Slow Food yahimiza matumizi ya vyakula vya asili, visivyo na sumu

NA DORINE ALOYCE

RAIS mpya wa Shirika la Kimataifa lisilo la Kiserikali la Slow Food, Bw. Edward Mukiibi kutoka nchini Uganda ameeleza kuwa,kila mmoja wetu anao wajibu wa kuzalisha vyakula vya asili na salama kwa ajili ya matumizi ya kila siku ndani ya familia na maisha kwa ujumla.
Mukiibi ameyasema hayo hivi karibuni baada ya kuhitimisha mkutano wa Terra Madre huko Parco Dora, Turin nchini Italia ambao ulifanyika kwa wiki moja huku ukiwakutanisha wawakilishi kutoka matiafa zaidi ya 160 duniani kote.

Amesema, shirika lake linahamasisha vyakula bora, safi na matumizi ya mfumo wa ikolojia ya kilimo, hatua inayolenga kutatua tatizo la usalama wa chakula linalodaiwa kusababishwa na mabadiliko ya tabia nchi duniani.

"Kama unavyojua, Afrika haiwezi kutegemea mzunguko wa chakula duniani, hivyo matumizi ya mfumo wa ikolojia ya kilimo ni muhimu kwa usalama endelevu wa chakula,"amefafanua.
Amefafanua zaidi kuwa, Slow Food pia inashirikiana na wakulima wadogo ili kuzuia kutoweka kwa tamaduni na mila za vyakula vya kienyeji, kukabiliana na ongezeko la maisha ya haraka na kupambana na kupungua kwa hamu ya watu katika chakula wanachokula, kinatoka wapi na jinsi chakula chetu kinavyoandaliwa.

“Slow Food huu ni mtandao wa kimataifa, ulioanzishwa mwaka 1989, na tangu kuanza kwake, mtandao huo umekua na kuwa vuguvugu la kimataifa linalohusisha mamilioni ya watu katika nchi zaidi ya 160, linalofanya kazi kuhakikisha kila mtu anapata chakula bora, safi na cha haki,” ameeleza.

Pia amebainisha kwamba,Slow Food inaamini kwamba chakula kinafungamana na nyanja nyingine nyingi za maisha, ikiwa ni pamoja na utamaduni, siasa, kilimo na mazingira.

"Kupitia uchaguzi wetu wa chakula tunaweza kushawishi kwa pamoja jinsi chakula kinavyolimwa, kuzalishwa na kusambazwa, na kubadilisha dunia kwa matokeo bora," Mukiibi ameelezea.

Mukiibi ameeleza zaidi kuwa, matumizi sahihi ya ardhi katika uzalishaji wa chakula bora na safi ni muhimu kwa usalama endelevu wa chakula kutokana na mabadiliko ya tabianchi duniani, na Slow Food inashirikiana na wakulima wadogo kukabiliana na tatizo hilo kama mtandao wa kutatua tatizo hilo.

Kwa upande wake, Valentina Meraviglia kutoka Shirika la Kimataifa la Slow Food (Global South Network) ameeleza kuwa, mkutano wa Terra Madre ulionesha kwa mara nyingine tena kwamba pamoja na washiriki kutoka nchi 160 duniani kote, zaidi ya changamoto ambazo wanapaswa kukabiliana nazo tofauti na mtu mmoja mmoja, mtandao na wote wako pamoja, kila akichangia kujenga mfumo endelevu wa chakula.

"Tukio hili liliimarisha uhusiano wetu wa mshikamano na kuaminiana, na kuimarisha azimio ambalo tunatekeleza lengo letu la pamoja la kupata kila mtu upatikanaji wa chakula bora, safi na cha haki," amefafanua na kuongeza kuwa,

"Kama vile Rais wetu Edward Mukiibi alivyosema: “Suluhu ya migogoro mingi tunayokabiliana nayo tayari ipo. Tumeziona, kuzisikia na kuzibadilisha kwa siku chache zilizopita na mamia ya wakulima, wapishi, wazalishaji wa chakula, wanaharakati na wataalam waliokutana pamoja mjini Turini,"ameeleza.

Naye Mratibu wa shughuli za Slow Food Tanzania, Reguli Marandu akitoa maoni yake juu ya mkutanao wa Terra Madre alisema kuwa, kongamano hilo ni muhimu sana kwa jamii na vizazi vijavyo.

"Kama unavyoona wadau mbalimbali kuanzia wakulima wadogo kabisa kutoka Afrika,Amerika ya Kusini na kote ulimwenguni pamoja na mashirika muhimu katika sekta ya kilimo wakiwemo wadau wa Kimataifa kama FAO na IFAD.

"Wote tumekutana hapa kujadili masuala mbalimbali ya usalama wa chakula, kilimo na mazingira na kutafuta suluhu ya changamoto mbalimbali katika mifumo yetu ya chakula,"amesema Marandu.

Amesema, mifumo ya uzalishaji chakula iliyojikita kwenye viwanda imekua ikiendelea kuathiri ardhi na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika mabadiliko ya tabia ya nchi na zaidi kugandamiza wakulima wadogo.

Marandu ameongeza kuwa, kongamano hilo pia limetoa angalizo la upotevu wa vyakula vya asili ikiwa ni pamoja na wanyama wa asili huku akitolea mfano Tanzania kuna makabila zaidi ya 120 na kila kabila lina vyakula vyake vya asili, lakini leo vyakula vinavyoliwa kwa wingi havizidi vyakula vitano.

"Tunapopoteza vyakula hivi sio chakula tu kinapotea bali tunapoteza sehemu ya tamaduni zetu za asili, uhaba wa chakula ni changamoto kubwa sana Afrika na athari ya mabadiliko ya tabia ya nchi kama ukame na mafuriko yanaongeza makali ya njaa,"amesema.

Amesema kuwa, ni muda sasa wadau wa kilimo na chakula kuanza kufikiria kuwekeza kwenye mifumo ya asili ya uzalishaji chakula, mifumo inayotumiwa na wakulima wadogo katika mashamba yao madogo ya familia,
"Mifumo hii ya wakulima wadogo tayari inatumia dhana za kilimo ikologia,kuna ujuzi fulani tayari wakulima hawa wadogo wamejifunza kwa uzoefu hivyo ni wakati wa kujifunza toka kwao na kwa pamoja kuleta ustawi katika sekta ya kilimo na chakula,"amesema Marandu.

Geofrey Ishengoma ni mkulima kijana kutoka Tanzanaia amesema, kongamano limeenda vyema sana na ilikuwa ni nafasi adimu ya kukutana na wadau toka maeneo mbalimbali duniani na kubadilishana uzoefu kuhusiana na mafanikio na changamoto za falsafa nzima ya Slow Food.

"Ni matarajio yangu Mtandano wa Slow Food Tanzania utanufaika sana na uwepo wangu katika Terra Madre hasa mtandao wa vijana wa Slow Food Tanzania,"amesema Ishengoma.

Katika kongamano hilo lijulikanalo kama Terra Madre ambalo limefanyika hivi karibuni Parco Dora mjini Turini nchini Italia lilienda sambamba na uchaguzi wa kiongozi mpya kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa mtandao huo baada ya mtangulizi wao kumaliza muda wake kutokana na umri.

Slow Food ni nani?

Slow Food International ni mtandao mkubwa uliopo kwenye nchi zaidi ya 160 duniani ambao unaojihusisha na wakulima wadogo katika kuhamasisha ulaji wa vyakula vya asili na salama.

Mtandao huu wa Slow Food ulianzishwa mwaka 1989 na mwanaharakati wa Kiitalino anayejulikana kwa jina la Carlo Petrin ambaye alilenga kukabiliana na changamoto zilizokuwa zimeletwa na ulaji wa vyakula vya haraka (fast food), .

Vyakula ambavyo vilitengenezwa viwandani na maisha ya haraka kwa ujumla ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa yamezalisha changamoto nyingi za kiafya kwa watu pamoja na kusabisha kusahaulika kwa vyakula vya asili.

Slow food ililenga kuhakikisha watu wanapata kula chakula chenye ladha nzuri inayoendana na utamaduni wao, kinachozalishwa kwa namna isiyoharibu mazingira na afya ya binadamu, lakini kinachomnufaisha pia mkulima ambaye ndiye mzalishaji.

Aidha, mtandao huo una wanachama zaidi ya laki moja kutoka mataifa zaidi ya 160 duniani wanaofanya kazi pamoja lengo likiwa ni kulinda na kuifadhi utamaduni na falsafa nzima ya Slow Food.

Kila baada ya miaka miwili wanachana na wanaharakati wa mtandao wa Slow Food kote duniani ukutana nchini Italia kubadilishana uzoefu na ujuzi juu ya uzalishaji, miradi na kufanya tathimini ya jinsi ambavyo shughuli za kilimo hai zimekuwa zikiendelea katika maeneo mbalimbali duniani kupitia kongamano maarufu kama Terra Madre.

Kupitia kongamano hilo watu mbalimbali hususani wakulima ambao hutoka mataifa tofauti uambatana na bidhaaa zao wanazolima kwa ajili ya maonesho na kujifunza aina ya vyakula ambapo pia watu huwa wanapata fursa ya kula vyakula tofauti kutoka mabara tofauti.
Aidha, katika kuendeleza mapambamo hayo ya ulaji wa vyakula asili, Slow Food International inaendelea kutoa wito kwa wanajumuiya barani Afrika na duniani kwa ujumla kutumia mfumo wa ‘Agro-Ecology’ ambao ni uwezekano wa Mabadiliko ya Tabianchi Duniani na uwezo wa kulisha Afrika ili kuboresha usalama wa chakula barani humo.

Mtandao huo pia unatoa wito kwa wanajamii kuzalisha na kutumia vyakula visivyo na sumu katika miili yao na vyakula vinavyoheshimu utamaduni kwa afya bora endelevu ambao kwa kiasi kikubwa huwa vinasaidia kuepuka magonjwa yanayosababishwa na ulaji mbaya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news