimbali nchini ikiwemo Sekta ya Madini.

Vile vile, Biteko amesema Sekta ya Madini ni nguzo muhimu na ni chachu ya maendeleo kwa kuzingatia kuwa sekta hiyo inafungamanisha moja kwa moja sekta nyingine za kiuchumi zikiwemo Sekta za Ujenzi, Viwanda, Kilimo, Usafirishaji na Mawasiliano.
"Maonesho haya, yana dhana ya kukuza teknolojia ya madini ambayo yanaenda sambamba na kufungamanisha na sekta zingine za kiuchumi," amesema Dkt. Biteko.

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Biteko amesema Serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kuweka mazingira bora na kusimamia mikakati iliyojiwekea ili kuwawezesha wachimbaji wadogo waweze kuchimba kwa faida.
"Kufuatia Serikali kuendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo, mchango wao katika maduhuli ya Serikali umeongezeka kutoka asilimia 4 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 40," amesema Dkt Biteko.

Pia, Biteko amesema maonesho ya mwaka huu yamekuwa tofauti na miaka mingine ambapo amesema mwaka huu kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wananchi na wadau wengi wa madini kujitokeza kushiriki maonesho hayo.
"Napenda pia kuwashukuru wananchi na wadau wengine wakiwemo wawakilishi wa nchi mbalimbali walioshiriki maonesho haya," ameongeza Dkt. Biteko.
Maonesho ya Teknolojia ya Madini hufanyika kila mwaka mkoani Geita katika viwanja vya Bombambili kwa lengo la kutangaza fursa zilizopo katika Sekta ya Madini na kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo wa madini namna bora ya kutumia teknolojia ya kisasa ili wafanye shughuli zao kwa tija.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news