Wareno waonesha utayari kuja kuwekeza Tanzania, Waziri Dkt.Tax awapitisha katika fursa

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt.Stergomena Tax amesema Serikali ya Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini ikiwa ni pamoja na kuzifanyia maboresho baadhi ya sheria za usimamizi wa biashara ili kuongeza ufanisi kwa sekta binafsi katika uzalishaji.
Mhe. Dkt. Tax akifungua rasmi Jukwaa la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno lililofanyika Lisbon. Pamoja na mambo mengine Mhe. Dkt Tax alitumia nafasi hiyo kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Ureno kuwekeza nchini.

Mhe. Dkt. Stergomena ametoa kauli hiyo jijini Lisbon wakati akifungua rasmi Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno lililoloandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ubalozi wa Tanzania nchini Ureno na Taasisi ya Biashara na Uwekezaji ya Ureno na kuishirikisha Jumuiya yaWafanyabiashara wa Ureno.

Mhe. Dkt. Tax amesema dhamira kuu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na ufanyaji biashara hususan kwa kuishirikisha ipasavyo sekta binafsi. Amesema tayari Serikali imefanya majadiliano ya mara kwa mara na sekta biafsi ili kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo.

Amesema katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini masuala mbalimbali yanaboreshwa zikiwemo huduma, sheria, miundombinu pamoja na kuishirikisha kikamilifu sekta binafsi ambayo ni muhimu katika kuchangia uchumi wa nchini.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Baiashara na Uwekezaji ya Ureno, Bw.Kuis Castro Henriques naye akiwakaribisha kwenye Ofisi za Taasisi yake washiriki wa Jukwaa la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno.

“Tupo hapa leo ili kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Ureno hususan katika masuala ya biashara na uwekezaji. Tanzania inaendelea kuhamasisha uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji. Katika maboresho hayo ni pamoja na Serikali kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi ili kuiwezesha sekta hii kuwa na ufanisi na kuchangia uchumi ipasavyo,” amesema Dkt. Tax.Balozi wa Tanzania nchini Ureno mwenye makazi yake nchini Ufaransa, Mhe. Samwel Shelukindo (kulia) akishiriki Jukwaa la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno.

Amesema, Serikali inaendelea kuboresha miundombinu kama barabara, bandari, reli, viwanja vya ndege na upatikanaji wa maji na umeme ili kuwawezesha wawekezaji kutopata changamoto zozote pale wanapokuja nchini kuwekeza.

“Serikali imefanya jitihada za makusudi za kuhakikisha miundombinu yote ya msingi kama maji, umeme, barabara, reli, usafiri wa anga na mawasiliano ya simu vinapatikana kwa ngazi tofauti tofauti. Kupitia maboresho haya ni imani yetu wawekezeji watapata ujasiri wa kuwekeza Tanzania na si mahali pengine popote,” amesisitiza Dkt.Tax.
Washiriki wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno wakifuatilia mada zilizowasilishwa kwao.

Amesema, masuala mengine yanayohamasisha uwekezaji, biashara na utalii nchini ni pamoja na ushiriki wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Filamu ya kutangaza Utalii nchini ya The Royal Tour, Sera ya Mambo ya Nje yenye msisitizo katika Diplomasia ya Uchumi ambayo imekuwa chachu katika kuwajengea ujasiri wawekezaji nchini pamoja na ushiriki wa Tanzania kwenye majukwaa mbalimbali ya kimataifa ya biashara na uwekezaji kama Maonesho ya Biashara ya Dubai ya mwaka 2020. 

Vyote hivi vimeipaisha zaidi Tanzania duniani na kuchangia ongezeko la watalii na wawekezaji nchini.

Dkt.Tax alitumia fursa hiyo pia kuwakaribisha wawekezaji na wananchi wa Ureno kwa ujumla kutembelea Tanzania ili kujionea vivutio mbalimbali vya utalii huku akiwahamasisha kuangalia Filamu ya Utalii ya Royal Tour ambayo ameilezea kuwa ni ya aina yake kwani mhusika mkuu katika Filamu hiyo ni Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waziri wa Nchi wa Ureno anayeshughulikia masuala ya Biashara na Uwekezaji, Mhe. Bernardo Ivo Cruz naye akizungumza wakati wa Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Ureno.

Kwa upande wake, Waziri anayeshughulikia Biashara na Uwekezaji wa Ureno, Mhe. Bernardo Ivo Cruz amepongeza ziara ya Mhe. Dkt. Tax nchini humo akisema imekuja wakati mwafaka ambao wakati dunia ikiendelea kushuhudia changamoto mbalimbali za kiuchumi, Tanzania na Ureno zinaangalia namna ya kushirikiana katika biashara na uwekezaji ili kujikwamua kiuchumi.

“Tanzania ni mshirika wetu muhimu katika biashara na uwekezaji na tupo tayari kuimarisha ushirikiano huu. Nakupongeza Mhe. Waziri kwa kufanya ziara katika kipindi hiki na tunaahidi kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali ya uwekezaji ikiwemo Kilimobiashara, Uchumi wa Bluu, Miundombinu na Sekta zingine za uwekezaji” alisema Mhe. Cruz.

Pia aliongeza kusema nchi yake inao Mpango wa miaka sita wa ushirikiano katika biashara na uwekezaji kuanzia mwaka 2021-2027 ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazonufaika na mpango huo.
Mkurugenzi wa Uwekezaji na Biashara kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. Revocatus Rasheli akinadi fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji zilizopo nchini kwa washiriki wa Jukwaa hilo. 

Akiwasilisha mada kuhusu Fursa za Uwekezaji zilizopo nchini kwa washiriki wa Jukwaa hilo, Mkurugenzi wa Biashara na Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. Revocatus Rasheli amewahamasisha wawekezaji na wafanyabiasha kutoka Ureno kuchangamkia fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji nchini huku akisema tayari anayo mkononi miradi 100 chini ya Sekta ya Umma na miradi 36 chini ya Sekta Binafsi ambayo ipo tayari na kwamba ni kiasi cha wawekezaji hao kuchagua na kuwekeza.

Aliongeza kusema Tanzania katika kuhamasisha uwekezaji imetenga ardhi yenye ukubwa wa Hekta milioni 1.6 kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo ambapo tayari Hekta 6,000 zipo mkoani Morogoro kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo.
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme (wa pili kulia) akiwa na Brigedia Jenerali Mbaraka Mkeremy wakifuatilia Jukwaa la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno.

Pia alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji hao kuwekeza kwenye sekta ya utalii ikiwa ni pamoja na kujenga Hoteli, Nyumba za Makazi na Kumbi za Mikutano.

“Serikali ya Tanzani ainazo fursa nyingi za uwekezaji. Nawakaribisha kuwekeza kwenye kilimo, uvuvi, madini, miundombinu lakini pia ujenzi wa hoteli, nyumba za makazi na kumbi za mikutano hususan katika miji mikuu ikiwemo Dar es Salaana na Makao Makuu ya Nchi yetu Dodoma ambako mahitaji ni makubwa zaidi,” alisisitiza Bw. Rasheli.

Kadhalika, Mkurugenzi huyo amesema Ureno ni mdau muhimu katika ushirikiano na Tanzania na kwamba ipo haja ya kuongeza biashara kati ya nchi hizi mbili ambapo amesema hadi sasa Ureno imesajili miradi 13 nchini yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni Tisa ambayo imetoa fursa za ajira 325 kwa watanzania.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwa kwenye mazungumzo rasmi na Waziri wa Nchi wa Ureno anayeshughlikia masuala ya Biashara na Uwekezaji, Mhe. Bernardo Ivo Cruz mara baada ya kuwasili kwenye Makao Makuu ya Ofisi za Taasisi ya Biashara na Uwekezaji za nchi hiyo zilizopo jijini Lisbon. Akiwa katika taasisi hiyo, pamoja na mambo mengine Mhe. Dkt. Tax alifungua rasmi Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno ambalo liliishirikisha Jumuiya ya Wawekezaji kutoka nchini humo. Mhe. Waziri Tax na yupo nchini Ureno kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia tarehe 20 hadi 22 Oktoba 2022.

“Ziara hii ni muhimu sana kwetu Tanzania na Ureno, ni imani yetu kuwa ziara hii itaongeza wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Ureno kuja nchini ili kwa pamoja nchi hizi zinufaike kupitia ushirikiano mzuri uliopo,” alisisitiza Bw. Rasheli.

Naye Mkurugenzi wa Utafiti na Mipango wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanziabar (ZIPA) Bw. Emmanuel Mashimba amesema Serikali ya Zanzibar inaendelea kuweka mazingira wezeshi katika kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara na kwamba Ureno ni miongoni mwa nchi muhimu ambazo Zanzibar ipo tayari kushirikiana nazo katika sekta za uchumi wa bluu, utalii na miundombinu.
Mhe. Dkt. Tax yupo nchini Portugal kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia tarehe 20 hadi 22 Oktoba, 2022. Akiwa nchini humo, Mhe. Dkt. Tax pamoja na mambo mengine atakutana kwa mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Joao Gomez Cravinho pamoja na kusaini Hati ya Makubaliano ya kuanzisha Majadiliano ya Kisiasa kati ya Tanzania na Ureno.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news