Waziri Dkt.Ndumbaro:Wadau wa habari ongezeni kasi, Rais Samia ameonesha nia njema

NA MWNADISHI WETU

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) na wadau wa habari nchini wametakiwa kupambana kwa hali na mali ili kuhakikisha sheria za habari ambazo zinaonekana kuwa kikwazo katika tasnia hiyo zinafanyiwa marekebisho

Hayo yamesema na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro alipokutana na uongozi wa TEF na Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI) hivi karibuni jijini Arusha.

Mheshimiwa Waziri amesema, kama kuna wakati mzuri wa kulisukuma suala la kubadili sheria za habari ni sasa.

“Rais tuliye naye sasa, Mheshimiwa Samia (Suluhu Hassan) ameonesha moyo na nia kubwa ya kutetea na kutoa haki za vyombo vya habari na waandishi wa habari nchini.

“Kwa sasa mazingira ni mazuri na yanaruhusu. Lisukumeni suala hili sheria zibadilishwe sasa hivi, maana mkisubiri miaka 10 ijayo, huwezi kujua atakayekuja baada ya hapo atakuwa na mtazamo gani juu ya vyombo vya habari,”amesema Dkt.Ndumbaro.

Rais Samia tangu aingie madarakani mwanzoni mwa mwaka jana aliudhirishia ulimwengu kuwa, tasnia ya habari ni muhimu kwa ustawi bora wa maendeleo ya jamii na Taifa.

Aidha, alianza kwa kuitaka Wizara ya Habari kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa huko nyuma huku akisisitiza wahusika wafuate sheria, jambo ambalo lilifanyiwa kazi hatua kwa hatua.

Pia, alitaka kanuni ziweke wazi makosa na adhabu zake ili kusiwe na ubabe kwa kuwa Serikali inaamini katika uhuru wa vyombo vya habari nchini.

“Nasikia kuna vyombo vya habari mlivifungia, vifungulieni, lakini wafuate sheria na miongozo ya Serikali, wafungulieni tusiwape mdomo wa kusema tunaminya uhuru wa vyombo vya habari, na kanuni ziwe wazi tusifungie vyombo vya habari kibabe,” Rais Samia aliagiza Aprili, mwaka jana katika hafla ya kuwaapisha makatibu na manaibu makatibu wakuu wa wizara mbalimbali Ikulu jijini Dar es Salaam.

Aidha, miezi kadhaa baadaye Rais Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo ya kufanyiwa marekebisho sheria za habari ambazo zinaonekana kuwa kikwazo katika taaluma hiyo.

Mheshimiwa Rais Samia aliyasema hayo Mei 3, mwaka huu wakati akiwahutubia Wadau wa Vyombo vya Habari kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ikiongozwa na kauli mbiu ‘Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti' katika ukumbi wa Gran Melia Hotel jijini Arusha.

“Nimeelekeza sheria zirekebishwe, lakini kwa majadiliano pande zote na si tu kwamba sisi tunataka nini. Nimemwelekeza Waziri sheria za habari zirekebishwe kwa kushirikisha wadau wote,"alielekeza Mheshimiwa Rais Samia.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Waziri Dkt.Ndumbaro amekubaliana na hoja ya TEF na wadau kuwa suala la Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) nchini kuwa na mamlaka ya kuwa mlalamikaji, mwendesha mashitaka, mtoa hukumu na msimamizi wa hukumu aliyoipitisha linafifisha misingi ya utawala bora na utawala wa sheria hivyo hili ni moja ya mambo yanayopaswa kubadilishwa.

“Hili la dispute settlement (utatuzi wa migogoro), linahitaji uwazi mkubwa. Kuna hatari kubwa katika kuweka madaraka yote kwenye chombo kimoja (Mkurugenzi wa Idara ya Habari/MAELEZO…) nafahamu sheria ililenga ku-balance conflicting interests (kuweka mlinganyo kwa masilahi yanayogongana), maana serikali zote duniani huwa zinawaza kudhibiti. Serikali yoyote duniani ina wivu sana na mamlaka yake. Kitendo cha kugawa sehemu ya mamlaka yake huwa hakipendwi, ila kutenganisha mamlaka ndiyo utawala bora,”amesema.

Hata hivyo, amesema kwa nia ya kusimamia na kuhakikisha haki inatendeka, ndiyo maana kilianzishwa chombo kama Mahakama ambayo ina jukumu la kusikiliza kila upande wenye malalamiko na kuamua nani anastahili haki ipi, hivyo akasema mamlaka ya kufungia chombo vya habari hayapaswi kuwekwa kwenye mikono ya mtu mmoja.

Vyombo vya habari vipo katika mazungumzo na Serikali kuomba Sheria ya Huduma za Habari, MSA 2016 irekebishwe katika vifungu vinavyofifisha Uhuru wa Vyombo vya Habari kikiwamo kifungu cha 9(a) kinachompa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) mamlaka ya kufungia vyombo vya habari bila kupitia utaratibu wa kuwasilisha malalamiko popote au pande zote mbili zilizo katika mgogoro kusikilizwa.

Jukwaa la Wahariri Tanzania na wadau, wanapendekeza mamlaka haya ya Mkurugenzi yafutwe na kiundwe chombo ambacho pamoja na mambo mengine kitashughulikia masuala ya usuluhishi yanapotolewa malalamiko dhidi ya chombo cha habari, badala ya kazi hiyo kufanywa na mtu mmoja.

Sheria nyingine zinazolalamikiwa ni Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Huduma za Posta (EPOCA, 2010), Sheria ya Makosa Mtandaoni (2015), Sheria ya Haki ya Kupata Habari (2016) na Kanuni za Maudhui Mtandao (2018) kama zilivyorekebishwa mara kadhaa. Sheria hizi zina vifungu vinavyofifisha uhuru wa habari nchini hivyo zinahitaji kubadilishwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news