Simba SC yawatangulia Yanga SC mbele Kimataifa

NA DIRAMAKINI

KLABU ya Simba SC ya jijini Dar es Salaam nchini Tanzania imejiweka kwenye nafasi nzuri ya kuingia Hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ni baada ya ushindi wa 3-1 dhidi ya wenyeji, Primiero de Agosto leo Oktoba 9, 2022 katika dimba la Novemba 11 mjini Luanda nchini Angola.

Simba SC wamesonga mbele kwa mabao ya kiungo Mzambia, Clatous Chama dakika ya nane, beki Mzawa, Israel Mwenda dakika ya 63 na mshambuliaji Mzambia, Moses Phiri dakika ya 76.

Aidha, kwa upande wao Primiero de Agosto kutoka jijini Luanda nchini Angola wamepata bao la kufutia machozi kupitia Dago katika dakika ya 78 ya mchezo huo.

Klabu hizo kwa pamoja zinatarajia kurudiana Jumapili ijayo, Oktoba 16, mwaka huu na mshindi wa jumla atakwenda hatua ya makundi, wakati timu itakayofungwa itakwenda kuwania kucheza makundi ya Kombe la Shirikisho.

Awali, wenyeji Klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam walilazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Al Hilal Omdurman ya Sudan.

Ni katika mchezo wa kwanza wa Hatua ya 32 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa Oktoba 8, 2022 katika dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Wenyeji Yanga SC walitangulia kwa bao la mshambuliaji wake, Fiston Kalala Mayele dakika ya 50, kabla ya El Hilal kusawazisha kupitia kwa Mohamed Yousif dakika ya 67.

Klabu hizo zitarudiana Oktoba 16,Jumapili ya wiki ijayo katika dimba la Al-Hilal Stadium jijini Omdurman nchini Sudan na mshindi wa jumla atakwenda Hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Aidha, timu itakayotolewa itakwenda kumenyana na timu ya Kombe la Shirikisho kuwania kucheza Hatua ya makundi ya michuano hiyo midogo ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Post a Comment

0 Comments