Tembo Worriors mguu sawa kuikung'uta Hispania leo

NA MWANDISHI WETU

SAA chache kabla ya ufunguzi rasmi wa Mashindano ya Kombe la Dunia la mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu, Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe.Jenerali Yacoub Mohamed ameitaka timu ya Tanzania Tembo Warriors inayoshiriki fainali Kombe la Dunia kuanza vizuri mashindano hayo kwa kuifunga Hispania kwenye mchezo wake wa kwanza.
Mhe. Balozi ambaye ameambatana na Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi na mlezi wa timu hiyo, Mhe. Riziki Lulida (MB) wamefanya kikao na timu hiyo na kuwatia moyo na hamasa wachezaji.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Balozi ameitaka Tembo Warriors kuanza mashindano hayo kwa nguvu na kuichabanga Hispania ili kusafisha njia ya kuendelea na kurudi na kombe nchini.

Aidha, ameishukuru na kupongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa inayoufanya kwenye michezo ikiwa ni pamoja na kuzigharimia timu zote za taifa kwa kuziweka kambini kipindi chote cha mashindano kwa gharama za Serikali.

“Serikali imewathamini sana, kaonesheni uwezo uwanjani, hakikisheni mnatoka na kombe na hilo liwe ndio lengo lenu kubwa,”amesisitiza Mhe. Balozi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Dkt. Abbasi amewaomba watanzania wanaoishi nchini Uturuki kujitokeza kwa wingi siku ya leo Oktoba 1, 2022 kuishangilia Timu ya Tanzania ikicheza dhidi ya Hispania, mechi itakayochezwa saa saba kamili mchana.

Mhe. Riziki Lulida yeye ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuiunga mkono timu ya Tembo Warriors toka imeanza mpaka hatua ya kufuzu kombe la Dunia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news