Waziri Dkt.Mabula atoa mwezi mmoja mapitio kesi za ardhi

NA MUNIR SHEMWETA-WANMM

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula ameagiza ufanyike upembuzi kwa mashauri yote ya ardhi yaliyokaa muda mrefu kutokana na sababu zisizo na mashiko.Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula (wa pili Kulia) pamoja na Katibu Mkuu, Dkt.Allan Kijazi (wa pili kushoto) pamoja na viongozi wengine wa wizara wakiwasili kwenye kikao kazi baina ya Kitengo cha Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya na Chama cha Wnasheria Tanganyika (TLS) kilichofanyika jijini Dodoma Oktoba 6, 2022. 

Amemtaka Msajili wa Mabara ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya, Stella Tullo kusimamia agizo hilo kwa kumpatia taarifa mapema mwezi Novemba, 2022.

Aidha, alimtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Allan Kijazi kuangalia kwa jicho la tatu Mabaraza yote ya Ardhi ya mkoa wa Dar es Salaam kwa kuwa kumekuwa na malalamiko mengi ya mrundikano wa kesi za muda mrefu.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akifungua kikao kazi baina ya Kitengo cha Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kilichofanyika jijini Dodoma Oktoba 6, 2022.

Dkt.Mabula alitoa agizo hilo Oktoba 6, 2022 wakati wa Kikao kazi cha Kitengo cha Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kilichofanyika jijini Dodoma.

Dkt.Mabula amesema,Serikali inatambua umuhimu na michango ya mawakili katika kuvisaidia vyombo vya utoaji haki na kuwakumbusha mawakili suala la maadili ya kiutendaj hasa kwa baadhi ya wajumbe kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Kwa mujibu wa Dkt.Mabula, uzoefu unaonesha mashauri mengi yanayowakilishwa na mawakili ndiyo yenye kuchukua muda mrefu kumalizika.

‘’Mshauri mengi ya ardhi katika mabaraza hayapewi kipaumbele na Wakili anaweza kupanga tarehe ya kesi ambayo kwa siku hiyo ana mashauri katika vyombo vingine vya kutoa haki,"amesema.
Sehemu ya washiriki wa Kikao Kazi baina ya Kitengo cha Mbaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kilichofanyika jijini Dodoma Oktoba 6, 2022.

Waziri wa Ardhi aliongeza kwa kusema kuwa, uchunguzi wa awali unaonesha pia baadhi ya mapingamizi yana dhamira ya kupoteza muda hususan yale mashauri yanayohusu taasisi za fedha.

‘’Mashauri mengi yanayofunguliwa na wananchi walioshindwa kurejesha mikopo kwa wakati au kukiuka mikataba ya mikopo, wananchi wanakimbilia kwenye mabaraza kwa kushauriwa na mawakili,’’amesema Dkt.Mabula.

Kwa mujibu wa Dkt.Mabula, ucheleweshaji mashauri kwa sababu zozote zile ni kuchelewesha kupata haki kwa wakati na kutoa rai kwa mawakili kuona umuhimu wa kuunga mkono juhudi za serikali kwa kutumia nafasi zao kama maafisa wa mahakama kwa nia ya kuhakikisha mashauri ya ardhi yanamalizika kwa wakati na kwa haki kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Allan Kijazi akizungumza katika kikao kazi baina ya Kitengo cha Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) jijini Dodoma Oktoba 6, 2022.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Allan Kijazi alisema, wizara yake imeitisha kikao cha pamoja na mawakili wa kujitegemea kwa lengo la kuhakikisha mashauri ya ardhi katika mabaraza yanasikilizwa na kumalizwa kwa wakati.

‘’Mawakili wa kujitegemea mnapotekeleza kwa uadilifu uaminifu na weledi jukumu lenu la kuwakilisha wananchi katika mashauri mnawarahisishia wenyeviti wa mabaraza ya ardhi kazi ya kusikiliza na kutoa maamuzi kwa wakati kwani uwakilishi wenu kwa namna moja ama nyingine unatoa dira mapema ya kufahamu mwananchi yupi ana haki na yupi hana haki katika shauri husika,"alisema Dkt.Kijazi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akizungumza na Jaji Mfawadhi wa Mahakama Kuu, Abdi Kagomba (katikati) wakati wa kikao kazi baina ya Kitengo cha Mabaraza ya Ardhi na Nyumba na Wilaya kilichofanyika Oktoba 6, 2022 jijini Dodoma. Kushoto ni Wakili Msomi Ally Nkangaa. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI).

Kikao Kazi cha Kitengo cha Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kina lengo la kupata uelewa wa pamoja, kupokea changamoto wanazokutana nazo katika mabarza ya ardhi pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya Wizara na TLS katika kutatua kero za wananchi nwenye mashauri ya ardhi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news