WAZIRI MKUU AELEZEA DHAMIRA NA NIA YA RAIS SAMIA KUWAHUDUMIA WATANZANIA

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuhakikisha inawahudumia Watanzania kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi inayowagusa wananchi.

Waziri Mkuu amesema kuwa katika kuhakikisha anatekeleza hayo, Mheshimiwa Rais Samia ameendelea kufanya ziara katika maeneo mbalimbali nchini ili kuona utekelezaji wa miradi pamoja na kutatua changamoto kwenye sekta mbalimbali za kimaendeleo.

“Ndugu zangu watumishi wa umma fedha hizi zinazotolewa na Rais wetu kwa ajili ya kutekeleza miradi hii ya kimaendeleo ni lazima ziendee kutekeleza miradi hiyo, na ni muhimu tuisimamie miradi hii ili thamani ya fedha ionekane kwenye miradi hiyo, nawasisitiza muwe na weledi na uadilifu wa hali ya juu.”
Ameyasema hayo Oktoba 18, 2022 alipokuwa akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, katika ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa ni matamanio ya Rais Samia kuona kila Mtanzania ananufaika na miradi inayotekelezwa na Serikali, hivyo Watanzania waendelee kumuunga mkono ili aweze kufanikisha malengo aliyojiwekea katika kuwaletea Watanzania maendeleo. “Ni lazima sasa watumishi wa umma wahakikishe miradi hii inatekelezwa na kukamilika”.

“Leo Mheshimiwa Rais baada ya kumaliza ziara yake katika mikoa ya Kagera na Geita, sasa yuko katika mkoa wa Kigoma. Haya yote yanaonesha namna Mheshimiwa Rais amejitoa kuwatumikia Watanzania.”

Akizungumza na Watumishi wa wilaya ya Namtumbo Waziri Mkuu amewataka viongozi wa Mkoa na wilaya kuchukua hatua kwa wafanyakazi wa kitengo cha manunuzi cha wilaya hiyo kwa kushindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo na kuisababishia hasara Serikali, kwa kukwamisha miradi iliyotolewa fedha na Serikali katika miradi hiyo.

Waziri Mkuu amesema taarifa alizonazo zinaonesha kuwa idara ya manunuzi inawatumia sana kampuni ya PLM Stores kufanya kazi zao na kupandisha bei za bidhaa na amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo waache mara moja kuitumia kampuni hiyo.

“Mkurugenzi hii kampuni hakuna kuitumia tena kufanya manunuzi. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya itupieni macho, na mfuatilie.”

Amewataka watumishi hao wafanye ziara vijijini na wahakikishe vikao vya kisheria katika ngazi ya Kijiji vinafanyika. Pia amewataka wahakikishe makusanyo ya fedha yanafanyika kwa kufuata taratibu na kanuni. “Fedha zikikusanywa ziende benki mara moja, siyo mnazikusanya halafu mnasema tumepata dharura halafu mnazitumia,” amesisitiza.

Kuhusu hoja za ukaguzi unaofanywa na Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Fedha za Serikali (CAG), Waziri Mkuu amewataka wakamilishe hoja zilizobakia na kuzifuta. “Taarifa ya CAG inaonesha mlikuwa na hoja 61, mmekamilisha nyingine lakini bado hoja 27 hazijaisha. Ukiuliza utakuta mtu anadaiwa risiti. Suala la risiti linachuku siku ngapi? Iweje mtu adaiwe risiti wakati zinatolewa za EFD?,” alihoji.

Kuhusu usimamizi wa mazingira, amewatala wahakikishe wanapanda miti ili kukabiliana na mahitaji ya kwenye kilimo cha tumbaku.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news