Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wapewa maelekezo

NA MWANDISHI WETU

NAIBU Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt.Boniphace Luhende amewataka wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) kutumia mafunzo wanayopatiwa kujenga uelewa kuhusu umuhimu wa Baraza la wafanyakazi katika kuweka mahala pa kazi kuwa sehemu salama katika utendaji wa kazi na kuhakikisha kuwa wajumbe wa OWMS wanatekeleza majukumu waliyokasimiwa.
Katibu wa Baraza la wafanyakazi, Zuhura Kussaga (katikati) kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali akifuatilia kwa makini mafunzo kuhusu umuhimu wa Baraza la Wafanya kazi mahala pa kazi katika mkutano wa Baraza hilo uliofanyika jijini Dodoma. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Ofisi hiyo, James Kibamba.

Dkt. Luhende ameyasema hayo leo wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa wajumbe wapya wa Baraza la Wafanyakazi wa OWMS yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Takwimu jijini Dodoma ambapo amesema kuwa mada tatu zitawasilishwa kwa wajumbe hao ikiwemo Wajibu na Majukumu ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi; Kupitia Mkataba wa Baraza la Wafanyakazi; na Umuhimu wa Baraza la wafanyakazi mahala pa kazi.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende akizungumza na wajumbe wa Baraza la Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (hawapo pichani) wakati akifungua mafunzo ya kujenga uelewa kuhusu umuhimu wa Baraza kwa wajumbe wa Baraza jipya wa Ofisi hiyo yaliyofanyika jijini Dodoma.

Amewataka wajumbe kutumia fursa hiyo kuzijua hadidu za rejea ambazo zitawaongoza katika utendaji kazi wa kila siku na kutekeleza majukumu katika kipindi chote cha miaka mitatu watakachokuwa wajumbe wa Baraza hilo kuwa nguzo kati ya Baraza na watumishi wengine kwa kuwa Baraza la wafanyakazi ni chombo muhimu mahala pa kazi na kuwa sehemu salama ili kuleta tija katika utendaji kazi wa kila siku wa OWMS na amewataka wajiandae kuhamia Dodoma mwaka huu.

“Mada inayohusu Mkataba wa Baraza la Wafanyakazi ni mahususi kwa ajili ya kujenga uwezo na maarifa ya kujua kilichopo katika mkataba wetu kati ya Menejimenti na Baraza hili ikiwemo matarajio ya OWMS kutoka kwa wajumbe ukizingatia kuwa mkataba huu ni nyenzo muhimu kabisa katika utendaji kazi wetu kwa sababu unaainisha majukumu na mipaka yetu na matarajio kutoka kwa wafanyakazi,” amesema Dkt. Luhende.
Stanley Mahenge (kushoto) na Bi. Frazia Mulokozi (kulia), Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakifuatilia mafunzo kuhusu umuhimu wa vyama vya wafanyakazi mahala pa kazi yaliyotolewa na Samuel Nyungwa, Katibu wa TUGHE wa Mkoa wa Dodoma (hayupo pichani) yaliyofanyika ukumbi wa Takwimu jijini Dodoma.

Akitoa mada ya Umuhimu wa Baraza la Wafanyakazi, Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dodoma, Samuel Nyungwa amesema kuwa ni muhimu kwa kila mtumishi kujiunga na chama cha wafanyakazi kwa sababu ni taasisi pekee ya wafanyakazi ambayo imeundwa kwa ajili ya kulinda na kutetea haki kwa kuweka sawa mahusiano ya kazi kati mfanyakazi na mwajiri wake mahali pa kazi.

“Vyama vya wafanyakazi ni wadau muhimu sana katika kulinda, kutetea haki na maslahi ya wafanyakazi katika kuchangia jitihada za Serikali kuhakikisha kwamba ustawi wa raia wake ambapo ni wafanyakazi unaboreshwa na utendaji kazi unasimamiwa,” amesema Nyungwa.
Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakifuatilia mada zinazotolewa wakati wa mafunzo ya kujenga uelewa kuhusu umuhimu na majukumu ya Baraza hilo yaliyofanyika jijini Dodoma.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Sebastian Innosh amewasilisha mada kuhusu umuhimu na uendeshaji wenye tija wa mabaraza la wafanyakazi ambapo amesema kuwa mabaraza yanatakiwa kushauri na kujadili masuala muhimu ya taasisi; kutumia rasilimali watu na fedha kwa manufaa na uendelevu wa taasisi husika na taifa kwa ujumla; na kuimarisha mahusiano mema na kudumisha amani na utulivu mahala pa kazi.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Rugemarila Rutatina amesema kuwa mkataba wa Baraza la Wafanyakazi unaleta mafanikio na ushirikiano mahala pa kazi kwa kuwa unawaweka pamoja na kuwaleta karibu watumishi mahali pa kazi.
Athumani Zunda, mjumbe mpya wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali akichangia mada ya umuhimu wa Bazara la Wafanyakazi wakati wa mafunzo kwa wajumbe wa Baraza jipya la wafanyakazi wa Ofisi hiyo yaliyofanyika jijini Dodoma.

Akitoa maoni yake wakati wa mkutano huo, Athuman Zunda ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Baraza hilo la OWMS amesema kuwa wamejifunza masuala mbalimbali kuhusu muundo wa Baraza hilo na idadi ya wajumbe wake kwa kuwa yeye ni mjumbe kwa mara ya kwanza kwenye Baraza hilo hivyo wamejifunza na kufurahishwa na namna ambavyo uongozi wa Baraza unavyofanya kazi ikiwa sambamba na suala la mjumbe wa kuchaguliwa kutoruhusiwa kutuma wawakilishi kwa kuwa wamechaguliwa na watumishi wengine ili kuwawakilisha na mjumbe wa kuchaguliwa asipohudhuria vikao vitatu (3) mfululizo bila ya kutoa taarifa kwa uongozi wa baraza atakuwa amepoteza sifa ya kuwa mjumbe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news