Serikali yapongeza mchango wa taasisi za dini katika kuleta maendeleo nchini

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imesema inatambua mchango wa Jumuiya ya Waislam Waahmadiyya katika maendeleo ya Sekta ya Elimu kupitia taasisi zake za elimu, Sekta ya Afya kupitia hospitali.

Sambamba na namna wanavyojitolea kuchangia damu salama katika benki ya damu pamoja na sekta ya maji kupitia mpango wao wa kuchimba visima vya maji maeneo mbalimbali nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe.George Simbachawene akisalimiana na viongozi mbalimbali wa Jumuiya ya Waislam Waahmadiyya.

Hayo yamesemwa Septemba 30,2022 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene wakati wa uzinduzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa 51 wa Jumuiya ya Waislam Waahmadiyya Tanzania jijini Dar es Salaam, kwa niaba ya Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyekuwa mgeni rasmi.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu anawapongeza Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry-Amir na Mubashir Mkuu, pamoja na Wasaidizi wako wa Jumuiya ya Waislam Waahmadiyya kwa uongozi mahiri unaolenga kudumisha amani na utulivu hapa nchini, kupitia kauli mbiu yenu ya Upendo kwa wote bila chuki kwa yeyote.

"Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa ustawi wa taasisi hizi ili ziendelee kuwa sehemu ya kuliletea maendeleo Taifa letu.
"Wote mnatambua kuwa nchi yetu kupitia ibara ya 3(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, 1977 haiegemei upande wowote katika masuala ya dini - Secular State. Hata hivyo, sehemu kubwa ya watu wake wanaamini katika Mungu kupitia dini zenye madhehebu mbalimbali.

“Kwa msingi huu, nchi yetu kupitia ibara ya 19 ya Katiba, inatambua uhuru wa kuabudu kwa mtu mmoja mmoja au kundi la watu katika madhehebu na dini zao ili mradi tu wafuate masharti ya Katiba na Sheria za Nchi.

"Aidha, nichukue fursa hii adhimu kuwasihi katika siku zote tatu mtakazo kuwa hapa, muendelee kuliombea taifa letu amani, utulivu, upendo na mshikamano ili kwa pamoja tuendelee kulijenga taifa bora licha ya changamoto mbalimbali tunazokumbana nazo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe George Simbachawene akitembelea moja ya banda la vitabu la Jumuiya ya Waislam Waahmadiyya.
 
"Kwa namna ya pekee nawaomba muiombee nchi yetu dhidi ya majanga mbalimbali likiwemo janga la njaa linaloweza kusababishwa na ukame, ukosefu wa mvua za kutosha au mafuriko, changamoto za kiuchumi zinazosababishwa ama na sisi wenyewe au mataifa mengine, magonjwa, dhiki na mmomonyoko wa maadili,"amesema Waziri Simbachawene.

Naye Naibu Amir Shekhe Abdurahman Mohamed amesema, Jumuiya ya Waislam Waahmadiyya inashika mafundisho ya Kiislamu kwa usahihi wake.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Sera Bunge na Uratibu, Mhe George Simbachawene akipokea zawadi ya vitabu kutoka kwa Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry-Amir na Mubashir Mkuu.
 
"Shida inakuwepo pale waumini wanapofundishwa dini na wakaiacha, na kuiwakilisha dini kwa sura ambayo sio yenyewe, hili ni jambo ambalo Jumuiya ya Waislam Waahmadiyya inaliepuka.

“Maisha ya binadamu ni roho na mwili, lazima apate mafunzo ya kupata maendeleo ya kimwili na wakati huo huo apate maendeleo ya kiroho, chochote ukikiacha kingine kinapoteza maana yake,” amesema Shekhe Abdurahman.

Post a Comment

0 Comments