Tanzania,Zambia zasaini Mkataba wa Kubadilishana Wafungwa na Mkataba wa Utatu kati ya Chemba za Biashara

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Zambia zimesaini Mkataba wa Kubadilishana Wafungwa na Mkataba wa Utatu kati ya Chemba za Biashara za nchi hizo wakati wa Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia katika Ngazi ya Mawaziri uliomalizika leo Oktoba 15,2022 jijini Lusaka,Zambia.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Stanley Kabubo wa Zambia wakisaini Mkataba wa Kubadilishana Wafungwa kati ya nchi zao leo tarehe 15 Oktoba 2022 jijini Lusaka, Zambia wakati wa hafla ya kufunga Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia.

Mkataba wa Kubadilishana Wafungwa ulisainiwa kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Mhe. Stanley Kabubo.

Wakati huo huo, Mkataba wa Utatu kati ya Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) na Chemba ya Taifa ya Biashara ya Zanzibar (ZNCC) za Tanzania na Chemba ya Wafanyabiashara na Viwanda (ZACCI) ya Zambia ulisainiwa na Rais wa TCCIA, Bw. Paul Koyi na Mtendaji Mkuu wa TCCIA na Bw. Nerbat Mwapwele kwa niaba ya Mwenyekiti wa ZNCC. Pia kwa upande wa Zambia mkataba huo ulisainiwa na Mtendaji Mkuu wa ZACCI, Bw. Phil Daka.
Aidha, Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia katika Ngazi ya Mawaziri, ulitanguliwa na mkutano katika ngazi ya wataalam uliofanyika tarehe 11 na 12 Oktoba 2022 na kufuatiwa na Mkutano katika ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 13 Oktoba 2022.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Stanley Kabubo wa Zambia wakishuhudia Rais wa Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), Bw. Paul Koyi na Mtendaji Mkuu wa Chemba ya Wafanyabiashara na Viwanda ya Zambia, Bw. Phil Daka wakisaini mkataba wa ushirikiano kati ya chemba hizo.

Pamoja na mambo mengine mkutano huo pia ulitathimini utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa wakati wa ziara ya Kiserikali ya Rais wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema aliyofanya nchini Tanzania mapema mwezi Agosti 2022.

Post a Comment

0 Comments