Serikali yadhamiria makubwa elimu ya watu wazima nchini

NA GODFREY NNKO

SERIKALI imesema itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali nchini ili kuhakikisha inafikia malengo yake ya kuwa na Watanzania walioelimika na wenye uwezo wa kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 19, 2022 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bi.Rehema Madenge kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Prof.Riziki Shemdoe katika ufunguzi wa Kongamano la Juma la Elimu ya Watu Wazima.

Kongamano hilo limefanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) jijini Dar es Salaam ambapo, Bi.Madenge alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Prof.Shemdoe.

"Ndiyo maana Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo imekuwa ikitekeleza proramu na mipango mbalimbali ya elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi kwa lengo la kuwa na Watanzania walioelimika na wenye uwezo wa kushiriki katika shughuli za maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla;

Bi.Madenge amefafanua kuwa, mipango na programu za elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi inayotekelezwa ni pamoja na Mpango wa Elimu Msingi kwa Waliokosa (MEMKWA), Mpango wa Elimu ya Sekondari kwa njia Mbadala (AEP).
Pia amesema, kuna Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana Walio Nje ya Shule (IPOSA),Mpango wa Uwiano kati ya Elimu na Jamii (MUKEJA), Uzalishaji Mali (UMALI),Shughuli za Ugani (SU) na VIKOBA (Village Community Bank).

Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima kwa mwaka 2022 ambayo pia yanajumuisha maonesho katika viwanja vya DUCE yanaongozwa na kauli mbiu ya "Kuboresha mazingira ya kujifunza kusoma na kuandika yatakayozingatia ubora, usawa na ujumuishi wa makundi yote".

Bi.Madenge amebainisha kuwa, kauli mbiu hiyo inatoa uwanda mpana kwa washiriki katika kongamano hilo kutafakari, kutathimini na kuweka mikakati ya kuboresha shughuli za utoaji wa elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi hapa nchini.

"Ni matumaini yangu kuwa, tutaweza kubadilisha mitizamo juu ya mipango, uendeshaji, usimamizi, ufuatiliaji na tathimini ya elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi ili kuendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwak 2025 sambamba na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030 hasa katika lengo namba nne ambalo ni mahsusi kwa maendeleo jumuishi ya kisomo na elimu kwa umma,"amesisitiza Bi.Madenge.
Lengo namba 4.6 linataka ifikapo mwaka 2030 vijana na watu wazima wote kwa maana ya wanaume kwa wanawake wafikie kiwango cha kujua kusoma, kuandika na kuhesabu.

Pia amewaeleza washiriki wa kongamano hilo kuwa, Serikali inatarajia kupata mrejesho wa maazimio ya majadiliano yatakayofikiwa ili kuisaidia kuja na afua stahiki zitakazoleta ufanisi katika utoaji wa elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi.

Miongoni mwa mada zinazojadiliwa katika kongamano hilo ni dhana ya falsafa ya elimu ya watu wazima jumuishi katika karne ya 21,usimamizi na uratibu shirikishi wa elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi.

Nyingine ni kujenga uwezo wa usimamizi na uendeshaji wa elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi,upimaji sahihi wa stadi, maarifa, ujuzi na mafanikio ya elimu ya watu wazima katika hali halisi ya maisha.

Mada nyingine ni maandalizi ya vitabu vya programu za elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi na zana za kujifunzia na kufundishia kwa kuzingatia mazingira halisi ya jamii ikiwemo mada ya mchango wa wadau mbalimbali katika utekelezaji wa programu za elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi.

Kamishna wa Elimu

Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Kamishna wa Elimu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika kongamano hilo, Mwalimu Venance Manori amesema kuwa, maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima yamekuwa yakifanyika kila mwaka katika ngazi ya Kitaifa, mkoa au wilaya kwa kushirikisha taasisi mbalimbali zinazotekeleza programu za elimu ya watu wazima.
"Mwaka huu maadhimisho haya Kitaifa yanafanyika kuanzia Oktoba 17 hadi 21, 2022 katika viwanja hivi vya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE),"amesema Manori.

Amesema, lengo kuu la maadhimisho hayo ni kuimarisha ushirikiano miongoni mwao pamoja na kupata sauti kwa pamoja kuhusu umuhimu wa elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi kwa jamii.

"Hivyo, ninaamini kongamano hili litaongeza ufanisi na kujenga uelewa wa pamoja miongoni mwa wadau na jamii nzima ya Watanzania,"amesema Manori.

Walikotoka

Pia amesema,miaka ya 1980, Tanzania ilifikia rekodi ya kushuka kwa kiwango cha kutojua Kuandika, Kusoma na Kuhesabu (KKK) kutoka asilimia 80 mwaka 1961 hadi kufikia asilimia 9.6 mwaka 1986.

"Hii ilikuwa miongoni mwa viwango vya juu zaidi duniani. Hali hii ilitokana na jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali za kuondoa changamoto ya kutojua KKK ikiwemo kuanzisha programu za Kisomo (KCK na KCM) na kufanya kampeni za kuelimisha umma kama vile Kazi ni Uhai, Kupanga ni Kuchagua, Uhuru na Kazi.
"Wakati wa Furaha, Uchaguzi na Wako, Mtu ni Afya na nyinginezo. Kwa sasa, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na UNESCO kiwango cha watu wazima wanaojua kusoma, kuandika na kuhesabu ni asilimia 77.89 hali ambayo si mbaya sana, lakini nchi imerudi nyuma ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

"Hivyo, natoa rai kwa watendaji kutumia kongamano hili kuendelea kuweka mikakati thabiti ya kuondoa changamoto hii ya kutojua KKK nchini.

"Ni dhairi kuwa, Taifa lenye watu walioelimika ni rahisi kuleta maendeleo yatakayoweza kubadili maisha ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla,"amesema.

Mikakati

Manori amefafanua kuwa, ili kukabiliana na changamoto ya kushuka kwa kiwango cha wanaojua KKK, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeandaa mpango mkakati wa miaka mitano kwa kipindi cha mwaka 2020 /2021 hadi 2024/2025 ambao umelenga kukuza na kuendeleza Kisomo na Elimu kwa umma (MTaKEU).

"Amebainisha kuwa, mkakati huu uliandaliwa kwa makusudi kama nyenzo ya kuongoza wadau mbalimbali ambao wanatekeleza programu za kisomo.

"Mpango huu unatambua kisomo kama haki ya msingi kwa maendeleo ya mtu binafsi, kijamii, kiuchumi na kisiasa,"amesema Manori kwa niaba ya Kaimu Kamishna wa Elimu.
Pia amesema, wizara imeandaa miongozo mitano ambayo itasaidia katika utekelezaji wa kuimarisha ubora wa utolewaji wa Elimu ya Sekondari kwa Njia Mbadala (SEQUIP).

Amesema, mpango huo umelenga kuwapa fursa ya kuendelea na masomo vijana walio nje ya mfumo rasmi hususani wasichana waliopata ujauzito.

"Katika kipindi cha 2021 jumla ya wasichana 3,333 walijiunga na programu hii katika vituo 131 nchi nzima, haya ni baadhi ya mambo yaliyofanywa na Serikali, kwa hiyo ninawaasa wadau wote kutumia kongamano hili kujadili na kuangalia namna ya kuboresha mazingira ya ujifunzaji katika programu ya kisomo yanayozingatia ubora, usawa na ujumuishi wa makundi yote,"amesema.
Hata hivyo, Juma la Elimu ya Watu Wazima (EWW) huadhimishwa Kimataifa kila mwaka ifikapo Septemba 8 kwa lengo ka kujenga uelewa na kutambua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo katika jamii na Dunia kwa ujumla.

Maadhimisho hayo yaliasisiwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) mwaka 1966 kwa lengo la kuikumbusha jamii kuhusu umuhimu wa elimu ya watu wazima kama suala la heshima na haki za binadamu.

Post a Comment

0 Comments