Wizara yaongeza siku kusikiliza migogoro ya ardhi jijini Dodoma

NA GODFREY NNKO

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Allan Kijazi amesema, wizara yake imeamua kuongeza siku tatu za kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi kuhusu Sekta ya Ardhi.

Ameyasema hayo Oktoba 3, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya Kamati ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi iliyofanya kazi kuanzia Septemba 26 hadi Septemba 30, 2022 jijini Dodoma.

‘’Zoezi la Dodoma lilifanyika kuanzia Septemba 26 hadi Septemba 30, 2022 na katika zoezi hilo tulitegemea kwamba siku tano zingetutosha katika kusikiliza hiyo migogoro, lakini hadi kufikia Septemba 30, 2022 tulikuwa tumepokea malalamiko 806 na malalamiko haya mengine yalikuwa yanahitaji ufafanuzi wa kina na kuna wananchi walikuwa wanalalamika kwamba hawakupata nafasi ya kusikilizwa.

"Kutokana na hali hiyo, tumeona kwamba ni vyema tuongeze siku za kusikiliza migogoro ya wananchi kwa eneo la Kizota, Nkuhungu na Nara hivyo tumepanga kwamba zoezi hili litaendela Oktoba 17,2022 kuanzia saa mbili mpaka saa 10:00 jioni na wananchi wa maeneo hayo malalamiko yao yatasikilizwa katika ofisi za Kata ya Kizota.

"Na wananchi wa maeneo ya Mnadani na Miyuji malalamiko yao tutasikiliza Oktoba 18,2022 kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa 10:00 jioni. Tunawaomba wafike katika ofisi za Kata ya Miyuji kwa ajili ya kuwasilisha malalamiko yao.

"Na wananchi wa eneo la Mtumba Chahwa na Ibara tunawapa fursa ya kuwasilisha malalamimo yao Oktoba 19, 2022 kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 10:00 jioni na hawa tutawasikiliza katika ofisi ya Kata ya Chahwa,"amesema Dkt.Kijazi.

Katibu Mkuu amesema, zoezi hilo wameliongezea siku tatu kutokana na kwamba malalamiko bado ni mengi yanayohusiana na sekta hiyo.

"Lakini pia kuna haja ya wataalamu wetu kabla ya kutoa mrejesho kwa baadhi ya malalamiko kutoa elimu, kufanya ukaguzi, kufanya mahojiano hii itatusaidia kuweza kutatua migogoro hii kwa haki bila upendeleo wowote. Baada ya kumaliza zoezi la Dodoma tutaendelea na zoezi katika mikoa mingine,"amesema Dkt.Kijazi.

Dar

Wakati huo huo, Dkt.Kijazi amesema, wanaendelea kufanyia kazi matokeo ya ripoti iliyowasilishwa kwake hivi karibuni na kamati ya wataalamu aliyoipa jukumu la kupokea na kusikiliza malalamiko ya wananchi jijini Dar es Salaam.

‘’Kwa upande wa Dar es Salaam, tumepokea malalamiko 386 uchambuzi wa kina umefanyika, baadhi ya malalamiko yameshatolewa uchambuzi,baadhi ya malalamiko tunachambua nyaraka mbalimbali kabla ya kutoa maamuzi. Kwa wale wananchi ambao bado hawajapata mrejesho wasifikirie kwamba malalamiko yao hayajafanyiwa kazi.

‘’Yapo baadhi ya malalamiko kama yanahusu pande mbili au tatu...tunakutanisha pande zote kusikiliza ili kutoa uamuzi sahihi, lakini tukiri nimekuwa nikipokea simu na meseji toka kwa wananchi kwamba hawakupata taarifa za jambo hili, ni imani yangu kwamba baada ya kutoka Dodoma tutakuja kumalizia Dar es Salaam ili wale ambao hawakupata taarifa waje kuleta malalamiko yao.

‘’Tutakachofanya safari hii, tutatoa taarifa hii hata wiki mbili kabla ili wananchi watambue na utakapofika wakati huo tutawaita tena mje mtusaidie kuwahabarisha wananchi.

"Migogoro ambayo tunaisikiliza ni ile tu ambayo haipo kwenye mihimili ya sheria, mingine ipo mahakamani, kwenye mifumo ya sheria, labda tu kuwe na uthibitisho mlalamikaji yeye kwa hiari yake alikwenda kuiondoa katika mfumo wa sheria,’’amesema Dkt.Kijazi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news