Wahitimu Kidato cha Nne Shule ya Sekondari Iringo wafundwa

NA FRESHA KINASA

WAHITIMU wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Iringo iliyopo Manispaa ya Musoma mkoani Mara wameshauriwa kuwa mabalozi wema wa kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya rushwa.
Kauli hiyo imetolewa Oktoba 22, 2022 na Meneja wa Radio Victoria FM iliyopo Manispaa ya Musoma mkoani Mara, Shomari Binda wakati akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Kitengo cha Elimu kutoka Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Mara katika mahafali ya kuwaaga wanachama wa TAKUKURU katika mahafali yaliyofanyika katika eneo la Le Grand Beach Manispaa ya Musoma.

Binda amesema, kwa muda wa miaka minne ambayo wamekuwa wanachama wa TAKUKURU wameweza kupata elimu kwa kina kuhusu madhara ya rushwa hivyo elimu hiyo waitumie vyema katika maisha yao sambamba na kuihimiza Jamii kushiriki mapambano ya vitendo vya rushwa ili kujenga uadilifu.
Aidha, amewatahadharisha juu ya rushwa ya ngono ambayo imekuwa ikijitokeza katika maeneo ya kazi na vyuo vya elimu ya juu, wawe sehemu ya kudhibiti rushwa hiyo hasa watakapoendelea na masomo yao ya juu wakasimame kidete kwa kushirikiana na serikali kuhakikisha rushwa haipati mizizi itakayoleta athari kwa taifa.

"Mtafanya mitihani ya kuhitimu kidato cha nne, mtangulizeni Mwenyezi Mungu katika mitihani hiyo kusudi msonge mbele na masomo ya kidato cha tano na sita. Mmepata elimu ya kina juu ya rushwa kaweni mabalozi wa kuelimisha jamii kwamba rushwa inasababisha ubovu wa huduma, maendeleo kufanyika chini ya kiwango na kupata wataalam wasio na uwezo. Mwalimu Nyerere alikemea rushwa na Rais wetu Mheshimiwa Samia amekuwa akikemea rushwa lazima rushwa ipingwe na njia bora ni kutoa elimu kuanzia chini,"amesema.

Akitoa taarifa ya klabu hiyo Mwalimu Makuru amesema kwamba, klabu hiyo imeweza kupata elimu thabiti ya madhara ya rushwa kutoka kwa Maafisa wa TAKUKURU Mkoa jambo ambalo amesema kwa sehemu kubwa wamefanya jukumu hilo kwa ufanisi.
Katika kukabiliana na rushwa, Mwalimu Makuru ameomba wanafunzi waandaliwe kukabiliana na rushwa kuanzia shuleni ili kuandaa taifa la watu waadilifu wasiopenda rushwa jambo ambalo litaisaidia nchi kupata Viongozi bora na wataalam wenye ubora katika nyanja mbalimbali.

Amesema, Mheshimiwa Rais Samia Samia ametoa fedha nyingi za kujenga vyumba vya madarasa maeneo mbalimbali nchini, hivyo ametoa ombi na msisitizo kwa wasimamizi wa fedha hizo, kuzisimamia kikamlifu kusudi zilete tija iliyokusudiwa.

"Sote tuunge mkono mapambano ya rushwa, kila mwananchi awe mdau wa kuunga mkono mapambano hayo. Kwani rushwa ni adui wa haki. Mheshimiwa Rais Samia Hassan hivi karibuni alisikika akiwaomba TAKUKURU kudhibiti fedha kabla hazijaliwa sio kwamba mpaka uovu ufanyike ndipo wanaanzagaje uchunguzi hii ni hatua njema katika kulinda rasimimali za nchi ziwaneemeshe Wananchi wote,"amesema Mwalimu Makuru.
Martine Ojung'a akisoma risala ya Wahitimu wa kidato cha nne wa Klabu ya TAKUKURU Mkoa wa Mara amesema Taasisi hiyo imekuwa ikiwatunuku vyeti wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne ambao ni wanachama Jambo ambalo linawapa ari ya kuthaminika mchango wao.

Ameongeza kuwa wamekuwa wakipata malezi kutoka Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Mara na ushirikiano wote na kwamba wao Kama wanachama wamekuwa wakifanya kazi ya kutoa elimu ya madhara ya rushwa kwa wanafunzi wengine

Ameongeza kuwa, kutokana na hamasa kubwa kutoka Ofisi ya Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Mara imefanya klabu kupata ongezeko la wanachama wengi ambapo mwaka 2015- 2016 wanachama walikuwa 150, mwaka 2020-2022 idadi ya wanachama imefikia 178. Huku matarajio ni kuwa na wanachama wengi zaidi.
Ametaja changamoto ni pamoja na kuondolewa kwa siku ya Klabu ya TAKUKURU Shuleni jambo linalopelekea kutojifunza mambo mbalimbali yanayohusiana na Klabu kwa upana zaidi. Pia uhaba wa vipeperushi na majarida, ukosefu wa bango linalotambulisha kiunga cha kupinga rushwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news