Ukame waathiri mabwawa manne ya kuzalisha umeme kutoka Megawati 266 hadi 34, TANESCO yachukua hatua za haraka

NA GODFREY NNKO

SHIRIKA la Umeme nchini (TANESCO) limesema kuwa, kutokana na ukame mkubwa unaoikumba nchi, mabwawa ya kuzalisha umeme ya Hale, Kihansi, Nyumba ya Mungu na Pangani yenye uwezo wa kuzalisha megawati 266 za umeme yamepungua uwezo wake na kwa sasa yanazalisha megawati 34 za umeme tu.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Oktoba 30, 2022 na Kurugenzi ya Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO) makamo makuu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hali hiyo imeathiri upatikanaji wa umeme wa kutosha katika sehemu mbalimbali za nchi hususani mikoa ya Arusha,Kilimanjaro na Tanga.

"Kutokana na ukame huu mkubwa, mikoa italazimika kupata umeme wake kutoka katika vituo vya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia vilivyopo Dar es Salaam.

"Aidha, kutokana na kuongezeka kwa kasi kwa shughuli za uchumi katika mikoa hiyo,njia za kusafirisha umeme kutoka Dar es Salaam kwenda kwenye mikoa hiyo zimezidiwa na hivyo kusababisha umeme unaopatikana katika mikoa hiyo kutokidhi mahitaji,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Pia kwa mujibu wa taarifa hiyo, ili kukabiliana na changamoto hiyo, shirika hilo limechukua hatua mbalimbali ikiwemo kujenga njia mpya kutoka kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Luguruni ili kuhudumia maeneo yote kati ya Luguruni mpaka Chalinze.

"Hivyo, kutoa nafasi ya umeme mwingi zaidi kufika katika mikoa Arusha, Kilimanjaro na Tanga. Hii itasaidia kupunguza mzigo wa umeme katika njia ya sasa inayotoka Ubungo hadi Chalinze na hivyo kuruhusu umeme mwingi kwenda katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa hiyo, TANESCO imechukua hatua ya kujenga njia mpya kutoka kituo cha kupoza na kusambaza umeme kilichopo Kisongo jijini Arusha.

Hatua hiyo inatarajiwa kupunguza mzigo wa umeme unaopitia kwenye Kituo cha Njiro, hivyo kuongeza kiasi kingine cha umeme kufika katika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga kupitia Arusha.

"Na kutatua tatizo la sasa la Arusha ambapo Kituo cha Njiro kinapitisha umeme wa Kilimanjaro na Tanga na hivyo kuzidiwa na kusababisha umeme kutokidhi mahitaji katika Mkoa wa Arusha,"imeeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hali ya ukame mkubwa ilitabiriwa kutokea mwaka huu na shirika hilo limechukua hatua za kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia vituo vyake vya gesi.

"Kazi katika upanuzi wa Kituo cha Kinyerezi 1 imefikia ukingoni na inategemewa kukamilika kabla ya mwisho wa mwezi huu ili kuingiza megawati nyingine 185 katika Gridi ya Taifa. Megawati 90 kati ya hizo zipo kwenye majaribio hivi sasa. Hatua hii itaimarisha uwezo wa kukabiliana na upungufu wa maji ambao unategemewa kuendelea,"imeongeza taarifa hiyo.

Wakati huo huo, TANESCO imefafanua kuwa, pamoja na kazi zote hizo kuendelea kufanyika, ofisi zao za mikoa zitaendelea kutoa ratiba ya upungufu wa umeme kwenye maeneo yote yanayoathirika.

"Na wateja wetu watapewa taarifa kwa njia mbalimbali zikiwemo pamoja na ujumbe mfupi na maeneo kwenda kwa mhusika wa eneo hilo litakaloathirika, shirika linashukuru kwa ushirikiano linaoupata kwa wateja wake katika kutafuta majawabu,"Kurugenzi ya Mawasiliano kwa Umma, TANESCO imefafanua.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news