Watajwa kuchochea migogoro ya ardhi Dar es Salaam na Dodoma

NA GODFREY NNKO

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imesema kuwa,migogoro mingi ya ardhi jijini Dodoma na Dar es Salaam imesababishwa na watu kuhamia maeneo ya wengine bila kufuata taratibu, kanuni na sheria.

Hayo yamesemwa Oktoba 3, 2022 jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt.Allan Kijazi wakati akitoa taarifa ya Kamati ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi iliyofanya kazi kuanzia Septemba 26 hadi Septemba 30, 2022 jijini Dodoma.

"Changamoto ya uvamizi wa viwanja au mashamba imekuwa ni changamoto kubwa sana katika nchi yetu na hii imechangiwa na baadhi ya waliopewa maeneo hayo kutofuata taratibu za uendelezaji.

"Unakuta mtu aliomba shamba akapewa shamba au eneo limekaa tu, wananchi wakaona eneo limekaa, anakwenda mwaka wa kwanza anaweka kibanda...hakuna anayejitokeza, anaweka tena kibanda haoni mtu mwisho wake anaweka kibanda cha kuku hakuna anayejitokeza hatimaye anaweka ghorofa mwenye kiwanja akishituka anakuta ghorofa limesimama.

"Nitoe rai kwa wale wote waliopewa maeneo kwa maana ya kumilikishwa wayaendeleze na wahakikishe maeneo yao ni salama ili kupunguza migogozo kwa serikali, eneo jingine la pili ambalo limekuwa chanzo cha migogoro ni elimu duni kwa wananchi kuhusu sheria, kanuni na miongozo mbalimbali kuhusu sekta ya ardhi.

"Wananchi wengi wamekuwa wakinunua ardhi bila kufuata sheria, unakuta kuna wajanja wachache wanaelewa hizo sheria, lakini wanatumia huo mwanya kuwalaghai wananchi ambao hawajui sheria na mwananchi anapokuja kuelewa anakuta tayari ameshajifunga kwenye mikataba ambayo tayari ni vigumu kutoka kwa wepesi,"amesema Dkt.Kijazi.

Katibu Mkuu huyo ametoa wito kwa wananchi huku akiwataka wajitahidi kufuata sheria, taratibu na kanuni na miongozo mbalimbali inayohusu masuala ya umilikishwaji wa ardhi ili kukwepa kitanzi cha wajanja wachache wanaowalaghai wananchi na kuuza maeneo yao kinyume na taratibu.

"Tunaelewa kuna changamoto ya uelewa, sisi kama wizara tumejipanga kuimarisha utoaji wa elimu kwa wananchi ili waweze kujua taratibu mbalimbali za ardhi, lakini kabla ya kufika huko nitoe wito kwa wananchi kabla hajaingia kwenye makubaliano yoyote ya ununuaji au uuzaji wa ardhi apate ushauri wa wataalam wetu wa ardhi walioko maeneo yetu.

"Ili ahakikishe utaratibu anaoufanya haumuumizi yeye na baadaye kuja kulalamika kwa kitu ambacho kinaweza kuwa ni kigumu kubadilishwa kwa ajili ya taratibu kukiukwa,"amesema Dkt.Kijazi.

Katika hatua nyingine amesema kuwa, eneo jingine ambalo limekuwa likichangia sana migogoro ya ardhi ni udanganyifu wa wale wanaojiita madalali wa ardhi.

Dkt.Kijazi amesema, kuna watu wamekuwa wakidanganya wananchi hivyo wanakwenda kuuza maeneo wakidai wamepewa idhini na wamiliki kuyauza au maeneo ni ya kwao kumbe hakuna ukweli wowote.

‘’Wakati wale wenye maeneo wanapokuja kubainisha yale maeneo ni ya kwao na yameuzwa unakuta wale wauzaji wameshatoroka, anayenunua anajikuta hana haki mwenye eneo naye anadai eneo ni la kwake anatuingiza sisi serikali kwenye mchakato ambao usingekuwa lazima kama mwananchi angekuwa makini.

"Jambo lingine, nikiri kwamba kumekuwa na changamoto ya kiutendaji, baadhi ya watendaji wetu wamekuwa si waadilifu, waaminifu nimesikia kuna changamoto ya viwanja kuuzwa mara mbili mbili au ramani kukosewa hii pia imechangia migogoro sana,"amefafanua Dkt.Kijazi.

Amesema, wizara inaandaa utaratibu mzuri ikiwemo kuangalia mianya na mpango mzima wa kutoa maamuzi kuanzia hatua ya kwanza hadi ya mwisho ili kubaini ni wapi watendaji wamekuwa wakitumia aidha kwa makusudi au kwa kutokuelewa na kusababisha migogoro.

Dkt.Kijazi amesema, lengo la kufanya hivyo ni ili kuziba mianya hiyo na kuhakikisha kwamba watendaji wa sekta hiyo hawawi chanzo cha migogoro ya ardhi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news